Barua ya Wazi kwako Mheshimiwa Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam

Salaam Kaka. Ni matumaini kuwa ni mzima wa afya na unaendelea kulitumikia taifa. Naomba niwasilishe barua hii, nikitambua wazi kuwa inawezekana kabisa usijibu, au jibu likatufedhehesha zaidi nafsi zetu. Nimefunga na kusali leo kuomba hata kama ni kulisemea hili, basi iwe kwenye maneno ambayo hayatopokelewa kama shambulizi na wala lisije kuendeleza mlolongo wa visasi kama wengi wamekua wakiniaminisha. After all, mimi ni mkazi wa mkoa wako, if anything that should count for something. Allow me to tell like it is, as I believe I always do.

Naamini ni haki yangu kama Mtanzania kusema pale ninapoona sijatendewa haki, na si mimi tu, naandika kwa niaba ya wafanyakazi 33 wa Nyama Choma Festival na watoa huduma, wafanyabiashara na washiriki wote zaidi ya 200 waliokua wanategemea kwa kiasi kikubwa tamasha hili lililokua linafanyika mara 3 kwa mwaka mkoani kwako.

Ni siku nyingi tangu ofisi yako imesikia kutoka kwetu, yaani Waandaji wa Tamasha la Nyama Choma Festival, tangu tulivyokuja mwanzoni mwa mwaka huu (March 2018) na kusisitiziwa na ofisi yako tukufu kuwa bado uamuzi ni ule ule kuhusu matumizi ya Leaders Grounds.

Rejea tamko lako la tarehe 24.11.2017 https://youtu.be/nZDug8mQP- ambapo ulitangaza kupiga marufuku matukio yanayoenda zaidi ya saa 12 jioni kufanyika viwanja vya Leaders Club. Ulisisitiza kuwa ulitoa ruhusa maalum kwa watayarishaji wa Tamasha la Fiesta kwa sababu maalum lakini ulisema na nanukuu ‘ni haki ya watu kwenye makazi hayo kulala’. Ulitoa rai kuwa ni kutokana na makazi ya watu na ubalozi kwenye eneo.

Tamko hili lilitolewa wiki moja kabla ya tarehe iliyopangwa na kutangazwa kufanyika tamasha letu la nyama choma festival. Tulipatwa na mshtuko mkubwa sana ukizingatia kuna fedha nyingi sana ambazo tayari tulikua tumeshaingia gharama kwenye maandalizi na zisingeweza kurejeshwa.

Rejea barua yetu tuliyokuandikia Desemba 2017 kuomba kama inawezekana na sisi kupewa kibali maalum, kwa masharti kama waliyopewa wenzetu wa Fiesta ya mwisho saa 6 Usiku (ingawa waliruhusiwa kupiga mziki hadi asubuhi). Nikukumbushe tu pia, tamasha letu halina tofauti sana na hilo la wenzetu waliloruhusiwa kwani letu pia huambatanisha burudani ya muziki ingawa main concept ni Nyama Choma za kila aina na biashara mbali mbali.

Tulifuatilia jibu wiki nzima ofisini kwako huku tukiwataarifu wateja wetu kuwa inabidi tuahirishe tamasha hadi pale ambapo tungepata mbadala. Majibu tuliyopewa sihitaji kukumbusha kwani naamini utakua unayakumbuka fika.

Nilipoona jitihada hizi hazijibiwi, ilibidi niombe msaada kwa kila ninayemfahamu aliye karibu na wewe atoe appeal on my behalf. Hili pia liligonga mwamba. Kwanza mmoja alinijibu kuwa hata hunifahamu. Naomba nikukumbushe mimi ni yule yule Carol tuliyokua tuna mawasiliano ya salaam, na pia ni yule yule niliyokuhoji kwenye kipindi cha siasa za siasa one on one wakati ukiwa Mkuu wa wilaya ya Kinondoni kwa lisaa lizima. Pia ni yule yule anayehusika na kutayarisha hili tamasha ambalo ulihudhuria 5 Desemba 2017 kama picha inavyoonyesha hapa

Hili tamasha la 5 Desemba lililofanyika Leaders lilikua la huzuni pia kwani wakati wa tamasha tulimpoteza mshiriki wetu, mhudhuriaji na supporter mkubwa sana wa tamasha letu, alikua kama mama yetu pia. Rest in Peace Mama Mzungu. Wakati tunashirkiana na kikosi cha polisi kutoa mwili na kuupeleka Muhimbili ulikuwepo na ulikua unasisitizia kama kuna lolote nahitaji kama msaada nikwambie. Sijui kama haya matukio ni kumbukizi tosha, mimi ni yule yule.

Nilijibiwa vitu tofauti,kuna wengine walisema kabisa ‘Carol, hapa pagumu sana’.Wengi walikuwa wananiuliza ‘kwani umemkosea nini’. Kitu ambacho hakikua kwenye kumbukumbu yangu kabisa kwani hata tuhuma zozote zilizokua zinasemwa juu yako hata kipindi kile cha ‘identity crisis’ sikuwahi kutia neno. Nilijihoji sana na kuwauliza wote niliokua nao karibu kama wana kumbukumbu yoyote. Mmoja alinijibu hivi…

Mwisho, nilipigwa simu saa 2 usiku, bahati mbaya nilikua nimeshalala kutokana na kusumbuliwa sana na Pressure wiki hiyo lakini asubuhi nilikutana na Ujumbe huu .

Nilipo mpigia simu Kaka yangu Lemutuz, kwanza alinitaarifu na ‘kunikanya’ kama Kaka. Alisema kuwa Umeniruhusu kwenda kufanya Tanganyika Packers na nifanye taratibu za kibali. Huwezi kuniruhusu kufanya Leaders kwani umeshatoa tamko na kama kiongozi ukitengua utaonekana hauna msimamo. Nilimshukuru kwa taarifa na kumwambia nitaanza taratibu za kupata uwanja wa Tanganyika Packers.

Hata hivyo kama wengine, nilimuuliza kama anafahamu kama nimewahi kukukosea, kwani hata nilivyoenda ofisini kwako sikuruhusiwa kukuona, jambo lililo si la kawaida ukizingatia utayari wa kiongozi wetu wa mkoa kuonana na wananchi wake kila siku.

Nilihoji ili kama ni kosa, niombe msamaha kwani mimi ni binadamu na si timilifu. Kaka Lemutuz alisema yeye hafahamu na akasema pia ‘kwanza amesema hata hakufahamu na wewe umekua caught kwenye cross fire tu’, nikamkumbusha hilo tamasha la 5 Desemba 2017 kwani walikua wote, na nilivyoenda kuwasabahi na kuwakaribisha kwenye tamasha walikua wamesimama wote. Akasema ‘anyway, inabidi uangalie sana unachoongea, you look like you are anti-government, mimi nakufollow twitter naona unavyoongea, am just telling you to be wise’.

Nilimshukuru kwa ushauri na kumwambia nitamtaarifu taratibu zinaendaje kupapata Tanganyika Packers. Hili pia lilikua na changamoto, na hadi tarehe 8 Desemba asubuhi, siku moja kabla ya tamasha kufanyika Tanganyika Packers tulikua hatujapewa kibali. Hatimaye kilitolewa na tukaendelea na tamasha. Halikua zuri kabisa. Rejea ‘Barua kwako Mjasiriamali unayeanza’ ambayo nilielezea changamoto tulizokutana nazo.https://medium.com/@CarolNdosi/barua-kwako-mjasiriamali-unayeanza-2e0b71d100

Mhe. Paul Makonda, naandika hii barua kwa kuwa nimetaarifiwa kuwa sasa viwanja vya leaders vinatumika tena, na utenguzi wa tamko umefanya wewe mwenyewe. Ni mwaka mzima sisi kama waandaji tumesitisha shughuli zetu za tamasha kwani ingawa tunafanya mikoa mingine, Dar es Salaam ndio ilikuwa inatuwezesha na kutupa mtaji wa kwenda huko kwingine.

Nilivyosikia tangazo la kwanza la wenzetu,wakitangaza kuwa tamasha lao linafanyika pale pale Leaders nilipata mchanganyiko wa hisia. Kwanza nilifurahi maana nilisema hatimaye, na kama wenzetu wameruhusiwa basi na sisi tutaruhusiwa. Lakini mara baada ya hapo nikapatwa na fedheha, nilipowakumbuka vijana wangu wote na watoa huduma waliokua wanatutegemea, kuwa wamekosa kipato kwa mwaka mzima.

Ni haki yangu kuuliza na kupewa sababu ambazo zimepeleka utenguzi huu na kama kuna mabadiliko yoyote ya sababu ulizotupa uliposema Leaders Grounds Hapafai. Ni ngumu kutokuamini utenguzi umefanyika coincidentally wakati wenzetu wamepanga tamasha lao. Ubinadamu unanifanya nihoji Je sisi la kwetu halina thamani au mchango wowote? Wao hawapigi mziki? makazi ya watu yamehamishwa Leaders sasa? Nawaelewesha vipi wenzangu kuwa haikua personal vendetta, au mimi ndio nilishindwa ‘kuget through’. Kama ni kunyanyua vipaji hata sisi tunanyanyua, kama ni kodi hata sisi tunalipa, na sio sisi tu, wote wanaoshiriki kwenye mnyororo wa thamani wa tamasha hili. Kama ni ajira na fursa, hata sisi tunatoa kupitia tamasha hili. Kwanini ilibidi tuteseke mwaka mzima kama mazingira hayajabadilika?

Nimeambiwa hata mimi nikitaka kufanya sasa naruhusiwa..bahati mbaya tumechelewa sana kwani wadhamini wengi wameshafunga vitabu vyao na bila ya wao hatutaweza kufanikisha.

Nimesali sana kuwa tuweze kuendelea mwaka 2019 na hii ruhusa bado iwepo na tuweze kufanya tamasha kwa amani na kurudisha chanzo kingine cha ajira na vipato kwa mamia ya watu.

Yangu yalikua haya machache, na kama nilivyojihami, sitarajii jibu. Langu lilikua kukueleza tu jinsi ambavyo tuliathirika na tamko lako, na hisia zetu baada ya utenguzi mwaka huu. Pia kukusihi tu kuwa ingawa tunaweza kupishana mitazamo na mawazo, tunajitahidi sana kupitia nyanja mbali mbali kusukuma gurudumu la maendeleo nchini kwetu. Mimi kama Mtanzania najivunia sana nchi yangu and I remain loyal to my purpose which is to contribute to this country’s development. Mimi sio ADUI. Ni mwananchi mwenzako, ni Mama, ni mtoto, ni dada and most importantly, ni BINADAMU.

Naomba Bwana Yesu, Malaika wake na Roho Mtakatifu wakaseme na wewe, wakuonyeshe uchungu tuliopitia. Mwisho nikutakie uongozi mwema wa Mkoa wetu wa Dar, na ushiriki mwema kwenye tamasha linalokuja, natumai na sisi tukikukaribisha mwakani Insh’allah, utajumuika na sisi na kutuunga mkono kama wenzetu.

Namalizia na bandiko kutoka kwa Operations Manager wa Nyama Choma Festival- labda maneno yake pia yataleta mwanga zaidi kwenye hili.