#BlockMtatiro #UnfollowMtatiro: Msaliti Huyu Atapata Tabu Sana

Moja ya dhamira kuu za Magufuli ni kuua upinzani. Na hilo lilikuwa moja ya mambo ambayo yalitupa wasiwasi baadhi yetu tulioshiriki kumnadi katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Alianza kwa kuharamisha shughuli za kisiasa za vyama vya upinzani, kwa kupiga marufuku mikutano na maandamano ya vyama hivyo. Awali, sie tuliokuwa tunamuunga mkono tulijifariji kwamba “ana hoja ya msingi. Watanzania wanahitaji maendeleo na si mikutano ya siasa au maandamano.”

Hata hivyo, ukweli kwamba zuio hilo lilikuwa dhidi ya vyama vya upinzani tu huku CCM wakiruhusiwa sio tu kuendelea na shughuli za kisiasa bali pia kutumia raslimali za umma katika shughuli hizo, uliashiria kuwa Magufuli ana ajenda kubwa zaidi ya hiyo ya “maendeleo kwanza, shughuli za kisiasa baadaye.”

Lakini wanaomfahamu Magufuli kabla hajawa Rais, na hasa waliokuwa naye wakati wa kampeni zake mwaka 2015 wanaeleza kuwa mara kadhaa alisikika akitoa kauli za kuogopesha dhidi ya wanasiasa wa upinzani na vyama vyao Inaelezwa kuwa mara kadhaa alisikika akitamka “si muwauwe tu” dhidi ya wanasiasa wa upinzani ambao kwa mtazamo wa chama tawala,CCM, walionekana kama wakorofi.

Halafu sijui kwanini moja ya matukio ya kutisha na kusikitisha mno katika siasa za Tanzania, mauaji ya kinyama ya kada maarufu wa Chadema, Kamanda Mawazo, yaliyotokea takriban wiki moja tu baada ya Magufuli kuingia madarakani hayajawahi kuhusishwa na utawala wake unaoendeshwa na chuki dhidi ya Upinzani.

Baada ya tukio hilo la kinyama, yaliyojiri yalizidi kuthibitisha kuwa Magufuli yule aliyetupatia matumaini tele — hadi baadhi yetu kufikia hatua ya kuandika kitabu kilichosheheni pongezi kwake siku 56 tu tangu aingie madarakani — sio tu alikuwa na dhamira ya kuangamiza upinzani bali pia kukandamiza uhuru wa habari na uhuru wa kujieleza.

Orodha ya yaliyojiri ni ndefu sasa, lakini miongoni mwa matukio makubwa ni pamoja na “kupotea” kwa kada maarufu wa Chadema, Ben Saanane, ambaye alikuwa akimkosoa Magufuli hadharani PhD yake, na baadaye jaribio lililofeli la kumuuwa kiongozi maarufu wa Chadema, Tundu Lissu, aliyekuwa mkosoaji mkubwa wa Magufuli.

Na tangu wakati huo hadi sasa Watanzania wameshuhudia mengi yanayoashiria waziwazi kuwa Magufuli ni dikteta. Lakini pengine kinachompa jeuri zaidi ni ukweli kwamba hadi sasa hakuna jitihada za makusudi za angalau kumfanya atambue kuwa Watanzania hawaungi mkono udikteta wake.

Huku akiukandamiza kwa nguvu zote, Magufuli ameokea kunogewa na mbinu chafu ya kununua wanasiasa wa upinzani na kuwaingiza CCM. Wengi wao ni madiwani na wabunge kadhaa.

Hata hivyo, pengine mwanasiasa ambaye kuhama kwake kutoka upinzani sio tu kumetushangaza bali pia kumetusikitisha na kutuudhi ni kwa aliyekuwa kiongozi wa moja ya kambi mbili za chama cha CUF, Julius Mtatiro.

Awali niliposikia habari za kuhama kwake, nilihisi kuwa “labda njaa yake tu”

Lakini baadaye nilipata taarifa kwamba inawezekana uamuzi huo wa Mtatiro ulitokana na yeye “kufanyiwa kitu mbaya” iliyopelekea uwepo wa “kompromat” dhidi yake.

Awe amehama kwa sababu ya “kompromat” au njaa zake tu, Mtatiro atakumbukwa katika historia kama kigeugeu, msaliti na tapeli wa kisiasa.

Lakini kwa uapnde mwingine, na kama nilivyoandika kwenye kichwa cha habari, Mtatiro atapata tabu sana angalau as long as Watanzania wataendelea kukumbuka na kuibua matamko yake mbalimbali dhidi ya Magufuli, CCM na serikali yake.

Mtatiro anakuwa mwanasiasa wa kwanza kabisa mtumiaji mahiri wa mitandao ya kijamii kuwa “mhaga wa tabia ya mtandao wa intaneti kutosahau.” Na tayari kuna jitihada kubwa za “kufukua makaburi” yaani kuibua matamka ya nyuma ya mwanasiasa huyo tapeli. Baadhi ya matamko yake ni haya hapa chini

Ushahidi wa usaliti,unafiti,ubabaishaji, utapeli (you name it) wa Mtatiro upo tele mtandaoni.Na ndio maana nimeeleza kuwa “atapata tabu sana.”

Lakini pengine jambo jingine linaloweza kumsumbua sana Mtatiro ni kampeni ambayo binafsi nimeshiriki kuiasisi nikiwataka wote waliokerwa na utapeli wake kum-unfollow

Na kampeni hiyo imeshika kasi kiasi cha kuwa habari kwenye gazeti la The Citizen

Japo hatuwezi kumlazimisha Mtatiro abadili uamuzi wake au aache utapeli huo wa kisiasa, kwa hakika tunaweza kumwonyesha hasira zetu kwa kum-unfollow au kumbloku kokote kule mtandaoni.