CATCH 22: CDM Ikisusa, CCM Itakula. Isiposusa, CCM “itaila” CDM .

Kuna hali inaitwa “Catch 22” ambapo kwa tafsiri rahisi katika Kiswahili ni kama “ukinipiga unanionea, usiponipiga unaniogopa,” au “usiposhuka nshale, ukishuka nshale.” Ni hali ambapo kufanya au kutofanya kitu kuna madhara.

Na “Catch 22” inaweza kutumika sawia kueleza ugumu wa kimaamuzi unaovikabili baadhi ya vyama vya upinzani nchini Tanzania, hususan chama kikuu cha upinzani, Chadema.

Pengine ni muhimu kurejea nyuma kidogo kuelewa kwanini baadhi ya vyama vya upinzani vinakabiliwa na “Catch 22.” Kwa kifupi, tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, haki za kikatiba za vyama vya upinzani — hususan haki za kidemokrasia za kuviwezesha kufanya shughuli zao za kisiasa kwa ufanisi — zimekuwa zikitolewa kama fadhila badala ya kuwa stahili yao.

Kwa tunaofuatilia siasa za Tanzania, tangu kuruhusiwa kwa mfumo wa vyama vingi, vyama vya upinzani vimejikuta vikilazimika kuomba ruhusa ya kufanya shughuli za wazi kwa chama chochote cha siasa, kama vile mikutano ya ndani au nje, na maandamano.

Lakini hata kama haki hiyo ya kikatiba kwa vyama hivyo ingekuwa ni fadhila, kinachosikitisha zaidi ni pale chama tawala CCM kinapokuwa na uhuru wa kufanya chochote inachotaka, iwe mikutano au maandamano, na wakati mwingine hata kuvifanyia vurugu vyama vya upinzani. Lakini mamlaka husika hufumbia macho.

Wakati mgumu zaidi kwa vyama vya upinzani ni katika chaguzi. Kila uchaguzi mkuu kuanzia ule wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995 hadi huu wa mwaka juzi 2015, hali imekuwa ile Waingereza wanasema sio “level field,” ambapo chama tawala kimekuwa kikipendelewa waziwazi huku vyama vya upinzani vikikandamizwa waziwazi pia.

Kwenye chaguzi ndogo — iwe za udiwani au ubunge — hali huwa mbaya zaidi, pengine kwa vile chaguzi hizo ndogo hazigusi hisia ya waangalizi wa kimataifa.

Uchaguzi mdogo wa madiwani kuelekea mwishoni mwa mwaka jana utabaki kwenye vitabu vya kihistoria kama mzaha wa kisiasa na uhuni mkubwa dhidi ya demokrasia.

Ni katika mazingira hayo — na nimeyaeleza kwa ufupi mno, vinginevyo yanaweza kumliza mtu yeyote anayependa kuona haki inatendeka — vyama vya upinzani vimejikuta vikikabili na “Catch 22.” Kwa upande mmoja, kwa mwenendo ulivyo, na hali inavyozidi kuwa mbaya, je vyama vya upinzani viendelee kushiriki katika chaguzi ambazo ni wazi sio huru wala za haki hata kabla hazijafanyika? Jibu la haraka ni HAPANA. Sio tu kwa vile kushiriki kwao kutahalalisha “uhuni” wowote utakaojitokeza katika uchaguzi husika, lakini pia uwezekano wa kushinda — katika mazingira ya uonevu wa waziwazi - ni kama haipo.

Lakini vyama hivyo vikigoma kushiriki — kama ilivyokuwa kwenye chaguzi ndogo za hivi karibuni — haitoizuwia CCM kupewa ushindi “wa kiulaini.” Kwamba idadi ya wapiga kura inaweza kuwa ndogo mno kwa vile vyama vya upinzani vimesusia, kwa CCM na Tume ya Taifa ya Uchaguzi cha muhimu ni ushindi kwa chama hicho tawala.

Imeshuhudiwa majuzi ambapo Chadema ilisusia chaguzi ndogo za hivi karibuni, idadi ya wapigakura ilikuwa ndogo mno lakini hiyo haikizuwia Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwatangaza wagombea wa CCM kuwa washindi, na wala haikuizuwia CCM kujigamba kutokana na matokeo hayo.

Na kwa vile Watanzania ni wasahaulifu wazoefu — hali ambayo imeambukizwa kwa vyama vya upinzani — zile “kelele” za vyama vya upinzani kuhusu “uhuni” uliofanywa dhidi yao kwenye uchaguzi mdogo wa madiwani, na sababu zilizopelekea baadhi ya vyama hivyo kususia chaguzi ndogo za ubunge za hivi majuzi, zimetokomea kusikojulikana.

Pengine vyama vya upinzani havina njia nyingine ya kukabiliana na mazingira mabovu kabisa yaliyotengezwa kitambo dhidi yao. Pengine vinategemea miujiza flani, kwamba ghafla hizo “mbinde” zote dhidi yao zitapotea.

Kilicho bayana ni hiyo “Catch 22.” Wakisusia chaguzi, CCM watashinda “kiulaini.” Wakishiriki, wataishia kufanyiwa “uhuni” wa mchana kweupe, na watashindwa, hasa kwa sababu mazingira yaliyopo ni “piga ua, mgombea wa CCM lazima ashinde.”

Ni katika mazingira hayo sijapata jawabu sahihi kuhusu uamuzi wa Chadema kususia chaguzi ndogo tatu zilizopita, na kuamua kushiriki mbili zijazo. Je sababu zilizowapelekea kususia chaguzi hizo tatu zimebadilika kwenye chaguzi mbili zijazo?

Sote tunajua jibu la swali hilo: mazingira yaleyale ya “uhuni wa kihistoria” katika chaguzi ndogo za madiwani mwaka jana, na mazingira yaleyale ya chaguzi ndogo tatu za ubunge, ndio mazingira hayohayo yatayotawala chaguzi mbili ndogo za ubunge. Je ni busara kwa vyama vya upinzani, hususan Chadema, kushiriki uchaguzi huo?

Je kwa mazingira yalivyo, kuna uwezekano wowote kwa vyama vya upinzani kuibuka mshindi kwenye majimbo hayo mawili?

Jana niliona picha za wafuasi wa Chadema wakiwa na mgombea wao katika uchaguzi mdogo ujao jimbo la Kinondoni, Salum Mwalimu, wakiwa na hamasa kubwa. Nilifarijika kuona mwanasiasa huyo na wafuasi wake wakitwa na “uhuru adimu” wa kufanya shughuli ya kisiasa bila kubughudhiwa. Lakini pia nilijiskia uchungu kwa namna flani.

Nilijiskia uchungu kwa sababu, unless kutokee miujiza flani, mgombea wa CCM, Maulid Mtulia, aliyejivua ubunge alioupata kwa tiketi ya CUF, kabla ya kupoteza ubunge baada ya kuhama chama hicho na kuhamia CCM, na — kama mchezo wa kuiguza — akapitishwa na chama hicho tawala kuwa mgombea wake kwenye uchaguzi huo mdogo, ndiye mwenye nafasi kubwa ya kushinda.

Naamini kuna watakaokerwa na “ubashiri” huu, na ninatambua mazingira magumu ninayojiwekea kwa kubashiri waziwazi kuwa mgombea wa CCM atashinda, lakini ukweli una tabia moja muhimu: kuuchukia hakuufanyi kugeuka uongo.Na ukweli ni kwamba mazingira yaliyopo yanampendelea mgombea huyo wa CCM.

Na ukweli huo ndio unaoweza kutufanya kuhoji busara za Chadema kushiriki uchaguzi huo. Ikumbukwe tu kwamba CCM itawekeza kila kitu kwa Mtulia, kwa sababu asiposhinda, itakuwa aibu ya karne kwa chama hicho tawala.

Najua makada wa Chadema sio tu watapingana na mtazamo wangu huu lakini kuna wanaoweza kwenda mbali zaidi na kunitukana (kama sio kudhamiria kunitoboa macho kwa bisibisi haha). Lakini naamini kwamba baada ya uchaguzi huo mdogo, watanielewa tu.

Chadema nayo inapaswa kufanya kila iwezalo ishinde jimbo hilo linalowaniwa tena na Mtulia, kwanza kwa sababu itakuwa ni adhabu mwafaka kwa kila “msaliti” anayehama kutoka upinzani na kisha kutengewa nafasi ileile aliyoiacha akiwa Upinzani, na pili ukweli kwamba mgombea wao, Mwalimu, ni kiongozi wa kitaifa wa chama hicho. Akishindwa, wadhifa wake wa Unaibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar unaweza kuwa shakani.

Nihitimishe makala hii kwa kupigia mstari vitu viwili. Kwanza, ninaamini Chadema wanafahamu fika kuwa uamuzi wao wa kususia chaguzi ndogo tatu na sasa kuamua kushiriki katika chaguzi ndogo mbili unajenga taswira ya chama hicho kutokuwa na msimamo. Salama yao ni ushindi. Wakishindwa, sio tu watanyooshewa vidole lakini kelele za “ymeuonewa” zitakuwa hazina maana -hazitobadili matokeo, na wanajua bayana muda huu kuwa wataonewa katika chaguzi hizo lakini wameamua kushiriki hivyohivyo.

Pili, na hili ni la msingi zaidi, Chadema inapaswa kuamka na kurejea zama zile chama hicho kikuu cha upinzani kilikuwa sauti halisi ya wanyonge na mbadala tarajiwa wa CCM. Chadema iliyoilazimisha serikali ya CCM kupora baadhi ya sera ambazo mwanzoni chama tawala kilizipinga, kwa mfano Katiba mpya.

Ndio, mazingira ni magumu, lakini hakuna wakati tangu mfumo wa siasa za vyama vingi uanzishwe mwaka 1992 ambapo mazingira yalikuwa mepesi kwa vyama hivyo. In fact, mazingira magumu yaliyopo yanawea kabisa kuwa “yanaficha” mapungufu ya kiungozi ndani ya Chadema. Lakini ni muhimu kutambua kuwa hakuna mabadiliko yanayopatikana kwa kulalamika tu, kupiga kelele tu au kuonyesha hasira tu. Si mkoloni wala Nduli Idi Amin walioondoka kwa sie kulalamika tu , au kuwapigia kelele tu au kuonyesha hasira dhidi yao.

Kama alivyosema aliyekuwa Katibu Mkuu wa chma hicho kabla hajabwaga manyanga mwaka 2015, Dkt Willbrord Slaa, “kunahitajika mkakati makini utakaohusisha watu makini.” Unfortunately, kwa sasa hakuna kitu kama hicho. Pasipo jitihada za makusudi, uchaguzi mkuu ujao mwaka 2020 utashuhudia matokeo mabaya mno kwa chama hicho na upinzani kwa ujumla.

Kama kuna tatizo la kuchagua suala gani lipewe kipaumbele, ushauri wangu ni kurejesha upya vuguvugu la kudai Katiba mpya. Kumkemea Nkamia na ndoto zake za miaka saba ya urais, ilhali kutofanya jitihada zozote za kudai Katiba mpya ni suala lisilopendeza.

Nawatakia siku njema