Heri Ya Mwaka Mpya 2018: Ubashiri Kuhusu Mwaka Huu kwa Tanzania

Heri ya mwaka mpya 2018.

Kwa takriban miaka 10, nilikuwa na utaratibu wa kukaribisha mwaka mpya kwa kuandika makala maalum yenye ubashiri kuhusu mambo ya kutarajiwa katika mwaka mpya husika. Makala hizo zilikuwa zikichapishwa katika magazeti niliyokuwa nikiyaandikia, lakini mwaka jana niliamua kustaafu uandishi wa makala magazetini na badala yake nitajikita kwenye nyenzo nyingine za mawasiliano kama hii Medium, Spreaker, blogu yangu ya Kulikoni Ughaibuni, Twitter, Facebook, nk.

Japo ubashiri huo hujumuisha maeneo mbalimbali, msisitizo mkubwa huwa kwenye masuala ya siasa. Na bila kupoteza muda, twende moja kwa moja kwenye ubashiri kuhusu hali ya siasa nchini Tanzania kwa mwaka huu 2018.

Kwa bahati mbaya — au pengine makusudi — hakutarajiwi kuwepo mabadiliko yoyote chanya kwenye siasa za Tanzania ambazo kwa takriban mwaka mzima uliopita zilitawaliwa zaidi na uhasama kati ya chama tawala CCM na chama kikuu cha upinzani Chadema.

Kimsingi, uhasama huo ulikuwa zaidi ya CCM na Chadema, kwani kama ilivyozoeleka, taasisi mbalimbali za serikali hususan za dola, pia zilielemea upande wa CCM dhidi ya Chadema. Kwahiyo pengine namna sahihi ya kueleza hali ilivyokuwa ni “uhasama baina ya CCM + Serikali vs Chadema.”

Na uhasama huo ulikuwa wa upande mmoja. CCM kwa kutumia nafasi yake kama chama tawala ambacho mwenyekiti wake wa Taifa, John Magufuli, ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano, ilifanya unyanyasaji na ukandamizaji wa wazi wa demokrasia dhidi ya vyama vya upinzani.

Kwa baadhi yetu ambao tumeshuhudia siasa za upinzani nchini Tanzania tangu zilipozaliwa mwaka 1992, uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995, na chaguzi kuu zilizofuata mwaka 2000, 2005, 2010 na 2015, hakuna wakati ambapo vyama vya upinzani vilikuwa huru kufanya shughuli zake bila kubughudhiwa na CCM au serikali zake (ya Muungano na ya Zanzibar).

Kuna hisia zilizotawala mwaka jana kwamba “haijawahi kutokea kwa vyama vya upinzani kunyanyaswa na CCM/Serikali kama wakati huu.” Dhana hiyo sio sahihi. Si kwamba hakuna unyanyasaji bali uliopo ni mwendelezo tu.

Na kwa bahati mbaya — au makusudi — hali hiyo isiyopendeza inatarajiwa kuendelea mwaka huu mpya 2018. Na huenda ikawa ile wanayosema kwa kimombo “from bad to worse.”

Kwa upande mmoja, CCM ni mnufaika mkubwa wa ukandamizaji wa demokrasia ikiwa ni pamoja na unyanyasaji, hujuma, na wakati mwingine uhuni dhidi ya vyama vya upinzani. Tuwe wakweli, ni nani katika “Uswahili” wetu ambaye anaweza kuwa tayari kuwaruhusu wapinzani wake watekeleze majukumu yao bila vikwazo, kisha wapinzani hao wajitengenee mazingira mazuri ya kukung’oa madarakani?

Kwa mantiki hiyo, kinachofanywa na CCM dhidi ya vyama vya upinzani sio cha kushangaza japo hakipendezi. Ni kasumba iliyoota mizizi katika nchi nyingi za Dunia ya Tatu ambazo, hususan zile zilizopokea wimbi la mabadiliko ya kisiasa/uchumi mwanzoni mwa 1990s.

Kwa upande mwingine, na hili ni tatizo sugu, takriban vyama vyote vya upinzani vina “chembechembe” za u-CCM ndani yake. Kabla ya kuruhusiwa mfumo wa vyama vingi, Tanzania ilikuwa nchi ya chama kimoja. Na kwa tuliokuwa na ufahamu wa kinachoendelea wakati huo, ilikuwa kama suala lisilowezekana kutokuwa mwanachama wa CCM na/au jumuiya zake.

Kwa maana hiyo, takriban viongozi wote wa upinzani waliwahi kuwa wana-CCM. Hilo si tatizo sana laiti “u-CCM” wao wa zamani ungekuwa umewatoka “damuni.” Ukweli mchungu ni kwamba kuna idadi kubwa tu ya wanasiasa wa upinzani ambao kimwili wapo Upinzani lakini kiroho wapo CCM.

Na hali hii inakuwa mbaya zaidi kutokana na vyama vya upinzani kuwa mikono wazi kuwakaribisha wanasiasa kutoka CCM, hata kama ni “makapi.” Lakini hili sio suala la kukimbilia kuvilaumu vyama vya upinzani kwamba “vinawababaikia wanasiasa wanaohama CCM.”

Ukweli ni kwamba takriban vyama vyote vya upinzani ni vichanga, na katika jitihada zake za kukua havina budi kukaribisha watu wengi — ikiwa ni pamoja na “makapi” kutoka CCM — na miongoni mwao kuna “waliojiunga kwa ajenda zao binafsi.”

Lakini adui mkubwa anayetafuna vyama vya upinzani ni “nguvu za giza” kwa maana ya hujuma zinazofanyika kwa siri dhidi ya vyama hivyo bila vyenyewe kuelewa. Hizi ni hujuma kutoka nje ya vyama hivyo. Lakini pia kuna hujuma zinazofanyika ndani ya vyama kwa maelekezo kutoka nje ya vyama hivyo. Huu ndio mtihani mgumu zaidi kwa vyama vya upinzani kwani baadhi ya watu wanaoaminika mno katika vyama hivyo wanashiriki kuvihujumu.

Tuendelee kuangalia yanayotarajiwa kujiri mwaka huu 2018. Zoezi la “hama hama” kutoka vyama vya upinzani kwenda CCM litaendelea, na ninabashiri kwamba kasi ya kuhama itaongezeka kwa kasi kadri mwaka “unavyozidi kukomaa.” Kasi hiyo ya viongozi wa upinzani kuhamia CCM inatarajiwa kufikia “hatua ya kutisha” kadri uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 unavyokaribia (na sasa imebaki miaka miwili na miezi 10 hivi)

Vilevile ninabashiri kwamba “jitihada za kuuwa upinzani” zitachukua sura ya kisheria, kwa maana kama tulivyoshuhudia hujuma dhidi ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, akiandamwa na baadhi ya taasisi za serikali, basi itarajiwe kuwa viongozi wengi zaidi watakumbwa na hali hiyo. Miongoni mwa viongozi maarufu wa upinzani wanaoweza “kuandamwa” ni pamoja na mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye, na mwana-CCM wa zamani aliyejiunga na Chadema hivi karibuni, Lazaro Nyalandu.

Kamata kamata ya viongozi wa upinzani inatarajiwa kuendelea, sambamba na jitihada za “kuwashawishi wafuasi wa upinzani kwamba ni suala hatari kuwa na ukaribu na vyama vya upinzani.” Badala ya kunadi sera zake ili kuwavutia wafuasi wa upinzani, inatarajiwa kuwa CCM itategemea zaidi mkakati wa vitisho na manyanyaso kwa kila mwananchi anayejihusisha na upinzani, ili ifike mahala ionekane kwa “njia pekee ya kuwa salama katika Tanzania ni kujihusisha na CCM.”

Kwa upande wa chama tawala CCM, inatarajiwa kuwa Magufuli ataendelea kujitengenezea mazingira ya kuwa na nguvu kubwa zaidi katika chama hicho. Inatarajiwa kuwa kiongozi huyo atafika mahala ambapo nguvu zake za uongozi zitakaribiana na alizokuwa nazo Baba wa Taifa, Marehemu Julius Nyerere.

Kadhalika, kuna uwezekano wa Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana kutoka madarakani (kwa amani) na nafasi yake kuchukuliwa na “mtu wa karibu wa Magufuli,” huenda kutoka Kanda ya Ziwa.

Vilevile chama hicho tawala kinatarajiwa kushinda kila uchaguzi utakaofanyika mwaka huu. “Haitojalisha” kama vyama vya upinzani vitashiri au vitasusia chaguzi hizo. Ni muhimu kutambua kuwa pamoja na kukandamizwa na kinyanyaswa, vyama hivyo vya upinzani navyo vina mapungufu yake .

Kwa upande wa Chadema, inatarajiwa kuwa kitaendelea kuhujumiwa huku baadhi ya viongozi wake wakihama na kwenda CCM. Ni muhimu kutambua kuwa pamoja na uwezekano mkubwa kuwa wanasiasa wanaohama kutoka upinzani na kwenda CCM “wananunuliwa,” lakini kwa kiasi kikubwa siasa za Tanzania ni ajira, na sio ajira tu bali ya kuaminika.

Sasa ukichanganya na jinsi “vyuma vilivyokaza” inakuwa sio jambo la ajabu kuona baadhi ya wanasiasa huko upinzani wakitamani bora wangekuwa “upande mwingine.”

Na ni rahisi kuwalaumu watu wanaopiga kikumbo itikadi kwa sababu ya “kuhakikisha njia ya msalani haioti nyasi” a.k.a “kuhakikisha mkono unaenda kinywani,” lakini pengine ukirudi nyuma kidogo na kujiuliza, “hivi chama changu cha Chadema (kwa mfano) kinasimamia ajenda ipi hasa?” unaweza kubaini kwanini ni rahisi mtu “kutekeleza itikadi kwa sababu ya njaa.” I mean, ili mtu aweze kutetea itikadi basi shurti iwepo kwanza.

Inatarajiwa kuwa Chadema, kama inavyotarajiwa kwa vyama vingine vya upinzani, itaendelea kuendeshwa na matukio badala ya kuwa na ajenda zinazoweza kulivutia kundi muhimu katika chaguzi za Tanzania, yaani wale wasiofungamana na chama chochote.

Kama namna chama hicho kilivyoshughulikia suala la kada wake Ben Saanane ambaye haijulikani alipo tangu mwishoni mwa mwaka jana, na jaribio la kumuua mbunge wa chama hicho, Tundu Lissu, itaendelea mwaka huu 2018, basi huenda matukio kama hayo yanayohusisha “watu wasiojulikana” yataendelea.

Kwa kifupi, Chadema haikupaswa kuitegemea serikali ikisaidie chama hicho katika suala la Ben na la Lissu. Sio kwamba chama hicho kilikosea kuiomba serikali kupitia vyombo vya dola ifanye uchunguzi, lakini ni kama “kutwanga maji kwenye kinu” kumtarajia “mtu unayemtuhumu kukuloga awe sehemu ya kutafuta tiba ya mgonjwa.” Katika uhusiano mbaya kabisa kati ya chama hicho na jeshi la polisi, hakuna uwezekano wowote ule kwa jeshi hilo kuwa na msaada katika kutafuta ufumbuzi wa matukio hayo mawili.

Moja ya matukio yanayoweza kujitokeza huko Chadema ni “chokochoko”za kudai demokrasia zaidi, ambapo Mwenyekiti Mbowe anaweza kukumbwa na shinikizo la kuitisha uchaguzi mkuu wa kuchagua viongozi wapya. Japo CCM inaweza kuwa na “mkono wake” katika shinikizo hilo, haja ya demokrasia zaidi ndani ya chama hicho inaweza kuwa chanzo kikuu cha shinikizo hilo.

Ikitarajiwa kuwa Lissu hatimaye atatoka hospitali na kurejea tena kwenye ulingo wa siasa, yawezekana kujitokeza watakaoona “umuhimu” wa kumwenzi kiongozi huyo kwa kumpatia uongozi wa taifa wa chama hicho. Sio siri kwamba kama kungekuwa na tuzo ya “mwanasiasa mahiri wa mwaka 2017 kwa upinzani” basi tuzo hiyo ingeenda kwa Lissu.

Kwa upande wa Chama cha Wananchi CUF, dalili za ufumbuzi wa mgogoro unaokikabili kitambo sasa, ni ndogo. Tegemeo kubwa la chama hicho ni taratibu za kisheria, na kuna ishara kuwa mahakama imekuwa ikiutendea haki upande “halali” kati ya pande mbili zinazopingana, yaani “CUF- Maalim Seif” vs “CUF-Lipumba.”

Kinachosikitisha zaidi kuhusu mgogoro huo ni jinsi “upande usio halali” wa Lipumba “unavyobebwa waziwazi” na taasisi kama Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Bunge la Muungano. Kwahiyo, moja ya changamoto kwa kambi ya “CUF-Maalim Seif”ni kuhakikisha kuwa maamuzi ya mahakama (yanayounufaisha upande huo) yanatekelezwa na taasisi nyingine.

Kwanini ufumbuzi wa mgogoro huo wa CUF ni muhimu hata nje ya chama hicho? Kwa sababu pindi ikizoeleka kuwa kiongozi anaweza kujiuzulu kwa hiari yake kisha akaamua kujirejesha madarakani kwa nguvu, kama ilivyokuwa kwa Lipumba, basi medani ya uongozi kwa vyama vyetu vya upinzani ambavyo uongozi wake si imara sana itakuwa mashakani.

Kuna uwezekano kwa “sauti za nyikani” huko Zanzibar zilizoanza kusikika zikidai kurefusha muda wa urais visiwani humo kutoka miaka mitano ya sasa hadi saba, kutumia mgogoro wa CUF kuimarisha hoja hiyo. Ifahamike kuwa mafanikio ya hoja hiyo huko Zanzibar yatarahisisha kui- “copy and paste” kwenye urais wa Magufuli.

Kuhusu ACT-Wazalendo, binafsi ninalazimika kukiri kuwa mwenendo wake umepelekea kunipunguzia kuaminika kwangu kama mchambuzi wa siasa za Tanzania. Mara baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, nilifanya ubashiri uliokipa chama hicho fursa kubwa ya kuwa chama kikuu cha upinzani badala ya Chadema.

Kikwazo kikubwa kwa chama hicho kukua zaidi ya kilipo sasa ni ukweli kwamba kwa kiasi kikubwa kimeendelea kuwa “chama cha mtu mmoja,” yaani Kiongozi wake Mkuu Zitto Kabwe. Pasipo kuondoka kwa dhana ya ACT-Wazalendo ni Zitto, na Zitto ndio ACT-Wazalendo, chama hicho chenye sera nzuri kabisa, na kinachoendesha siasa zake kwa umakini, kitaendelea kuwa jina tu.

Moja ya fursa zilizopo kwa chama hicho ni kujaribu kusambaza “mapinduzi ya kiutawala” yanayotokea kwenye halmashauri iliyopo chini ya uongozi wa chama hicho huko Kigoma, na kuyafikisha sehemu nyingine za Tanzania. Najua ugumu wa suala hilo hasa mazoea ya serikali ya CCM kutopenda zuri lolote la Wapinzani lisambae, lakini itabidi Zitto na washauri wake waangalie namna wanavyowea kuitumia turufu hiyo muhimu.

Kwa upande wa NCCR-Mageuzi, kuna uwezekano mkubwa mwaka huu ukashuhudia James Mbatia, mwenyekiti wa taifa wa chama hicho, akilazimika kuachia ngazi kwa sababu binafsi. Sio kama mabadiliko hayo yatabadilisha chochote, lakini nimeona muhimu kuyajumuisha katika ubashiri huu.

TLP ya Agustino Mrema itaendelea kuwa “chama jina” kama ilivyo kwa vyama vingine vya upinzani ambavyo siwezi kupoteza muda kuvitaja.

Katika duru hizo za siasa, kuna uwezekano wa wimbi la “dini kama nyenzo ya mabadiliko ya kisiasa” kushika hatamu. Nakumbuka nilipokuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mhadhiri wetu wa somo la ‘Serikali na Siasa Tanzania’ (Governments and Politics in Tanzania) alitufundisha kwamba “nguvu” mbili kubwa zinazoweza “kulazimisha” mabadiliko ni taasisi za kidini na nchi/taasisi wahisani.

Wakati tunaelekea mwishoni mwa mwaka jana tulishuhudia baadhi ya viongozi wa dini “wakiliamsha dude,” kwa maana ya kuanza kuongelea mwenendo usiopendeza wa siasa za Tanzania. Katika maadhimisho ya sikukuu ya Krismasi, wiki iliyopita, viongozi kadhaa wa Kanisa walitumia mahubiri yao kukosoa ukandamizaji dhidi ya demokrasia na haki za binadamu.

Aliyekwenda mbali zaidi ni Askofu Zakaria Kakobe ambaye bila “kuuma maneno” alimtaka Rais Magufuli atubu dhambi zake kwa kukandamiza demokrasia. Mahubiri wa askofu huyo yamepelea viongozi na makada mbalimbali wa chama hicho “kumcharukia” huko serikali nayo ikionekana kumpa vitisho (kwa Mamlaka ya Mapato TRA kudai itachunguza ulipaji kodi wa Askofu Kakobe na Wizara ya Mambo ya Ndani ikitishia kuyafungia makanisa yanayochanganya “dini na siasa”)

Inabashiriwa kuwa vuguvugu hilo litaendelea. Hata hivyo, kwa vile suala hilo limeanza kuchukua taswira ya “maaskofu vs mashehe” kwa maana ya kwamba tofauti na ilivyozoeleka ambapo viongozi wa Kikristo huwa watetezi wa serikali huku wale wa Kiislamu wakiilaumu serikali kuwa inawabagua na kupendelea Wakristo, mwenendo unaonyesha hali tofauti. Kwa ujumla sauti za kumkosoa Magufuli zinasikika zaidi kutoka kwa viongozi wa makanisa huku sauti za “kumtetea” zikisikika zaidi kutoka kwa viongozi wa Kiislamu.

Hata hivyo, suala hilo linaloweza kuzua matatizo huko mbeleni lisiposhughulikiwa kwa umakini, halipo “kirahisi” hivyo. Kwa mfano, wakati baadhi ya viongozi wa Kanisa Katoliki wakidiriki kumkosoa Magufuli, msimamo wa Kanisa hilo kupitia kwa kiongozi wake mkuu kitaifa, Mhashamu Kardinali Pengo ni kumuunga mkono Magufuli (ambaye inaelezwa kuwa na ukaribu na kiongozi huyo wa dini).

Katika Uislamu nako, kuna viongozi kama vile Sheikh Ponda Issa Ponda mbao wamekuwa mstari wa mbele kupingana na kile kinachoelezwa kuwa uonevu dhidi ya Waislamu hususan katika sekta ya elimu na ajira, sambamba na kugusia masuala mengine yanayogusa haki za jamii.

Kwahiyo pengine sio sahihi kuhitimisha kuwa vuguvugu hilo ni kati ya “maaskofu na mashehe” bali baina ya, na miongoni mwa viongozi wa dini.

Je Magufuli atasikia vilio vya viongizi hao wa dini?Uwezekano huo ni mdogo. Lakini la muhimu zaidi sio kuwa atawasikiliza au atawapuuza bali mbinu zitakazotumika “kuwanyamazisha.” Je vitisho kama alivyopewa Askofu Kakobe vitakwenda mbali zaidi na kushuhudia kamata kamata iliyozoeleka dhidi ya wanasiasa wa upinzani ikihamia kwa viongozi wa dini?

Katika medani ya uongozi, inatarajiwa kuwa viongozi mbalimbali serikalini watachukua maamuzi yanayolenga “kumpendeza Rais” zaidi kuliko faida za maamuzi hayo kwa wananchi. Sio siri kwamba uchapakazi wa watumishi wengi wa umma kwa mwaka jana ulichangiwa zaidi na uoga kwa kiongozi huyo mkuu wa nchi kuliko kiu ya kuhudumia umma.

Kadhalika, inatarajiwa kuwa Daudi Albert Bashite atazidi kuwa mwanasiasa mwenye nguvu zaidi nchini Tanzania. Kwa tathmini ya mwaka jana, kiongozi huyo swahiba wa Magufuli alikuwa ni mtu wa pili kwa nguvu zaidi katika siasa za Tanzania baada ya Rais. Isingekuwa kosa kumwita “naibu Rais.”

Kuongezeka kwa nguvu za kijana huyo anayetuhumiwa kufoji elimu yake na jina lake kutazidi kuchafua taswira ya Magufuli hasa ikizingatiwa kuwa Bashite hana aibu katika kuutumia ipasavyo upendelea anaopewa na “baba yake.”

Kwenye upande wa uchumi, takwimu ziyaendelea kuonyesha kuwa uchumi wa Tanzania unafanya miujiza kwa kukua kwa kasi ya radi, ilhali hali mtaani itazidi kuwa nguvu. Kwahiyo “vyuma vitaendelea kukaza.” Lakini ni vema kila msomaji wa makala hii kuzingatia onyo la Magufuli kwamba kila atakayelalamikia “vyuma kukaza” akamatwe.

Kimsingi, kwa zingatia ukweli kwamba Tanzania katika Awamu ya Nne ya Rais Jakaya Kikwete ilikuwa ikiendeshwa kwa uchumi wa kifisadi/kihalifu, ilikuwa lazima kwa Magufuli kufanya jitihada za kuinusuru nchi hii. “Vyuma kukaza” ilikuwa hatua ya lazima, kwa sababu hata mgonjwa ili apone shurti anyweshwe dawa inayoweza kuwa chungu.

Mapungufu ya serikali katika suala hilo la jitihada za kufufua uchumi yapo ya aina kama mbili hivi: kwanza, ni taswira kwamba serikali inawakomoa wananchi makusudi, hasa ukisikia kauli mbalimbali za Magufuli kuhusu “wapiga dili.” Kwake, kila anayekumbwa na ugumu wa maisha alikuwa mpiga dili huko nyuma. Hii ni kebehi kwa mamilioni ya Watanzania masikini wanaoishi kwa kutegemea kilimo huko vijijini.

Mapungufu mengine ni katika kile alichosema Baba wa Taifa, “kupanga ni kuchagua.” Hivi kweli inaingia akilini kwa serikali kujenga uwanja wa ndege wa kimataifa “kijijini kwa Rais” huko Chato? Kuna ndege gani ya kimataifa itakayokwenda huko? Kwanini uwanja huo usingejengwa kwenye miji muhimu kiuchumi?

Sambamba na hilo la “Cahto International Airport” ni ununuzi wa ndege, almaaruf “bombadia.” Sawa, kuna haja ya kufufua “Air Tanzania” lakini kuna vipaumbele vingi tu vya muhimu zaidi ya hizo ndege.

Serikali ikiendelea na vipaumbele fyongo kama hivyo, basi uwezekano wa “vyuma kukaza ili hatimaye uchumi uimarike” utageuka mateso juu ya mateso.

Kuhusu sera ya viwanda ambayo “inapigiwa debe” kila kukicha, uwezekano wa mafanikio ni mdogo kutokana na suala hilo kuendeshwa kisiasa badala ya kiuchumi/kiuhalisia. Tanzania ya viwanda haitowezekana kwa kuchakachua data au “kujenga viwanda vya kufikirika.”

Kimataifa, kuna uwezekano kuwa uhusiano kati ya Tanzania na Kenya ukazidi kuharibika, ikichangiwa zaidi na “mgongano wa maslahi binafsi kati ya Magufuli na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta (kuhusu Raila Odinga) na ukweli kwamba nchi hizo mbili zimekuwa kwenye vita vya kiuchumi kwa muda mrefu, na ndio miongoni mwa sababu zilizochangia kuvunjika kwa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Hali ya usalama katika ukanda wa Maziwa Makuu haionyeshi dalili za kuwa njema. Matatizo ya “kijiopolitiki” katika eneo hilo yanachangiwa zaidi na maslahi binafsi ya viongozi, Paul Kagame wa Rwanda, Yoweri Museveni wa Uganda, Pierre Nkurunziza wa Burundi, Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na Magufuli wetu. Jinsi gani “mahesabu” ya urafiki kwenye lindi la uadui yatafanikiwa itategemea vitu kadhaa ikiwa ni pamoja na ufanisi wa Idara za Usalama wa Taifa katika nchi husika.

Pengine nitapata wasaa wa kurefusha ubashiri huu na kugusia masuala mengi zaidi lakini nadhani kwa sasa niishie hapa. Lakini kabla ya kuhitimisha makala hii ningependa kusisitiza kuwa “ubashiri sio exact science,” na niliyobashiri kwenye makala hii sio lazima yatokee.

Kadhalika, kwa atakayeona labda ubashiri wangu ni “wa kishetani” kwa maana ya kutompendeza, basi asijiskie huru kufanya ubashiri wake, na anaweza kunitumia nikaubandika hapa.

Heri ya mwaka mpya 2018.

One clap, two clap, three clap, forty?

By clapping more or less, you can signal to us which stories really stand out.