Vitabu nilivyosoma 2017

Heri ya Mwaka Mpya

Mwaka 2017 kwa upande wangu ulikuwa umejaa mchanyato wa vitu tofauti lakini hiyo haikuzuia utamaduni wangu wa kujisomea vitabu ingawa sio kwa kiasi kile nilichotaka kutokana na majukumu kuwa mengi. Niliweza kusoma jumla ya vitabu 30 asilimia kubwa ikiwa ni vya kuongeza Maarifa/Ujuzi ikifuatiwa na vya simulizi na vingine kadhaa vya Wasifu wa baadhi ya watu.

Kwa watumiaji wa Twitter wanafahamu nilikuwa na Thread ambayo nilikuwa naweka vitabu nilivyokuwa navisoma kwa wakati huo ingawa kuna vingine nilivisahau.

Naomba nikushirikishe vitabu vyenyewe:

1. Death of a Mafia Don — Michele Giutari

Kilikuwa kitabu cha kwanza na sababu kubwa ya kukichagua nilihitaji kitu cha kuuchangamsha ubongo safarini. Ni simulizi inayoelezea vita baina familia za wauza madawa ya kulevya. Hakijafikia utamu wa The Godfather.

2. Grit — Angela Duckworth

Katika kitabu hiki Angela Duckworth anajaribu kuelezea kwa nini watu waliozaliwa na karama wanashindwa kufanikiwa tofauti na wale ambao wamezaliwa kawaida lakini wanachagua kukomaa usiku na mchana mpaka kufikia malengo yao.

3. Shoe Dog — Phil Knight

Nina uhakika kila mmoja wetu katika maisha yake amevaa au kutumia bidhaa mojawapo ya Nike, ni kati ya kampuni zinazoingiza mabilioni ya dola kila mwaka ikiwa imetoa ajira lukuki duniani bila kusahau namna inavyowaneemesha wanamichezo. Lakini nyuma yake yupo Phil Knight ambaye ndie muasisi wake na katika kitabu hiki ameelezea kila kitu tangu anaianzisha Nike mpaka ilipofikia hapo ilipo. Ni kitabu kizuri kwa wajasiriamali wanaoanza.

4. Disrupted — Dan Lyons

Statup nyingi zilizofanikiwa zimewajengea watu picha kuwa ni sehemu nzuri sana za kufanyia kazi. Hata waanzilishi wake wanatumia nguvu kubwa hasa kwenye social media kuwaaminisha watu kuwa mambo ni mteremko, na kufanya vijana wengi watamani kukimbilia huko. Hata hivyo Dan Lyons ambaye amefanya kazi Forbes, Newsweek, ReadWrite na HubSpot anafichua “siasa” za ndani ya Startup na kuonyesha kuwa maisha sio rahisi kama tunavyodhani kufuatia uzoefu wake ndani ya HubSpot.

5. The Panther — Nelson Demille

Kwa wapenzi wa riwaya za kiupelelezi lazima watakuwa wanaomfahamu John Corey watakuwa wanaijua shughuli yake, na katika mfululizo huu hajatuangusha.

6. #AskGaryVee — Gary Vaynerchuck

Huwezi kuzungumzia nguli wa masoko mtandaoni “digital marketing gurus” bila kumtaja Gary Vaynerchuck na katika kitabu hiki amekusanya maswali mengi ambayo amekuwa akiulizwa na watu wanaotaka kujifunza kupitia kwake na kuyaweka kwa pamoja.

7. The Elements of Content Strategy — Erin Kissane

Naomba niseme wazi sikukisoma kwa kupenda, nilikuwa naangalia moja ya TedTalk na mmoja ya wasemaji akakitolea mfano nikaamua kukitafuta. Hata hivyo sikujuta.

8. Digital Fortress — Dan Brown

Kama umesoma vitabu vingine vya Dan Brown unaelewa aina yake ya uandishi ambayo kwa kiasi kikubwa inakutesa na kukufanya ushindwe kutabiri nini kitatokea mbele ya safari na nani atakuwa mtuhumiwa mkuu. Digital Fortress ni aina ile ile.

9. The Alliance — Reid Hoffman, Ben Casnocha & Chris Yeh

Waasisi wa LinkedIn na Comcate wanaelezea kwa kirefu kwa nini imekuwa ngumu kwa makampuni na biashara kuwazuia wafanyakazi wake bora hasa vijana kuhama toka kampuni moja kwenda nyingine pamoja na kuwaahidi maslahi mazuri.

10. The Girl With The Lower Back Tattoo — Amy Schumer

Amy Schumer ni kati ya wachekeshaji wazuri sana wa jukwaani na pia muigizaji mzuri wa filamu na katika kitabu chake hiki cha wasifu amejaribu kuelezea maisha yake kwa lugha ambayo imejaa ucheshi mwingi lakini inakuonyesha kuwa hapo alipo amehangaika mno hadi kupafikia.

11. Deliver Us From Evil — David Baldacci

Ni riwaya kipelelezi ikiwa ni ya pili katika mfululizo wa A. Shaw na Katie James. Kusema kweli sikukifurahia kama ilivyo kwa vitabu vingine vya Baldacci.

12. Business Model Generation — Alexander Osterwalder and Yves Pigneur

Kitabu kizuri kwa wanaoanzisha biashara au ambao tayari wana biashara kujifunza namna ya kutengeneza mkakati wa kuzifanya ziweze kujiendesha kwa ufanisi hata pale wasipokuwepo. Tatizo pekee nililoliona ni kuwa baadhi ya vitu haviwezi kufanyika kwa mazingira ya Afrika kwa hiyo za kuambiwa changanya na za kwako wakati unakisoma.

13. Msukule — Jackson Fute

Rafiki yangu Jackson Fute ni mwandishi mzuri wa simulizi na nilikuwa mmoja ya watu wa kwanza kusoma kitabu chake hiki ambacho kipo kwenye mfumo wa ebook.

14. Simulizi za Azimio la Arusha — Profesa Issa Shivji

Mwamko wa Azimio la Arusha umekuwa mkubwa tangu awamu ya tano iingie madarakani kwa hiyo ilikuwa ni muda muafaka wa kujikumbusha lilikuwa na lengo gani na kama kwa upepo wa siasa za sasa linaweza kufanya kazi miaka 50 tangu lilipoanzishwa.

15. The Divine Comedy — Dante Alighieri

Niliamua kukirudia kitabu hiki ambacho nilikisoma kwa mara ya kwanza 2010 baada ya kuwa mojawapo ya vitabu tulivyokuwa tunavifanyia mapitio kwenye Book Club.

16. Macbeth — William Shakespeare

Kiliwekwa iSwapMyBooks nikakichukua kujikumbushia enzi hizo za shule wakati tunajaribu uigizaji bila mafanikio.

17. The Rain Maker — John Grisham

Ukisoma vitabu vingi vya John Grisham unaweza tamani kurudi shule kusomea sheria kutokana na namna anavyoweza kuandika simulizi zenye mchuano unaohusisha mahakama au sheria kwa namna moja au nyingine, The Rain Maker ni kati ya vitabu hivyo.

18. The Burning Room — Michael Connely

Mpelelezi Harry Bosch anarudi tena kwenye mfululizo huu kutatua kesi ambayo inawapasua kichwa baada ya kumsaka mdunguaji aliefanya mauaji na kupotelea kusikojulikana.

19. This How You Lose Her — Junot Diaz

Rafiki yangu Joyceline alipoweka Twitter picha ya cover la hiki kitabu wakati anakisoma nikajua ni maufundi ya namna ya kufanya usimpoteze asali wa moyo lakini kumbe ni riwaya ya mahaba yenye wahusika wa Latin America. Hata hivyo nilikifurahia aina yake usimuliaji.

20. Tough Times Never Last But Tough People Do — Robert Schuller

Askofu Robert Schuller anatumia mifano ya vikwazo alivyopitia yeye, familia na watu aliokutana nao katika maisha kukumbusha kuwa kila gumu katika maisha lina mwisho. Hiki nacho nilibadilishana na Joyceline.

21. The Courtship Of Princess Leia — Dave Wolverton

Kila mpenzi wa Star Wars ana kitabu anachokipenda, na kwangu hiki ndio bora zaidi. Nilikisoma kwa mara ya kwanza mwaka 2002 na kila mwaka nimekuwa na utaratibu wa kukirudia nikihitaji kuchangamsha ubongo.

22. Born A Crime — Trevor Noah

Trevor Noah anajulikana kama mmoja ya wachekeshaji bora duniani na alizaliwa Afrika Kusini. Ukifuatilia ucheshi wake amekuwa na tabia ya kuzungumzia maisha yake wakati anakulia Afrika Kusini yenye ubaguzi hadi inapata uhuru na kufikia hapa ilipo sasa. Namshukuru Queen Saidi kwa kunitumia kitabu hiki.

23: Elon Musk: Tesla, SpaceX, and the Quest for a Fantastic Future — Ashlee Vance

Mara ya kwanza namsikia Elon Musk ilikuwa ni 2012 wakati wa Barack Obama na Mitt Romney wanachuana kwenye mdahalo ambapo Romney alimlaumu Obama kwa kutumia hela za walipa kodi kusaidia makampuni ambayo yalikuwa yanaelekea kufikilisika wakati mdororo wa kiuchumi 2008 wakati yalikuwa hayajaanza kuingiza faida. Tesla ambayo muasisi wake ni Elon Musk ilitolewa kama mfano. Hata hivyo muda mchache baada ya Obama kuchaguliwa kwa awamu ya pili Tesla ilianza kuingiza faida huku hisa zake zikifanya vizuri na wakafanikiwa kurudisha mkopo ndani ya muda mfupi. Baada ya hapo nilijikuta napenda kumfuatilia Elon Musk ambaye anafananishwa na Tony Stark ambaye ni anawakilisha character ya Iron Man kwenye filamu na comic book za Marvel. Kitabu hiki naweza kusema ni kati ya vitabu bora 5 nilivyosoma 2017.

24: The Strongman: Vladimir Putin and the Struggle for Russia — Angus Roxburgh

Nilikiona kwa mara ya kwanza kwenye orodha ya vitabu alivyovisoma Zitto Kabwe 2016 nikaamua kukiweka kwenye orodha yangu. Kimenisaidia sana kuelewa hali ya siasa ambayo dunia inapitia kwa sasa, sikushangaa hata iliposemekana kuwa Urusi iliingilia uchaguzi wa Marekani.

25: Origin — Danny Brown

Ni kitabu kipya kilichotoka 2017 kikiwa ni mfululizo wa Dr Robert Langdon ambaye safari hii anakwepa wauaji wanaomsaka wakati huo akijaribu kupata majibu ya nini kimemuua rafiki yake aliepigwa risasi wakati akijiandaa kuitangazia dunia kuhusu uvumbuzi ambao ungebadili suala la binadamu na imani kwa Mungu.

26. Meditations — Marcus Aurelius

Ni kitabu kilichotokana na machapisho binafsi ya Marcus Aurelius aliekuwa mtawala wa dola ya Roma miaka ya 160 na 180 AD. Machapisho yake nimekuwa nikikutana nayo kwenye vitabu vya maarifa ninavyosoma nikapata hamu ya kukisoma hiki.

27. The Special One — The Secret World of Jose Mourinho — Diego Torres

Kimeelezea vizuri yaliyo nyuma ya pazia kwa maisha ya kocha wa Man United Jose Mourinho.

28. Thomas Jefferson and Tripoli Pirates — Brian Kilmeade & Don Yaeger

Ukikisoma kitabu hiki kinakupa picha ya kuwa Marekani iko hapo ilipo kwa sababu waasisi wake waliamua kutengeneza taifa lenye nguvu duniani. Ni matukio yaliyowekwa kwa mfumo wa simulizi yanakufanya usitake kuacha kukisoma.

29. The Innovators DNA — Jeff Dyer & Clayton M. Christensen

Ilikuwa zawadi toka kwa mmoja ya watu waliohudhuria uzinduzi wa iSwapMyBooks. Kitabu kinaeleza vitu vitano ambavyo wagunduzi wote wakubwa wanavyo na vinaendelea kuwabeba mpaka sasa.

30. Ujasusi wa Kidola na Kiuchumi — Yericko Nyerere

Naomba niseme tangu kitabu hiki kipo kwenye hatua za muswada nilikuwa nakipitia lakini sikuweza kukisoma kwa uvivu wa kuwa nakifahamu, ila ilibidi nikisome vizuri ili nibishane na rafiki yangu Yericko.

Hii ndio orodha kamili ya vitabu nilivyovisoma 2017, lengo langu 2018 ni kusoma vitabu angalau 50 na nusu yake iwe ni vitabu vya waandishi wa Afrika.

Heri ya mwaka mpya 2018.

Like what you read? Give Uncle Fafi a round of applause.

From a quick cheer to a standing ovation, clap to show how much you enjoyed this story.