‘Msaada wenye Tija’

"Fukara hajawa Fukara kwa kukosa mkate pekee yake, Bali Fukara huwa Fukara kwa kukosa uwezo wa kujenga wazo jipya la kujikwamua na njaa inayomkumba" -adam adyz

Siku kadhaa zilizopita, japo napaswa kusema mwaka jana kwa sababu ni kweli mwaka umebadilika, lakini ki ukweli ni siku chache sana tumezihesabu toka tarehe za mwaka zibadilike.Ilikua siku ya jumapili jioni ambapo ni siku huitumia mara zote kwa ajili ya maandalizi ya juma jipya linaloanza yaani jumatatu. Basi nilijisogeza ilipo saluni, kwa kinyozi wangu mahiri ambaye hayupo mbali na ninapoishi.

Haikua siku tofauti na nyingine ila ilikua ni siku niliyobahatika kuwa na wakati mzuri wa mazungumzo fikirishi na kinyozi wangu mahiri. Mazungumzo ambayo nimeona niyahifadhi kwa kuyawekea kumbukumbu ya maandishi.

Pamoja na kuwa mara zote hua tunachambua mawili matatu kuhusu mitazamo mbalimbali ya maisha na jamii, hili ninaloweka hapa leo lilinipa funzo muhimu ambalo limenijenga kimtazamo na fikra chanya.

Kupitia makala hii nitaliboresha wazo hilo nikiliambatanisha na moja ya THREAD yangu ya mwaka 2018 kupitia ukurasa wangu wa Twitter ambayo ilizungumza juu ya mtu anavyoweza kusaidika kiuchumi bila kuwa kero kwa anao waomba msaada.

Link hii apa

https://twitter.com/adam_adyz/status/1072894908074213376?s=19


Rafiki kinyozi akiwa amekaza macho yake kwa umakini sana ili kuhakikisha anafuata maelekezo ya mteja wake, haikumfanya mdomo wake ushindwe kuendelea kupiga stori za hapa na pale huku tukitazamana kupitia kioo kilichopo mbele yetu.

Moja ya maada aliyokaa nayo muda mrefu kuigusia ni juu ya ‘changamoto kwenye maisha’, alisema hakuna binadamu asiye na changamoto. Iwe kwenye kazi, familia, mahusiano au maisha tu ya kila siku. Hakuna namna unaweza kumtenga mtu na changamoto, kupitia magumu fulani ni dalili tosha kuwa mtu anaishi maisha halisi. Alisema vingi lakini msisitizo ulikua kwamba changamoto hazina mwenyewe na zina kila mtu.

Unaweza ukaamka ukapata kazi au ukapoteza kazi, ukipata kazi inaweza ikawa ni kazi ngumu zaidi kuliko kazi ya kupata kazi. Unaweza ukapoteza kazi na ukapata kazi bora zaidi, au ukapata kazi ya kuanza kutafuta kazi. Changamoto zipo kwa kila mtu japo zinatofautiana.

Kama kuna kitu ambacho mwanadamu ana uhakika wa kukimiliki maisha yake yote, bila kujali umri, jinsia, rangi, kabila au kigezo chochote kinacho mtofautisha na mwingine… basi kitu hicho ni CHANGAMOTO za maisha. ~adam adyz

Kwa maisha tuliyonayo, yapo mengi sana tunayoyapitia ili kujifunza kuwa imara na bora.

KUTANGULIA SI KUFIKA, ILA NI KUTANGULIA

Japo kila mtu ana pambano lake binafsi ambalo wengine hatulifahamu ila ni ukweli ulio wazi kuna baadhi hupata njia mapema za kushinda. Wengine huchelewa kupata ushindi, wengine hupata ushindi na kukutana na changamoto ngumu zaidi. Katika haya yote aliyetangulia ametangulia tu, na anapaswa kumsaidia mwingine ili ajihakikishie msaada wa baadae.


Leo basi nitazungumzia kuhusu msaada wenye tija, msaada ambao hautamfanya yule anayesaidiwa kujihisi mnyonge wala asipoteze urafiki na watu.

Kwanza ifahamike wenye changamoto za maisha na wanaohitaji msaada ni wengi zaidi kuliko watoa misaada wenye utayari. Hivyo basi kwa kuzingatia idadi ya watoa msaada na wanaohitaji msaada, yafuatayo yanaweza kuwa mambo muhimu zaidi ya kuzingatia kabla hujaanza kuomba msaada:

  • Usitumie muda mwingi kuomba msaada wa pesa, utapoteza marafiki. Omba msaada wa mawazo jinsi ya kutengeneza fursa ya kujikwamua
  • Tumia muda mwingi kutafuta njia za kutengeneza pesa. Kaka yangu mpendwa ambaye ni mentor wangu pia aliwahi kuniambia, “Usione aibu kuitafuta pesa, eti watu watanionaje. Kama unaipata kihalali wala usipate shaka… piga pesa”.
  • Usimtegemee mtu yoyote kwa asilimia 100, hata marafiki wana ukomo wa kusimama na wewe. Tumia connections zote ulizokua nazo kujaribu kutengeneza fursa mpya.
  • Usimueleze kila mtu shida yako, chagua wachache wenye nia njema na wewe ambao wataugua na wewe kwa hatua unazopitia. Hao waelezee watakupa faraja!
  • Tengeneza muunganiko na watu wapya, mfano hata kupitia mitandao ya kijamii. Ukiona mtu ana uelekeo wa maarifa yanayoweza kukusaidia, zungumza naye jenga naye urafiki. Usieleze shida zako, eleza mipango yako na fursa za kiuchumi uone vipi atakusaidia. Usidharau chochote kinachoweza kuletea watu wapya.
  • Nimejifunza na nimeona, watu wakinunua bidhaa ili kumshika mkono mtu ali ajikwamue kiuchumi. Point ni hii, ukionesha nia ya kusaidika watu watakusaidia. Anza kitu, kifanye 'well done’, peleka bidhaa au wazo linalo onekana, watu watakusapoti bila kuchoka. Watanunua, hutaamini.

Kuwa na tatizo sio tatizo, tatizo ni mtazamo wako juu ya hilo tatizo. Kabla hujaanza kuwalaumu rafiki zako kwa kushindwa kukusaidia ni vema ukatambua kila mtu ana matatizo binafsi. Pia ni muhimu sana kwako kujifunza kuomba msaada kwa namna ambayo haitakuvunjia heshima na kukupotezea marafiki.

Onyesha nia ya kutaka kuondokana na tatizo ulilo nalo. Ikiwezekana usiombe msaada wa pesa kabisa, boresha fikra zako ili utoe mawazo ambayo yanaweza kugeuzwa kuwa fursa. Onyesha unahitaji kujua kuvua samaki na sio unahitaji kupewa samaki aliyevuliwa tayari. Kuwa endelevu.

Nihitimishe kwa kusema hivi

kumuokoa mfa maji ni lazima awe tayari kuokolewa, tofauti na hapo kutapatapa kwake kutawazamisha wote

...✍naweka kalamu chini!