Ado Shaibu
12 min readOct 15, 2018

RAIS MAGUFULI NI KARUME BILA BABU?

(Uchambuzi wa Hotuba na Matamko ya Dk. Bashiru Ally, Katibu Mkuu wa CCM Kwenye Maadhimisho ya Miaka 25 ya MVIWATA na Mjadala Kuhusu Chaguzi Barani Afrika Katika Kumbukizi ya Mwalimu Nyerere, UDSM)

Na Ado Shaibu

Ni muhimu kabla ya yote niweke bayana kwamba kilichonishajiisha kuitafuta na kuichambua hotuba yote ya Dk. Bashiru Ally, Katibu Mkuu wa CCM iliyotolewa kwenye Maadhimisho ya Miaka 25 ya Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Wadogowadogo (MVIWATA) yaliyofanyika mjini Morogoro ni kauli ya Prof. Shivji kuipa hotuba hiyo hadhi ya hotuba ya kipekee kihistoria.

Ingawa nilimpa changamoto Prof. Shivji upesiupesi alipoweka maneno hayo kwenye ukurasa wake wa Twitter nilifahamu lazima kutakuwa na jambo la kipekee kwenye hotuba hiyo lililomsukuma Prof. Shivji kuipa hadhi tajwa.

Pasi shaka, Prof. Shivji ni mwanazuoni na mchambuzi makini (sheria, siasa, historia) ambaye sidhani kama mahusiano yake binafsi na Bashiru ndiyo yaliyomsukuma kutoa sifa hizo kwa hotuba ya Bashiru iliyotolewa MVIWATA.

Kwa mujibu wa Prof. Shivji, baada ya kuondoka kwa Mwl. Nyerere, ndani ya miongo miwili iliyopita, hapajawahi kutokea hotuba ya mwanasiasa ndani ya CCM iliyoweza kupambanua mambo kwa ufasaha na uchungu halisi kuhusu maslahi ya wavujajasho kama alivyofanya Dk. Bashiru Ally kwenye hotuba yake.

Si kusudio langu kupima kama hotuba ya Dk. Bashiru ina hadhi iliyosemwa. Katika uchambuzi wangu (kwa kurejea hotuba yake ya MVIWATA na hivi majuzi UDSM) nitachambua;

i. Msukumo wa kimazingira wa hotuba mbili za Dk. Bashiru

ii. Lengo la uteuzi wa Dk. Bashiru na hotuba zake

iii. Masuala muhimu yanayohitaji mjadala wa kitaifa

iv. Maeneo yaliyopotoshwa

v. Hitimisho: Changamoto kwa Dk. Bashiru

USHUJAA AU MSUKUMO WA KIMAZINGIRA?

Dk. Bashiru amezungumza mara kadhaa baada ya kuteuliwa kushika nafasi yake ikiwemo kufanya mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari.

Lakini, ni dhahiri kwamba huko nyuma hajawahi kujipambanua kimapambano kama alivyofanya kwenye Mkutano wa MVIWATA na baadaye ukumbi wa Nkurumah pale UDSM kwenye kongamano la kumbukizi ya Mwalimu Nyerere ambalo lilijikita katika kujadili changamoto katika chaguzi Afrika.

Jambo hili halijatokea kwa bahati mbaya. Haijatokea kwa bahati mbaya hotuba na matamko haya hayajatolewa jukwaani Ukonga au Liwale mbele ya mbwembwe za Wana-CCM na badala yake yametolewa MVIWATA na ukumbi wa Nkurumah Chuo Kikuu cha Dar es salaam.

Bashiru ni mchambuzi na rafiki wa muda mrefu wa MVIWATA. Katika maadhimisho ya MVIWATA, ingawa alijitetea kwamba anazungumza kwa kofia mbili za rafiki wa MVIWATA na ile ya Katibu Mkuu wa CCM, lakini ni ukweli kwamba Bashiru alijitazama na kuzungumza kama bado ni rafiki wa MVIWATA.

Kwa koti hilo, alijikuta anarusha mishale mingi sana kwa serikali, taasisi za serikali na chama chake.

Mbele ya rafiki zake aliopigana nao pamoja kwa muda mrefu (Prof. Shivji, Prof. Kamata, Sabatho Nyamsenda, Wana-MVIWATA n.k) alilazimika kutuma ujumbe muhimu kuwa yeye bado hajabadilika.

Pichani: Prof. Shivji akikaribishwa na mwaanachama wa MVIWATA kushiriki kwenye Mkutano Mkuu wa MVIWATA mwaka 2010. Mwingine pichani ni Dk. Bashiru Ally.

Hivyohivyo, akianza kujieleza katika ukumbi wa Nkurumah kwenye mjadala juu ya chaguzi barani Afrika, Bashiru alisema kwamba "huingia katika ukumbi huo kwa hisia kali".

Kama mtu aliyeshiriki kuasisi na kukitumikia Kigoda cha Mwalimu Nyerere kwa muda mrefu, Bashiru alijikuta anazungumza kama mwanaakademia anayechambua kwa uhuru mapungufu ya vyama vya siasa na hasa zaidi chama chake.

Jambo la kujiuliza, Je Bashiru ataendelea na ari hii aliyoionesha MVIWATA na UDSM? Jibu langu ni hapana!

Nafasi yake ya sasa, kutokana na mwenendo mbovu wa siasa zetu, inamlazimisha awe na sura mbili.

Kwa upande mmoja analazimika kuendelea na kutoa mchango kwenye mapambano ya walalahoi. Kwa upande mwingine, analazimika kuzungumza mambo ya kipropaganda ili kuwaridhisha na kuwajengea imani wana CCM wenzake.

Kwa kutumia ujuzi wake mkubwa wa kucheza na maneno, Dk. Bashiru amekwishazicheza nafasi zote mbili.

Mathalani, mkutano wake wa kwanza na Wanahabari ulitawaliwa na tambo na propaganda za CCM lengo likiwa kuwapa imani wana CCM kwamba yeye ni mwenzao.

Kwa mfano, kupitia mkutano huo Bashiru alisema kwamba kutokana na "kupita bila kupingwa" kwenye kata kadhaa na "kushinda" kwenye kata zilizosalia, CCM ilipata ushindi wa "mia chini ya mia" na kwamba hiyo ni dalili ya kuongezeka kwa imani ya wananchi kwa CCM!

Dk. Bashiru anafahamu (na sasa ana taarifa muhimu za kiusalama pia) kwamba jambo hilo si la kweli na CCM inalazimika kupora uchaguzi na kutumia mabavu kushinda kimaigizo.

Mfano mzuri ni ule wa wagombea wote (8) wa udiwani wa vyama vya upinzani kwenye uchaguzi wa marudio huko Tunduma kutamkwa kwamba si raia wa Tanzania.

Jambo hili ni la kikaburu. Kwamba wagombea wote wa upinzani si raia bali wagombea wa CCM pekee ndio raia!

Ushindi unaotokana na vitendo vya kikaburu ndani ya chama kilichowahi kujipambanua huko nyuma kuwa cha kimajumui (Pan-Africanist) hauwezi kuwa "ushindi wa mia kwa mia".

Mfano mwingine wa Dk. Bashiru kuwapa imani wana CCM wenzake ni pale alipoulizwa juu ya mustakabali wa mchakato wa katiba mpya ambayo naye alikuwa kinara kuipigania.

Alichojibu, ni kwamba yeye sasa si "Bashiru mchambuzi" tena na kwamba akiwa Katibu Mkuu hawezi kwenda kinyume na chama chake.

Lengo lake hasa ni kuonesha utii usio na shaka kwa Chama hata kama kuzikwa kwa mchakato wa Katiba Mpya kumeliingizia hasara isiyomithilika taifa.

Hivyo basi, nihitimishe sehemu hii kwa kusema kwamba, kwa muundo wa siasa zetu, tutaendelea kuwa na Bashiru wote wawili; Bashiru anayekumbuka nafasi yake ya kimapambano kwenye ukombozi wa walalahoi na Bashiru anayejaribu kuwaridhisha wana-CCM wenzake.

2. LENGO HASA NI NINI?

Uteuzi wa Dk. Bashiru Ally haukuambatana na mjadala mkubwa nchini. Kwa maoni yangu, katika nchi ambayo tuna mfumo wa chama kimoja ndani ya vyama vingi (De facto one party state) uteuzi wa mtendaji mkuu wa Chama cha Mapinduzi sio jambo lililopaswa kupita kama upepo.

Kwenye eneo hili ninajaribu kuangazia kwa ufupi sababu za uteuzi na matamko ya Dk. Bashiru. Kwa maoni yangu, maeneo muhimu ya kuyaangazia ni matatu;

1. Jaribio la Kumpa Magufuli Mwelekeo wa Kiitikadi

2. Jaribio la kuinusuru na kurejeshea imani ya umma CCM

3. Jaribio la kuzubaisha umma wa walalahoi.

Kwa maoni yangu, sababu hizo (au moja kati ya hizo) ndizo zinazoelezea kiini cha uteuzi wa Dk. Bashiru Ally, kukubali kwake nafasi hiyo na msingi wa matamko yake ya kimapambano aliyoyatoa MVIWATA na UDSM.

Tuzipitie mojamoja kwa ufupi:

1. Kujenga Mwelekeo wa Kiitikadi: Magufuli ni Karume Bila Babu?

Kwenye utangulizi wa Kitabu cha “Husuda ya Marekani Dhidi ya Mapinduzi ya Zanzibar: Siku 100 za Kuundwa kwa Tanzania”, Komredi Abdulrahman Babu anajenga hoja kwamba ujio wa makomredi wa Chama cha Umma (Umma Party) kwenye Mapinduzi ya Zanzibar ulikusudia kuyapa mwelekeo wa kiitikadi mapinduzi hayo.

Fikra kama hizi zinaelezwa pia na Komredi Ali Sultan Issa kwenye Kitabu kuhusu maisha yake na Maalim Seif Sharrif Hamad kiitwacho “Zanzibar, Race and Revolution: Memoirs of Ali Sultan Issa and Seif Shariff Hamad”.

Imani ya Umma Party ilikuwa kwamba wangeweza kuibadili ASP na Mapinduzi ya Zanzibar ili yaweze kuchukua mkondo wa kiitikadi ya ujamaa.

Imani hii iliwalazimisha Makomredi wa Umma Party kufuta chama chao na kujiunga katika serikali ya ASP chini ya Rais Karume. Hawakufanikiwa!

Makomredi wa Umma walifanikiwa kushika nafasi nyeti katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano lakini hawakuweza kumbadili Karume na Kuielekeza nchi kwenye mkondo waliotaka.

Historia hii inajirudia sasa. Wapo watu, Dk. Bashiru akiwemo, bila shaka wana imani kwamba Rais Magufuli anaweza kuwa mtaji muhimu wa kuipeleka nchi kwenye siasa za mrengo wa kushoto na kujenga ujamaa.

Na inaonekana jambo hili limekuwepo kwa muda mrefu. Tunaofuatilia hotuba za Rais Magufuli tumekuwa tukijiuliza, nani amekuwa akimpa vionjo vya Azimio la Arusha alivyovitaja kwenye hotuba angalau mbili tatu.

Rais Magufuli si Rais mwanazuoni na mchambuzi anayeweza kujipambanua vyema kiitikadi akaeleweka kama alivyokuwa Mwalimu Nyerere.

Magufuli si Mjamaa. Lakini, kama nilivyosema awali, baadhi ya maamuzi na hotuba zake zina vionjo vya kijamaa hasa mambo matatu; Mosi, kuzirejea zama za ujamaa nchini kama zama za fahari ya kitaifa na mafanikio. Pili, kuonesha, kwa matamko kanganishi, chuki dhidi ya ubeberu na wale anaowaita "majizi" walioliibia taifa. Tatu, maamuzi yanayoelekea kuipanua sekta ya umma na kuiminya sekta binafsi.

Lakini, yote haya yamekuwa yakisemwa na kufanywa kwa mtindo usiojipambanua kiitikadi na unaojikanganya (contradicting).

Rais hupenda pia kujiita "Rais wa wanyonge" ingawa kwa hakika Serikali yake imechukua maamuzi mengi kuwakandamiza wanyonge kama vile kuwanyima mabinti wanaopata ujauzito haki ya kusoma, kupuuza maslahi ya wanyakazi, bomoabomoa, kunyakua fedha za wakulima wa korosho n.k

Bila shaka imani ya Dk. Bashiru ni kuwa mambo haya, licha ya mapungufu yake, yanaweza kutumika kama mtaji wa kujenga ujamaa na siasa za mrengo wa kushoto nchini. Hiki ndio kiini cha Dk. Bashiru kukubali uteuzi.

Kwa maoni yangu, kama ambavyo Babu hakuweza kuibadili ASP ya Karume, Dk. Bashiru na wale wenye mawazo kama yake hawatafanikiwa kuibadili serikali ya Magufuli na CCM kuchukua mkondo wanaoutaka.

Sababu zipo nyingi lakini iliyo kuu ni hulka na mtindo wa uongozi wa Rais Magufuli mwenyewe.

Rais Magufuli, na hili kwa kweli halihitaji miwani ya kukuza uoni kulielewa, ni Rais anayetaka kuamua na kutenda kila kitu peke yake.

Kuamini kwamba unaweza kujenga ujamaa kwa kiongozi ambaye kila kukicha kauli yake ni "MIMI nitafanya", "MIMI nitaleta pesa", "MIMI nimeamua" n.k ni kujidanganya.

Kitu kidogo watu wenye ndoto hiyo wanaweza kufanikiwa ni kuongeza nguvu kwenye mjadala juu ya ujamaa na siasa za mrengo wa kushoto nchini ambalo ni jambo jema kwa sababu Azimio la Arusha liliondolewa na CCM mwaka 1991 kimyakimya!

2. Jaribio la Kuongeza Imani ya CCM

Utafiti wowote huru utaonesha kwamba imani ya wananchi kwa Chama cha mapinduzi ndani ya miongo miwili imepungua sana.

Hili linaonekana waziwazi kupitia mwitikio wa watu kujitokeza kupiga kura na idadi ya kura ambazo CCM imekuwa ikizipata kwenye uchaguzi mkuu. Vyote viwili, kama ambavyo hata wakubwa wenyewe ndani ya chama na serikali wamekuwa wakinukuliwa hivi karibuni, vimepungua sana!

Rais Magufuli mwenyewe ambaye alitazamwa kama mtu ambaye angerejesha imani ya wananchi kwa CCM, ameipoteza fursa hiyo.

Matokeo ya utafiti wa mwisho ya utafiti wa #SautiZaWananchi wa Shirika la TWAWEZA yanaonesha kuwa Rais Magufuli ni Rais asiyekubalika zaidi (the most unpopular president) katika historia ya nchi yetu.

Matokeo ya approval rate (kiwango cha kukubalika) kwa Rais Maguguli chini ya Mpango wa #SautiZaWananchi yanaonyesha kukubalika kwa Rais Magufuli kumeporomoka kutoka 91% alipoingia madarakani hadi 54% mwaka 2018!

Kutokukubalika kwa CCM kwa upande mmoja na kuporomoka kwa kuungwa mkono kwa Rais Magufuli na Serikali yake kwa upande mwingine ndiko kunakosababisha vitimbi hivi vinavyoitwa "kuunga mkono juhudi" na maigizo yanayoitwa chaguzi za marudio.

CCM kimekoma kuwa chama cha siasa na nafasi yake imechukuliwa na vyombo vya dola hasa polisi. CCM sasa inapora kura waziwazi kwa kiwango ambacho hata mtoto mdogo anajua.

Uteuzi wa Dk. Bashiru na maoni yake MVIWATA, UDSM na kwingineko mbeleni yanalenga kuirejesha imani hiyo iliyopotea.

Njia hii, ingawa itawazubaisha watu kama nitavyoeleza kwenye hoja inayofuata, haitofanikiwa kuirejesha imani iliyopotea kwa chama, serikali na Rais.

Njia pekee ya kurejesha imani ya CCM na serikali yake kwa kweli si matamko bali ni kusimamia haki na maendeleo ya watu mambo ambayo si CCM wala serikali yake wanayataka.

3. Nia ya Dhati au Hadaa?

Bashiru anaweza kuwa na nia ya dhati. Lakini nia hiyo itamezwa na kukosekana kwake ndani ya CCM na serikali yake.

Hivyobasi, matamko yake yataishia kujenga tumaini la muda la wavujajasho.

Watu wanaweza kudhani kwamba Chama na serikali vinarejeshwa kwenye mstari na wakaweka matumaini yao.

Ubepari hudumu kwa njia nyingi. Moja wapo ni kuchipua kwa viongozi wenye mrengo wa siasa za kitaifa au za kushoto wanaoonyesha dalili za kuleta nafuu.

Walalahoi hufanya makosa ya kihistoria kuyakabidhi matumaini yao kwa watu hao na kusimamisha wajibu wao wa kihistoria wa kimapambano.

Hili jambo ambalo linaweza kuwafanya "wakubwa" ndani ya CCM wamvumilie Bashiru hata kama baadhi ya kauli zake zitawakera.

Rai yangu, ambayo imesemwa pia kwenye maadhimisho ya Miaka 25 ya MVIWATA na Prof. Shivji na Bashiru mwenyewe, umma usiyakabidhi majukumu yake ya kimapambano kwa wanasiasa pekee.

MAMBO YA HERI!

Sasa nakaribia mwisho. Kwenye hotuba zake MVIWATA na UDSM yapo masuala kadhaa ya kitaifa ambayo Dk. Bashiru aliyazungumza ambayo mimi binafsi ninayaunga mkono.

Hapa chini ninayakariri ili kuendeleza mjadala wa kitaifa.

Ninafiki kwamba;

*Kuhusu Mapambano ya Walalahoi*

1. Kwamba Walalahoi ni lazima waungane kupitia vyama vya ushirika na vyama vya wafanyakazi vinavyoendeshwa kidemokrasia.

2. Mfumo uliopo wa mikopo chini ya mabenki ya kibiashara si rafiki kwa walalahoi. Ni muhimu kutafakari mfumo mbadala hasa kupitia benki za maendeleo ambao hautawakamua walalahoi

3. Ardhi ni uhai, haifai kubidhaishwa

4. Umma unapaswa kushika nafasi yake katika kuendesha uchumi wa nchi na kuwajibisha viongozi

*Kuhusu Uchaguzi, Vyama vya Siasa na Uendeshaji wa Siasa*

6. Wananchi walio wengi wamekata tamaa na mfumo wa uchaguzi nchini kwa sababu umekuwa kama gulio la kununua kura kwa hongo. Kwa kuongezea, vyombo vya kusimamia uchaguzi pia havitendi haki hivyo uchaguzi umekoma kuwa njia ya wananchi kuchagua viongozi wao na kuelezea hisia zao.

7. Vyama vya siasa ni tegemezi

8. Vyama vingi vya siasa havina itikadi onayoeleweka na kufuatwa. Kwa kuongezea, itikadi haitazamwi kama jambo muhimu linaleta utofauti wa vyama na kuongoza mwelekeo wa nchi. Ndio maana Ndg. yangu Kirufi aliweza kuhama kutoka CCM, kisha CHADEMA halafu ACT ndani ya wiki moja. Ndani ya vyama kwa sehemu kubwa watu hufuata watu maarufu, siasa nyepesi za matukio na kishabiki badala ya itikadi.

8. Chuki na uhasama vimeongezeka ndani ya jamii kwa misingi ya utofauti wa vyama.

YALIYOKOROGWA!

Kama nilivyosema awali, yapo maeneo ambayo Dk. Bashiru aliyapotosha au kutoyatilia mkazo kwenye hotuba zake, hasa UDSM. Labda kwa sababu UDSM pia alikuwa na wanasiasa wenzake (Lowasa, Zitto, Mashinji n.k) na akaona ni muhimu kulitumia jukwaa hilo kushambulia na kujibu mapigo.

Maeneo nitayoyaangazia ni mawili; suala la hofu na CCM kujitegemea.

1. Mkate wa Hofu si Maendeleo!!

Katika hotuba yake fupi, Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Mzee Joseph Butiku alisema kwamba taasisi yake imezungumza na wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa na wamekubaliana na ukweli kwamba hapa nchini kuna viashiria vya uvunjifu wa amani.

Mzee Butiku aliongezea kwamba viashiria hivyo kwa sehemu kubwa vinasababishwa na viongozi.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa zamani Ndugu Edward Lowasa akasisitiza kwamba si tu kwamba kuna viashiria vya uvunjifu wa amani bali kuna “hofu”.

Akitoa mchango wake juu ya jambo hilo Ndg. Bashiru alidai kwamba

i. Wenye hofu ni wezi na mafisadi ambao nao wanasambaza hofu hiyo kwa wananchi ili ionekane kwamba nchini kuna hofu

ii. Kwamba hofu ya walalahoi ni kupata mkate wao.

Kwa maoni yangu, hoja zote za Dk. Bashiru juu ya jambo hili si sahihi.

Tuanze na hoja ya kwanza. Suala la kuongezeka kwa hofu hapa nchini ni jambo la dhahiri ambalo linaonekana kwa macho na limethibitishwa kwa utafiti.

Utafiti wa Sauti za Wananchi (TWAWEZA) unaokwenda kwa jina la “Kuwapasha Viongozi: Maoni ya Wananchi Kuhusu Siasa Nchini” unaonesha kupungua kwa uhuru wa wananchi ukilinganisha na miaka na miaka mitatu iliyopita.

Kwa mujibu wa utafiti huo wa TWAWEZA:

"Wananchi wanasema uhuru umepungua kwa vyama vya upinzani kufanya mikutano na kutoa maoni yao (64%), vyombo vya habari kukosoa au kuripoti maovu ya serikali (62%), na makundi yasiyofungamana na upande wowote kupaza sauti zao na kufanya mikutano (58%).

Nusu ya wananchi pia wanaona hawana uhuru wa kuonesha mitazamo yao ya kisiasa (54%)"

Kuminya uhuru wa watu ndiko kunakozalisha hofu. Dk. Bashiru hawezi kusema kwamba nchini hakuna hofu wakati kwa mujibu wa tafiti, watu hawana uhuru wa kusema. Labda aje na utafiti wake kwa sababu utafiti hupingwa kwa utafiti.

Tuje kwenye hoja ya pili, kwamba hofu ya msingi ya walalahoi ni mkate wao.

Dk. Bashiru anafahamu kama ilivyofafanuliwa na Mwongozo wa TANU wa mwaka 1971 kwamba maendeleo hasa ni kitendo kinachowapa uhuru wa kujiamulia mambo yao na kwamba kitendo chochote, hata kama kinaleta mkate mezani hakiwezi kusemwa kuwa ni maendeleo kama kinawakandamiza, kuwaumiza au kuwanyanyasa watu.

Kwa maneno ya Ibara ya 28 ya Mwongozo wa TANU (1971) ambao Dk. Bashiru alishiriki kuuchapisha upya akiwa Kigoda cha Mwalimu Nyerere inasema:

“Kitendo chochote kinachowapa watu uwezo zaidi wa kuamua mambo yao wenyewe na kuamua maisha yao wenyewe ni kitendo cha maendeleo japo hakiwaongezei afya wala shibe.

......kwetu sisi maendeleo maana yake ni yale yanayotuondolea kuonewa, kunyonywa, kunyanyaswa na mawazo ya kufungwa"

Hoja hii ya kuminya uhuru wa watu kwa kisingizio cha kuleta maendeleo si sawasawa. Maendeleo lazima yaambatane na uhuru. Yanayoitwa "maendeleo" yanayokwenda sambamba na utekaji, kamatakamata, mauaji, ufungiaji wa kipendeleo wa vyombo vya habari, kuminya haki za vyama n.k hayawezi kuwa maendeleo halisi. Maendeleo ni ukombozi, ukombozi ni uhuru.

KWAPUA KWAPUA YA CCM!

Dk. Bashiru alizungumzia pia utegemezi wa vyama vingi kwa wafanyabiashara na vikundi maslahi vya ndani na nje. Hoja yake ni muhimu. Uhuru ni kujitegemea, utegemezi ni utumwa.

Ambalo Dk. Bashiru hakulisema ni ukweli kwamba CCM imekwapua mali za Watanzania kama vile viwanja vya mpira, majengo, ardhi n.k na kujimilikisha. Jambo hili linaondoa uwanja sawa wa kiushindani baina ya vyama. Anaposema CCM ina hela nyingi ukweli ni kwamba kihistoria hela hizo zimetokana na kudhulumu mali za umma. Kwa hiyo rai ya vyama kujitegemea, licha ya umuhimu wake, iambatane na mjadala wa CCM kurudisha mali za umma ilizojimilikisha kinyume na utaratibu.

HITIMISHO

Kwenye hotuba zake mbili Dk. Bashiru amefanya mambo kadhaa ya kuungwa mkono. Kwayo aungwe mkono. Yapo pia aliyoyapotosha ambayo ni muhimu kumkumbusha ili kuweka sawa mambo. Tusiache kumkumbusha.

Kuhusu ndoto yake ya kuinyoosha CCM, tunamtakia kila la heri. Lakini sioni akinusurika mbele ya vikundi maslahi ndani na nje ya chama chake ambavyo vitaanza upesi kumpunguza spidi na ikibidi kumwangamiza kwenye ramani ya kisiasa akibaki na ari hii.

Mwenyekiti wake pia ambaye sasa nina hakika anamuunga mkono, mbeleni atashindwa kuhimili utamaduni wa kujikosoa (self criticism) na atalazimika aidha kumpunguza spidi au Dk. Bashiru au kumuondoa.

Mimi ninaamini namna bora zaidi ya kuisaidia CCM ni kuipumzisha kwa sababu haisafishiki.

Ado Shaibu,
Katibu Mwenezi, ACT Wazalendo

Simu: 0653619906