MAISHA NI FUMBO LA MUDA
Em jaribu kuvuta picha, japo ni ngumu ila jaribu kuvuta picha siku ya kifo chako itakavyokua. Pengine utaitegemea au pengine itakua ya kushtusha. Lakini utakapofariki ndio utakua mwisho wa Maisha yako hapa duniani. Japo katika uhalisia utaendelea kuishi ndani ya mioyo ya wale watu wako wa karibu utakao waacha duniani. Kwenye mazishi yako lazima wasome historia yako. Kwa kawaida historia hii huwa kwa ajili ya kumpamba marehemu maana huku kwetu “maiti huwa haisemwi vibaya”. Lakini pamoja na waandishi wa historia yako kukupamba kwa maneno mazuri yatakayoashiria ushujaa na umahiri bado ukweli utabaki kuwa katika mioyo ya wale ambao umegusa Maisha yao.
Usiache kuvuta picha tuendelee. Hivi unadhani yatakayosomwa mbele ya hadhara kukuelezea ndio ambayo watakuwa nayo watu mioyoni mwao? Je watakaposema kwamba ulikua mtu anaeijali na kuipenda familia yake, mke na Watoto wako watakua na mtazamo sawa juu ya hilo? Je Watakaposema kwamba ulikua Rafiki mwema na mwenye upendo, wale uliowaita marafiki watakua na mtazamo huo huo?
Ukiwa bado upo kwenye tafakuri hiyo basi jiulize swali hili “je Maisha ninayoyaishi leo yataacha alama gani siku nikifa?” wengi wetu hatupendi kujibu hili swali kwani tunadhani kwamba hatutakufa mapema na tutayafanya mengi makubwa siku zijazo lakini kwa leo acha tuishi tuu vile tunavyojiskia.
Kila siku tunapoamka asubuhi na kuelekea katika mizunguko yetu ya kawaida tunasafiri katika treni ya muda. Japo itaonekana kuwa treni hii inasafiri polepole sana na wala haikikaribii kituo cha mwisho huwa inawashangaza wengi pale inapopiga honi kuashiria kwamba inaingia kituoni wakati mhusika hajajiandaa kushuka.
Kimsingi muda huamua mambo mengi sana katika Maisha yetu yaani kwa lugha nyingine Maisha tunayoyaishi yanatawaliwa na muda. Siku uliyoingia duniani na siku utakayoondoka tofauti yake ni muda, siku ya kuwa chini na ile ya kuwa juu zimetenganishwa na muda tuu. Kuna wakati unaweza kuwa tone tu baharini halafu wakati mwingine ukawa bahari yenyewe, ni suala la muda tuu.
Mungu aliacha suala la muda kuwa fumbo kwetu sisi wanadamu ili tuwe wanyenyekevu na wenye kufikiri kuhusu yale yajayo. Ikiwa hatufahamu litakalotokea kesho, je si vyema Zaidi kuwa watulivu na wenye busara leo?
Kesho inaweza kuwa anguko letu au ikawa ndio siku yetu ya kuinuliwa, lakini nani ajuaye isipokuwa Mwenyezi pekee? Nafasi na nguvu ulizonazo leo zimefichwa katika muda na laiti kama ungalijua siku ya kupokonywa vitu hivyo basi ungalifanya maandalizi. Lakini huwezi kujua ili ufanye makosa na baadae upate kujifunza kupitia makosa hayo. Lakini ni wangapi kati yetu ambao huchukua nafasi ya kujifunza pale wanapokosea? Tena iwe bahati maana kuna makosa ukifanya huwezi kuyarekebisha labda utaambulia uzoefu tuu.
Ni ngumu sana kuirejesha dawa ya meno ndani ya “tube” yake pindi utapokua umeibinya itoke nje lakini haiwezekani kabisa kurudisha muda nyuma. Nafahamu kuna wakati huwa tunatamani walau muda ungerudi nyuma ili utupe nafasi ya kufanya mambo Fulani kwa usahihi Zaidi. Pengine unatamani ungemuomba msamaha baba yako kabla hajafariki, au labda ungekuwa mtoto bora Zaidi na kumjali mama yako pindi alipokua hai. Pengine unatamani muda urudi nyuma na kukupa nafasi ya kurekebisha yale makosa ulomtendea mpenzi wako maana sasa hataki hata kukuona. Lakini muda ni katili sana na wala huwa hausikilizi malalamiko yetu. Muda huwa umeziba maskio kwa yale yaliokwisha pita maana ni mengi na pengine ni vema yakaendelea kubaki jinsi yalivyo maana pamoja na kutuletea machungu hutuletea pia mafunzo ambayo yanatusaidia kuishi vema leo na kujiandaa pia kwa ajili ya kesho.
Lakini pamoja na muda kuwa katili muda una upendo pia na ndio maana hutupa nafasi ya kuendelea kuishi huku tukiwa na hekima na busara Zaidi. Maisha ni fumbo la muda na ili tuweze kulifumbua fumbo hili basi imetupasa kuishi vema na kila mtu leo ili kesho muda wetu wa kushuka kwenye treni utakapofika, honi itakapopigwa tushuke huku kila mtu akitamani kwamba tungeendelea na safari ila ni muda tuu umefika. Natazama, nafikiri, naandika.
