Ben Mcharo
Nov 1 · 4 min read

UMEJIPANGA KUWALEA AU KUWAKUZA WATOTO WAKO?
Umeshawahi kusikia kuhusu kilimo cha mpunga kule Ifakara Morogoro? Kule mashamba uhakika halafu mvua hazisumbui yani kwenye ekari moja ukikosa sana una gunia zako 25 tufanye umeuza kwa bei ya chini 60,000 Kwa gunia, unapata 1,500,00 ukitoa gharama zako ulizoingia kama 600,000 una faida ya 900,000 Na hapo sio lazima sana uende shambani mambo yanajipa tuu. Vipi kuhusu ufugaji wa kuku wa mayai na nyama? Unaanza zako na kuku mia moja baada ya miezi sita au mwaka mmoja una kuku wako 2000 tayari umeshatoboa. Hii mifano na hizo namba zinaweza zisiwe sahihi sana lakini natumaini umeipata ‘point’ yangu.
Usishangae, sio kwamba nimekosea kichwa cha Makala hii, hapana sina mpango wa kukufundisha kilimo au biashara hapa. Kuna watu walifanya maamuzi ya kuingia kwenye kilimo au biashara kutokana na hadithi za kuvutia kama ulizoziona hapo juu. Sio kwamba wote waliojaribu kufanya walishindwa lakini wengi walishindwa na hii ilisababishwa na kufanya kilimo au biashara kwa kutumia simu wakiamini kwamba mambo “yatajipa tuu” na wataamka matajiri. Hata mimi binafsi nilishawishika ila tuu sikuwa na mtaji wa kufanya kilimo cha kwenye simu. Kuna vitu ili ujifunze unahitaji kuvipitia wewe mwenyewe wazungu wanasema “experience is the best teacher” yaani uzoefu ni mwalimu bora Zaidi.
Kinachosabibisha kilimo au biashara za kufanya kwa simu zifeli pamoja na sababu nyingine ni kukosekana kwa uangalizi wa karibu wa mmiliki wa biashara au shamba husika. Huwezi kutegemea kufanyiwa 90% ya usimamizi wa shamba lako halafu utegemee faida, hizo ni ndoto za mchana tena unakuta wewe ndio mara yako ya kwanza kufanya hivo.
Jamii yetu kwa sasa ina changamoto nyingi lakini moja wapo ni ongezeko kubwa sana la Watoto wa mitaani. Watoto ambao pengine wana wazazi ila hawana walezi. Pia kuna ongezeko kubwa sana la Watoto wanaolelewa na mzazi mmoja, mara nyingi mama. Ukiachana na kifo sababu zinazofanya kuwepo kwa ongezeko hili la Watoto kulelewa na mzazi mmoja ni ndoa kuvunjika, mtoto kuzaliwa nje ya ndoa au kuzaliwa na wazazi ambao hawako tayari kuoana. Pamoja na makundi hayo yote bado kuna lile kundi ambalo mtoto ana wazazi wote wawili na wapo pamoja lakini wako “busy” sana kwahiyo mtoto anatumia muda mwingi/analelewa na dada wa kazi.
Kama ilivyo kwenye kilimo au biashara za kwenye simu ndivyo ilivyo kwenye swala zima la malezi ya mtoto/watoto. Unakutana na mwanamke au mwanaume wa ndoto zako mnapendana kweli kweli mnaamua kuoana na kabla hamjajua tayari mshapata mtoto wa kwanza. Kumbe hamkua tayari na mnaanza kuona kama vile mtoto anawapora uhuru wenu, mnaamua kutafuta msaidizi “dada wa kazi” ili awalelee mtoto wenu na nyie muendelee kuishi Maisha mnayoyataka.
Pamoja na kwamba mpo kwenye mahusiano na mnayafurahia sana siku ikitokea mimba mambo yanabadilika maana boyfriend wako hayuko tayari kuitwa baba, anaikataa mimba. Ila kwasababu wewe hutaki kutenda dhambi ya pili ya kuua achana na ile ya uzinzi ambayo sahivi wala huikumbuki. Unaamua kutunza mimba kwa msaada wa mama maana baba hataki hata kukuona “umemuaibisha”, unajifungua mwanao salama na unapambana kumlea pekeako huku ukifanya na majukumu mengine, jina linabadilika na unaitwa “single mum”. Kubali au kataa lakini mtoto anawahitaji wazazi wote wawili muda wote. Pengine kabla hatujafanya maamuzi ambayo yatawaathiri na watu wengine ikiwemo Watoto wetu ambao hatujawazaa bado ni vema tukajua kama tuko tayari au la.
Kuna wazazi ambao walitelekeza Watoto wao tangu wakiwa wadogo na wapo ambao walikataa mimba lakini mtoto anapokua na kufanikiwa mzazi yuleyule anarudi kumtafuta mtoto ili apate msaada. Kimsingi mzazi atabaki kuwa mzazi tuu lakini katika mazingira kama haya anakua amechangia vinasaba tu vya mtoto na si vinginevyo. Unahitaji Zaidi ya vinasaba kuwa mzazi, unahitaji Zaidi ya kumpa mtoto jina la mwisho kuwa baba yake. Uwepo wa wazazi ni muhimu sana, na hapa simaanishi kuwepo tuu nyumbani na kutumia muda wako wote kwenye simu yako. Unaweka picha ya mwanao mtandaoni inapata “likes” na “comments” kibao lakini malezi halisi ya mwanao anafanya dada wa kazi. Wakati tunaouendea utakua na changamoto nyingi kuliko wakati uliopita.
Wazazi wetu walikua wana kazi ya kutuzuia tusiingie kwenye mapenzi katika umri mdogo maana walijua kuwa yataathiri Maisha yetu ya mbele. Lakini sisi tutakapokua wazazi (wazazi wa kisasa) tutahitaji uangalifu Zaidi ya huo maana tutahitaji kuwalinda Watoto wetu sio tu dhidi ya mapenzi katika umri mdogo lakini mapenzi ya jinsia moja ambayo ni kinyume na maadili yetu. Wakati wa kukua kwetu mitandao haikuwepo kwa kiasi kikubwa kama ilivyo kwa sasa, tulifanya michezo uwanjani na kwenye baraza za majirani zetu. Kimsingi tulihitaji kutoka nje ili tuweze kufurahi pamoja na Rafiki zetu. Ila kwa sasa mtoto anaweza asitoke kwenda kuzurura lakini bado akawa kwenye hatari ya kuharibika na kuwa na tabia zisizofaa. Unaweza kudhani kwamba mwanao yupo ndani anaangalia tu katuni kumbe yupo darasani anafundishwa mila na desturi mpya.
Tusitegemee kufanya malezi kwa mtindo wa “remote control” halafu tutarajie kuwa na Watoto bora au kizazi bora chenye watu waliostaarabika hapo baadae. Huyo dada wa kazi ambae unamtegemea akusaidie kumlea mwanao naye hakupata malezi ya kutosha kwahiyo unajua matokeo yatakuaje. Na unapoikataa mimba uliyoisababisha unatengeneza mazingira ya mtoto wako wa kike kulelewa katika chuki na kukua huku akiamini kwamba wanaume wote ni wabaya. Lakini sio lazima kila mtu awe na mtoto maana kuna faida gani kuzaa mtoto ambaye hutoweza kumlea? Tujiandae kuwalea Watoto wetu ili waweze kukua katika njia iliyo sahihi. Natazama, nafikiri, naandika.

    Ben Mcharo

    Written by

    And from silence all my writings arise In the midst of chaos I write about calmness

    Welcome to a place where words matter. On Medium, smart voices and original ideas take center stage - with no ads in sight. Watch
    Follow all the topics you care about, and we’ll deliver the best stories for you to your homepage and inbox. Explore
    Get unlimited access to the best stories on Medium — and support writers while you’re at it. Just $5/month. Upgrade