Hatutauzima mtandao kufuatia maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha 2024, Mamlaka ya Mawasiliano nchini Kenya (CA) yasema
Katika mkesha wa maandamano nchini Kenya yanayoongozwa na vijana wa kizazi kipya — almaarufu Gen Z, yanayolenga kupinga Mswada wa fedha uliopendekezwa na serikali, kulizuka tetesi za kuwepo mipango wa kuzima mtandao ili kulemaza jitihada za maandamano hayo.
Hali hii ilipelekea Mashirika ya Kiraia yakiwemo KICTANET, Paradigm Initiative, Internet Society Kenya Chapter, na CIPESA, kutoa tamko la pamoja lililoelekezwa kwa serikali, na kuitaka ijizuie kufunga mtandao wakati wa maandamano yaliyopangwa kwani hii ingekiuka katiba ya Kenya na sheria za za kimataifa za haki za binadamu.
Tamko hili la pamoja lilisisitiza kuwa kuzima kwa mtandao kungeweza kuwa na athari mbaya kwa uchumi wa nchi, haswa kwenye soko la biashara ya mtandaoni — inayokadiriwa kuwa dola za Kimarekani milioni 801, miamala ya mtandaoni kama vile benki, na ufikiaji wa habari.
Kufuatia tamko hili,Mamlaka ya Mawasiliano nchini Kenya (CA), kwenye taarifa kwa vyombo vya habari iliyochapishwa kwenye mtandao wa X (zamani ukifahamika kama Twitter), ilipuuzilia mbali tetesi hizi za kuwepo kwa mipango ya kuzima mtandao kabla na wakati wa maandamano hayo yaliyopangiwa kufanyika mnamo Jumanne.
Mkurugenzi Mkuu wa CA David Mugonyi aliwahakikishia Wakenya kuwa serikali haikuwa na mipango kama hiyo.
“Mamlaka ya Mawasiliano ya Kenya (CA) imepokea maswali kuhusu mpango wa kuzimwa kwa mtandao siku ya Jumanne, Juni 25, 2024,” Mugonyi alisema kwenye taarifa hiyo kwa vyombo vya habari.
“Kwa kuepusha shaka, Mamlaka haina nia yoyote ya kuzima trafiki ya mtandao au kuingilia ubora wa muunganisho.”
Mugonyi alisema vitendo kama hivyo vingekuwa usaliti wa Katiba kwa ujumla na vilevile vingekiuka uhuru wa kujieleza na miiko ya Mamlaka hiyo.
Aliongeza kuwa serikali imejitolea kuhakikisha uchumi wa kidijitali unaimarika na kwa hivyo, kuzima mtandao kungeweza kurudisha nyuma mafanikio yaliyopatikana katika sekta hii.
“Zaidi ya hayo, vitendo kama hivyo pia vitaharibu uchumi wetu wa kidijitali unaokua kwa kasi kwani muunganisho wa Intaneti unasaidia maelfu ya maisha nchini kote,” alisema.
“Hata hivyo, tunawahimiza Wakenya kutumia majukwa ya kidijitali kwa heshima kwa wote na ndani ya mipaka ya sheria.”
Kufuatia taarifa hii, Mkurugenzi Mkuu wa Paradigm Initiative (PIN), Bw. ‘Gbénga Ṣẹ̀san, alikuwa na hili la kusema katika chapisho kwenye akaunti yake ya X: “Mashirika ya kiraia yanapoibua wasiwasi, hufanya hivyo kwa maslahi ya kila mtu — ikiwa ni pamoja na maafisa wa umma ambao kwa kawaida huwa wanapokea taarifa kama hizi. Njia moja ya kutojibu ni kutoa kauli zisizo na mnato. Kuna cha kujifunza kutokana na ubadilishanaji huu.”
Kwa wiki ya pili sasa, Kenya inaendelea kushuhudia wimbi la maandamano makubwa yaliyowapa ujasiri vijana kuingia mitaani jijini Nairobi na katika miji mingineyo nchini, kupinga mapendekezo tata ya serikali ya Mswada wa Fedha wa 2024.
Kwenye jukwa la X, midahalo mingi imeandaliwa na wanamitandao maarufu na wanajamii (maarufu kama KOX), huku wengi wakielezea kukerwa kwao na Mswada huo uliopendekezwa, na unaopigiwa upato na Rais Ruto aliyepewa jina la utani la “Zakayo” — mkuu wa watoza ushuru kwenye Bibilia.
Kibwagizo cha #RejectFinanceBill2024 kimekuwa kikivuma nchini na kimataifa.
Japo serikali imefaulu kubatilisha baadhi ya mapendekezo katika mswada huo kufuatia kilio cha waandamanaji, Wakenya wanasisitiza kuwa mswada huo unapaswa kutupiliwa mbali kutokana na hali ngumu ya kiuchumi, ambao bado unayumba kufuatia athari za UVIKO -19.
Vile vile, viwango vya maisha vimedorora na tatizo la ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana limezidi kuwa kitendawili kisichoweza kuteguliwa.
Wakati wa uchapishishaji makala haya, kulikuwa na ripoti kwamba bunge la Kenya lilikuwa tayari limepitisha mswada huo tata wa fedha.
Kwa kuwa uko hapa…
Iwapo umeyapenda makala haya na ungependa kuona maudhui zaidi ya Kiswahili kwenye blogu hii na au chaneli yangu ya YouTube, tafadhali fuata, penda, shiriki maoni, na iwapo itakupendeza pia, unaweza kunichangia tipu ya 50€ na au ujiunge nami kama mhisani mkuu kwa kiasi cha 200€ tu ili uniwezeshe kuendelea kujitolea muda wangu kuandika makala yenye kusisimua na yanaoelimisha.
Paypal yangu: bswitaba [at] yahoo.co.uk
Zingatia: Wahisani watapewa shukrani na sifa sufufu.