Elias Maeda
4 min readSep 19, 2019

MJUE REBECA GYUMI. (EXTENDED INTERVIEW)

Mapema mwaka huu nikiwa na jarida la Daladala,tulibahatika kufanya mahojiano na mrembo huyo aliyekava toleo la kwanza la jarida hilo ambaye kimuonekano,ujasiri alionao na jinsi anavyoongea kiingereza kizuri,huenda ukasema anatokea kwenye familia ya kishua(kitajiri); la hasha,amezaliwa kwenye familia yenye uchumi wa kawaida. Amesoma shule za serikali kuanzia shule ya msingi Mazengo,shule ya kata Kikuyu,shule ya sekondari Kilakala na kumaliza chuo kikuu cha Dar-Es-Salaam. Mama yake alikuwa ni mama wa nyumbani aliyejihusisha na biashara ndogondogo huku baba yake alistaafu yeye akiwa na umri mdogo.

Huyo ni Rebeca Gyumi anaekiri kuwa kutowekewa 'ukuta' na wazazi wake,jamii aliyokulia,fursa,changamoto,karama na kipawa cha kuongea vimemjenga zaidi kufika mahali alipo. Hadi sasa Rebeca na asasi yake ya 'Msichana Initiative' wanatambulika kimataifa na wamepokea tuzo lukuki kama pongezi kwa kile wanachokifanya.

Mahojiano yetu yalikuwa kama ifuatavyo:

Classmate : Rebecca unaonekana ni mtumiaji mzuri sana wa mitandao !
Rebeca : Natumia kiasi; natumia kwa manufaa kama kukutana na rafiki zangu,kuhamasisha na kuonyesha kazi ninayofanya.

Classmate: Wewe ni moja ya vijana ambao mnaendesha mashirika makubwa nchini, Msichana Initiative;Hongera. Kwanini ni 'Msichana' ?
Rebeca: Mtoto wa kike hukumbwa na changamoto nyingi zaidi. Tukiangalia kama elimu,changamoto kama hedhi,mimba na ndoa za utotoni humfanya asipate fursa ya kupata elimu bora.

Classmate: Mbali na elimu,ni changamoto gani nyengine mmeiwekea mkazo kwa msichana ?
Rebeca : Tunaamini elimu ndio 'entry point',zaidi tunaangalia changamoto zinazomfanya msichana akose elimu. Tunaamini katika elimu.

Classmate: Mnawezaje kumaliza changamoto ya msichana mjamzito kukosa haki yake ya elimu ?
Rebeca : Tunapambana kwa nafasi mbili;kwanza kuisihi serikali kupitia mheshimiwa raisi kuruhusu wasichana wajawazito kurudi shuleni na pili kutumia vilabu tunavyoanzisha kuwahusisha wasichana na mafunzo na elimu ambavyo vitawahamasisha na kuwaaminisha kuwa maisha yanaweza kuendelea.

Classmate: Wewe ni kiongozi wa namna gani ?
Rebeca: Mimi nina unoko 😅😅😅. Natania tu. Mimi ni mtu ambaye naamini sana katika uongozi shirikishi. Siwezi pekee yangu. Napenda kusimamia ukweli na uadilifu

Classmate: Muitikio wa wasichana na wanawake kwenye kupambania haki zao ukoje ?
Rebeca : Tunaelekea kuzuri,lakini tuna kazi kubwa. Kuna ambao hawawezi kusema na kufikia ndoto zao,safari ni ndefu.

Classmate: Msichana Initiative inaonekana ni 'non-profit organization',je mnanufaika vipi ?
Rebeca : Kutokupata faida ni kwamba hatufanyi kazi halafu tuhesabu faida,ila tuna washirika,wahisani,wafadhili ambao tunawapatia bajeti ya kukidhi mahitaji yetu. Sheria ndio inavyotaka.

Classmate: Mbali na shughuli hii unayofanya kuna shughuli nyengine ?
Rebeca : Mara chache nafanya ushauri kwa mashirika,makampuni,uchambuzi hivyo huniingizia kipato kando. Ila zaidi najihusisha na Msichana.

Classmate:Unawapokeaje vijana wanaokuja kwako wakihitaji msaada ?
Rebeca: Tulianzisha jukwaa la fire side chat kwa wasichana. Napenda kuwasikiliza na kuwashauri. Napatikana muda wote.

Classmate: Unapenda umaarufu ?
Rebeca: Sidhani,kwa nafasi nilizopita ningekuwa maarufu zaidi kama ningetaka iwe hivyo.

Classmate: Watu wanaojihusiha na mambo ya kijamii huwa na maisha flani ya chini au ya kawaida. Yaani ni aghalabu kukutana nao club au bar !
Rebeca: Watu wamechelewa kunijua,Mimi nimeruka 😅😅😅. Hayo mambo nilifanyaga. Na inabidi tufanye utafiti kidogo,wapo wanaoenda club ila kwa vile hatufahamiki ni ngumu kujua kuwa tunaenda.

Classmate: Ivi kuna ushindani baina ya mashirika ?
Rebeca: Sijui kama kuna ushindani ila kwangu hapana. Sote jukumu letu ni moja kukuza jamii.

Classmate: Mara nyingi tumekuwa tukiona mashirika haya yakitegemea msaada kutoka kwa mataifa ya nje !
Rebecca : Kwenye sekta ya kiraia,mashirika mengi ya nje yana sapoti kubwa. Ila pia Tanzania yapo kama Foundation for civil society. Tujikite kwenye kuonyesha matokeo,watuamini kuwekeza kwetu.

Classmate: Na je ni sahihi shirika kuingiza kipato mbali na kutegemea wafadhili ?
Rebeca: Sheria yetu inatubana. Kama shirika ni 'non-profit' halitakiwi kuwa na mradi mwengine zaidi ya hiyo(ya kuingiza faida).

Classmate: Ni sahihi elimu ya ngono kutolewa shuleni ?
Rebeca: Naamini elimu ya ngono ni muhimu sana. Watoto wapewe elimu sahihi.

Classmate: Swali gani sijakuuliza na ungependa watu wafahamu ?
Rebeca: Hapana,umejitahidi kuuliza maswali yote. Labda changamoto,levo ya shirika linapoanza watu wanakuwa na mategemeo makubwa sana. Na swala la haki za wasichana au wanawake ni mada zisizopendwa kwenye jamii.

Rebeca anasisitiza kuwa 'namshukuru Mungu,Femina walinipa part-time contract. Nilikua napata vijisenti kidogo. Femina imenijenga sana,sio tu kunipa mchango wa kifedha bali pia kuniwezesha kufika hapa nilipo’.

Kama kuna swali lolote nilisahau kumuuliza na ungependa kupatiwa majibu,unaweza kuliweka hapa nami nikuahidi kumuuliza siku nikionana nae au kuwasiliana nae. Shukran kwa kupitia makala hii,usisahau kunifuatilia kwenye kurasa zangu za Twitter na Instagram nikitumia @classmateTz.

Picha zote kwa msaada wa Instagram ya Rebeca Gyumi.

Elias Maeda

Passionate about using media for social change. Part time Afro-rapper/ Full time food lover.