HADITHI FUPI: Marafiki Wawili

SIKU MOJA MARAFIKI wawili walikuwa wakitembea jangwani. Safari ilikuwa ndefu, yenye kuchosha vilivyo. Kutembea juu ya mchanga wa jangwani, wenye joto kali, lilikuwa jambo lenye kuumiza sana. Wakati wakitembea, waliendelea na michapo ya hapa na pale. Basi katika michapo hiyo, wakaanza kubishana. Ubishani ulianza kidogo, ukaongezeka, na kukua hata mmojawapo kukasirika sana. Akiwa katika hali hiyo ya kukasirika, akamchapa mwenzake kofi la nguvu.
Aliyechapwa kofi aliumia sana, hata machozi kumtoka. Lakini, hakusema kitu. Badala yake, akaandika kwenye mchanga, “Leo, rafiki yangu mkubwa amenichapa kofi usoni pangu.”
Wakaendelea na safari yao pasipo kusemezana kabisa. Huko mbele, wakaona kisima. Kutokana na uchovu wa safari, wakaanza kuoga. Bado, hawakuwa wakisemeshana. Basi, ikatokea, rafiki yule yule aliyechapwa kofi hapo awali, akateleza na kutumbukia kisimani. Kisima kilikuwa kirefu sana. Lakini, kabla hata hajafika mbali, yule mwenzake akamdaka mkono. Akatumia nguvu zote kumvuta hata akafanikiwa kumwokoa. Akamlaza pembeni na kumsaidia huduma ya kwanza. Mhanga yule alipotulia na kurejea kwenye hali yake, akaandika kwenye jiwe kwa wino usiofutika. Maandishi yake yalisema, “Leo, rafiki yangu mkubwa ameyaokoa maisha yangu.”
Rafiki yule, ambaye awali alimtandika mwenzake kofi la uzamivu, akamwuliza, “Nilipokupiga kofi na kukuumiza, uliandika kwenye mchanga, na sasa, umeandika kwenye jiwe. Ni kwa nini?”
Akamjibu, “Pale inapoondokea mtu fulani akakuumiza maishani, unapaswa kuyaandika masononeko yako mchangani, ili pindi upepo wa kusamehe unapovuma, maandishi hayo yafutiliwe mbali. Lakini, pale inapoondokea mtu akakutendea jambo jema, unapaswa kuuandika wema huo kwenye jiwe, ambako hakuna upepo duniani, utakaoweza kuyafuta maandishi hayo.
Rafiki yule mchapakofi akayastaajabia maneno ya rafikiye. Akamwambia mwenzake, “Kumbe, sipaswi kuvithamini vitu nilivyonavyo maishani, bali, kuwathamini watu nilionao maishani.”
Mwenzake hakumjibu. Yungali akiyatafakari maneno yale.
Fadhy Mtanga,
Dar es Salaam.
Jumapili, Novemba 3, 2019.
