VoG Africa
4 min readSep 23, 2021

Tanzania yazidi kupaa kiuchumi

WAKATI uchumi wa Tanzania ukitajwa kukua kwa kasi kwa miongo miwili mfululizo na kupelekea kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi wa kati (wastani), imeelezwa kuwa huenda nchi tajwa ikachukua hatamu ya kuwa nchi yenye uchumi mkubwa zaidi kuliko nchi zingine za Afrika Mashariki kwa muongo mmoja ujao. VoG inaripoti
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wataalamu wa masuala ya uchumi nchini, wameeleza sababu zinazopelekea uchumi wa Tanzania kupaa kwa kasi licha ya changamoto ya UVIKO ambayo imeteteresha chumi za nchi mbalimbali duniani.
Akifafanua kwa utuo, moja ya wataalamu wa masuala ya uchumi nchini ambaye hakutaka jina lake litajwe, anasema kuwa, uchumi wa Tanzania umekuwa ukikua kwa kasi kwa kipindi hicho chote kutokana na sababu kubwa nane.
Akibainisha sababu hizo, mchumi huyo, anasema uchumi wa Tanzania unakua kwa kasi pasi kukwama kutokana na kwamba kumekuwa na sekta nyingi zinazo changia uchumi kukua kama: sekta ya madini, kilimo, utalii, viwanda pamoja na biashara.
Anaeleza kuwa, nchi zingine ikiwemo za jumuiya ya Afrika Mashariki uchumi wake wakati mwingine kasi ya ukuaji hupungua kutokana na kutegemea sekta moja au kuwa na sekta chache zinazochangia uchumi wa nchi zao.
Akitaja sababu zingine anasema kuwa, ni uwepo wa Bandari ambayo inahudumia nchi nyingi zinazoizunguka ambazo hazina hduma hiyo, jamabo ambalo linasaidia kukusanya mapato na kufungua milango ya biashara.

Bandari ya Dar es Salaam

Anaednelea kubainisha kuwa, uongozi mzuri ambao umeweka maslahi ya umma mbele zaidi pamoja na tunu ya amani ni moja ya vichocheo vya uchumi kukua.
“Wawekezaji wamekuwa wakija kwa wingi nchini kutokana na uhakika wa amani na usalama,” anasema Mchumi huyo
Pia, anabainisha kwamba, kukua kwa biashara kati ya Tanzania na nchi za kigeni ikiwemo za Afrika Mashariki, kwani mpaka sasa Tanzania imeuza mazao mengi ya chakula hususani mahindi kwenye nchi ya Kenya na Uganda kuliko bidhaa zilizoingizwa na nchi tajwa nchini Tanzania.
Aidha, anapongeza ziara zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan, kwenye nchi mbalimbali kwani zimesaidia kukuza sekta ya biashara.
“Kasi kubwa aliyoiweka rais kwenye kutembelea nchi jirani, kile kitu ni kitu kizuri sana, kwa sababu alipokwenda tu Kenya na kurudi, ...Idadi ya mazao ya chakula yaliyouzwa Kenya iliongezeka kwa takribani mara nane,” anasema mchumi huyo huku akibainisha kwamba hayo yote ni matokeo ya mahusiano mazuri ya kidiplomasia nan chi jirani
Anataja kuwa, idadi kubwa ya watu hasa rika la vijana ambao wamejikita katika uzalishaji na sio utegemezi ni miongoni mwa sababu zinazosaidia uchumi wa Tanzania kukua.
Hata hivyo anaweka bayana kwamba, vivutio kwa waekezaji kama punguzo la utitiri wa kodi au tozo na kutoa maeneo ya uwekezaji bure ni moja ya mambo muhimu yaliyosaidia uchumi wa taifa tajwa kuendelea kukua.
Mchumi huyo, anakwenda mbali zaidi kwa kubainisha kuwa, uchumi wa Tanzania umestahimili kipindi cha janga la UVIKO kutokana na kwamba watu hawakufungiwa ndani (lockdown), hivyo waliendelea na shughuli za uzalishaji mali.

Mwonekano wa daraja la kijazi lililopo Ubungo Dar es Salaam

Hata hivyo wananchi wamekuwa wakilalama kuwa, licha ya uchumi wa nchi kutajwa kukua bado haujawa na matokeo chanya kwao kwani bado hali zao za maisha ziko chini na haziendani na kile kinachotajwa kwenye takwimu za uchumi wa taifa.
Akijibu hoja hiyo, Mchumi Vasco Mbisse, anakiri kuwa ni kweli chanagamoto hiyo ipo kwenye nchi nyingi barani Afrika, na hiyo ni kutokana na nchi nyingi kuwekeza nguvu kubwa kwenye kukuza uchumi wa nchi au pato la taifa (economic growth), kuliko mwananchi mmoja mmoja (economic development).
“Unaonekana unakua,...Lakini unapokuja kwenye hali ya kawaida ya maisha ya watu (social welfare), ni mbaya, na hiyo ni kwa sababu pato la taifa ndilo linalokua na sio pato la mwananchi mmoja mmoja,” anasema Mchumi huyo
Aidha, anaendelea kubainisha kuwa, uchumi wa Tanzania unakua kwa sababu unachangiwa na watu wa chache wenye kipato cha hali ya juu (mamilionea) waliopo, hivyo wananchi wa hali ya chini hubaki kama walivyo pasipo mabadiliko ya kiuchumi.

Ramani ya mradi wa bwawa la umeme la Nyerere

Hata hivyo anaeleza kuwa, kwa upande wa sekta ambazo zimechangia kwa sehemu kubwa kukua kwa uchumi ni sekta ambazo haziajiri idadi kubwa ya watu, kama madini na utalii.
Anakwenda mbali kwa kubainisha kuwa, kwa sekta ya kilimo ambayo inaajiri idadi kubwa ya Watanzania ukuaji wake uko chini, ndio maana watu wengi bado hawajaguswa na ukuaji wa uchumi, kwani wanaoguswa na kukua kwa uchumi ni wale wanaofanya kazi kwenye sekta zinazokua.
Vasco Mbisse, anaeleza kuwa, njia rahisi inayoonyesha kuwa uchumi wa wananchi wa kawaida bado uko chini licha ya kukua kwa uchumi wa taifa ni idadi kubwa ya watu ambao hawana ajira hususan vijana.
Aidha, mchumi huyo, anaishauri serikali kuwa, licha ya uchumi wa taifa kukua, ipo haja ya kuelekeza nguvu kwenye kuweka mikakati ya kuinua uchumi wa mwananchi mmoja mmoja.
Kwa mujibu wa takwimu za Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF), zinatabiri kuwa ifikapo 2022, uchumi wa Kenya utakua kwa dola za Kimarekani bilioni 113, huku watanzania ukionekana utakua kufikia dola bilioni 78, hivyo Kenya itakuwa ikiipiku Tanzania kwa asilimia takribani 30.
Sambamba na hayo, miongoni mwa sababu zingine inaelezwa kuwa, kukua kwa uchumi wa Tanzania ni kutokana na serikali kuwekeza nguvu kubwa kwenye kupiga vita rushwa, ufisadi, ubadhirifu, miundombinu, uwajibikaji na matumizi ya raslimali za taifa kwa maslahi ya umma au jamii.

VoG Africa
VoG Africa

Written by VoG Africa

Owner: Getson Sanga Contact: +255 765 323 855/ +255 620 442 916 E-mail: getsonedson@gmail.com Location: Dar es Salaam - Tanzania

No responses yet