Timu ya Hatua ikielezea Mradi kwa Mwenyekiti Manispaa ya Sengerema, Ndugu Silvanus Bulapilo.

Mradi wa Hatua: Jitihada za kuimarisha ushiriki wa wananchi katika ngazi za utawala

Imeandikwa na Mujuni Baitani

Ushiriki wa wananchi katika ngazi za awali za Utawala inahusisha wananchi kutathmini mahitaji yao wenyewe na kushiriki katika mipango ya miradi endelevu na kuhakikisha ufuatiliaji wa miradi hiyo. Kuna umuhimu wa kuboresha usimamizi wa rasilimali za umma, kwa kufanya watumishi wa umma na viongozi kuwajibika kikamilifu. Zimesemwa njia na hatua mbali mbali ila hakuna jambo bora kama ushiriki wa wananchi kufanya kazi kwa ushirikiano na viongozi wao. Hii ni mmoja ya sababu ya uwepo wa Mradi uitwao, “Hatua”.

Timu ya Hatua wakishiriki mkutano wa kijiji cha Sima, Sengerema

Hatua ni mradi wenye ubunifu wa kukuza ufanisi katika kuimarisha ushirikiano bora baina ya watawala na watawaliwa. Hatua ni jitihada endelevu yenye kuhakikisha waamuzi wanashirikiana ipasavyo na wananchi katika kutatua changamoto zinazopelekea kudorora kwa jamii husika. Mradi huu una fadhiliwa na Making All Voices Count, HIVOS kwa kushirikiana na Sahara Sparks pamoja na Buni Hub. Mradi huu unatambua hali halisi ya jamii za kitanzania hivyo umedhamiria kujenga mahusiano endelevu katika ngazi zote za utawala kwa kuanzaa na Ngazi za awali.

Timu ya Hatua wakishiriki katika kikao cha kijiji cha Sima, Sengerema

Ushiriki wa wananchi na viongozi unahitaji uaminifu na imani. Kujihusisha kwa wananchi katika serikali za mitaa inaboresha uwajibikaji na uwezo wa serikali za mitaa katika kutatua matatizo. Mradi huu umejikita pia katika kujenga jamii yenye umoja na mshikamano, ikiwa ni kuhakikisha ongezeko la idadi ya mipango kutokana na mapendekezo ya wananchi. Hii ni moja ya njia ya kuongeza ufahamu na kuwawezesha wananchi kuwa na sauti kupitia majukwaa na nyenzo tofauti za kiteknolojia. Uwezo wa nyenzo na majukwaa haya ni kufungua nafasi kwa mjadala na mazungumzo ya kuboresha uwazi na kuimarisha utawala bora.

Mradi huu utajenga uwezo kwa watazania wengi kuelewa na kushiriki katika utawala bora, na maendeleo. Yote ikiwa ni hatua za kuhakikisha wananchi wanakuwa na mitazamo chanya na kushiriki ipasavyo katika kujenga jamii zao wenyewe.

One clap, two clap, three clap, forty?

By clapping more or less, you can signal to us which stories really stand out.