Michael Neligwa
5 min readNov 5, 2018

*KILIMO CHA GMO: KITAFUTA MAFANIKIO YAKO RAIS MAGUFULI•*

*HII NI BARUA YA WAZI*•

Harid Mkali, (mkali@live.co.uk).
London, Uingereza.

Mheshimiwa Rais,

Katika miaka hii mitatu ya uongozi wako umefanikisha mambo mengi kupita maelezo; wakati mwingine yanasomeka kama miujiza. Lakini kubwa kupita yote ni urejeshaji wa raslimali zetu kwenye mikono ya wananchi ambako Mwalimu Nyerere alizihifadhi .

Raslimali hizo ni pamoja na: madini, ardhi, maji, mbuga zetu za wanyama, mashirika yetu ya umma nk nk.

Hili linawauma sana hawa manyang’au wa nje na ndani ambao kwa muhula wa miaka 30 waliifanya Tanzania kama nchi ambayo haina wenyewe au mali yao binafsi. Lakini manyang’au hawa wamepania kurudisha raslimali zetu mikononi mwao kwa mara nyingine ima fa ima.

Na inaelekea huenda watafanikiwa, kupitia kilimo cha GMO. Je, watafanikishaje?

Katika nchi za Afrika na Dunia ya Tatu jamii ya watu ambao walikuwa kweli huru na walijitegemea katika maana halisi ya neno hili walikuwa ni wakulima, hususani wakulima wadogo.

Hawa walikuwa na mashamba yao; walitumia nguvu kazi kulima mashamba hayo na, mvua zilishuka kwa rehema za Mwenyezi Mungu. Kama Serikali zao ziwasaidia ilikuwa ni heri na kama hazikuwasadia ilikuwa ni kitu kilekile. Walijitegemea katika jinsi yao ya kujikimu.

Hizi nadharia za kitapeli za ‘international interdependence & globalisation’ wala hazikuwagusa wakulima wadogo kabisa. ‘They were truly independent even from their own governments except, perhaps, for the purposes of taxation’.

Uhuru huo wa Wakulima ndio uliotafsiri Uhuru wa Mataifa haya ya Afrika na Dunia ya Tatu.

Leo, miaka zaidi ya 50 baada ya Uhuru, uhuru uliopatikana kwa kumwaga damu, Viongozi huru wa Afrika ikiwa ni pamoja na nchi yetu ya Tanzania inakumbatia sera zinazofuta kabisa Uhuru wa Wakulima na kwa mwendelezo uhuru wa Taifa wa Chakula (National food sovereignty).

Na nchi ambayo haina uhuru wa chakula huwa haina Uhuru mwingine wowote. Na hili hatujitaji mtu mwenye PhD aje kutufafanulia.

*KILIMO CHA GMO*•

Mheshimiwa Rais Magufuli,
Chini ya kilimo cha GMO wakulima wa Watanzania watapigwa marufuku kuhifadhi mbegu za kupanda msimu ujao, ili wategemee kununua kutoka kwa makampuni ya kigeni. Pia hawaruhusiwi kupeana ua kuuziana hizo mbegu. Kwani kwa kufanya hivyo wanapunguza faida ya makampuni ya kigeni yatakayotuuzia mbegu zenyewe.

Yaani mkulima amezinunua hizo mbegu lakini zinabaki kuwa mali ya mtu ambaye amemuuzia . Hivi hiyo process inaleta maana?

Kwa mujibu wa Sheria za Tanzania zilizopitishwa na Bunge letu la Awamu ya Nne, faini ya “makosa” haya ni: miaka 12 jela au dola za Marekani ($230,000) au yote mawili.

Tangu kilimo kianze duniani miaka 10,000 iliyopita kuhifadhi mbegu haijawahi kuwa ni kosa la jinai. Sheria ya aina hii ni dhahiri inanyanyasa na kusaliti wakulima na kwa mwendelezo inasaliti Uhuru wetu wenyewe.

*Kilimo cha GMO* kinawafanya wananchi wetu wawe watumwa kwa makampuni ya mbegu na madawa ya kilimo.
Mheshimiwa Rais ume-‘risk’ kila kitu katika miaka yako mitatu madarakani ili kurudisha raslimali za nchi mikononi mwa Wananchi.

Lakini ukiwaweka wananchi hao mikononi mwa makampuni ya GMO hicho ulichokiweka mikononi mwao kitakuwa ni mali ya haya makampuni yatakayokuwa yawamiliki hawa wananchi wako kupitia utumwa wa kilimo cha GMO. Kwani mtoto wa mtumwa huwa naye ni mtumwa.

Wewe umeokoa raslimali za Taifa na kuziweka mikononi mwa Wananchi wako. Hawa manyang’au watawateka hao wananchi pamoja na raslimali uliziwakabidhi. What a coup?

Kwa mujibu wa Gazeti la *The Guardian* la tarehe 2/11/2018, “watafiti” kutoka huko Makutupora watakuja kwako ‘within a month’ kuomba idhini ya Serikali yako idhinishe huu usaliti wa kuingiza kilimo hiki haramu hapo nchini.
Rejeo ifanywe katika makala haya:
“New push in pipeline for acceptance of GMO seeds”.

Utafiti wa Umoja wa Mataifa uliochukuwa miaka minne na kufadhiliwa na Benki ya Dunia, ulioendeshwa na wanasayansi 400 waliobobea kutoka nchi 110 duniani unasema: hiki kilimo hakina tija na kinahatarisha Uhuru wa chakula wa mataifa pamoja na afya za watu na mazingira yao. Na katika nchi 58 zilizoidhinisha hiyo Ripoti - *(Agriculture at a crossroads)* Tanzania ni mojawapo.

Tafiti za kitaifa za Uingereza, Ufaransa, Austria, Urusi nk nk zote zinakubaliana na matokeo ya Umoja wa Mataifa.

Real life experiences za nchi zote zinazoishi na kilimo hiki zinathibitisha ukweli wa conclusions za wanasayansi wa Umoja wa Mataifa.

Sasa “utafiti” wa huko Makutupora is barely a year old. Halafu wanataka kuja kukudanganya kuwa GMO ndio mkombozi wa tatizo la njaa Tanzania?

Mh Rais hawa vibaraka wa Biotech waliopo Tanzania nimewasikia mara nyingi wakiunganisha matakwa yako ya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na Industrial agriculture. Hivi ni vitu viwili tofauti.

Viwanda vinaweza kundeleza nchi, lakini Industrial or plantation agriculture mara nyingi haileti maendeleo yakinifu katika nchi. Wasikuchanganye hawa. Uwawezeshe wakulima wadogo, chonde.

Wakulima wadogo million 500 duniani ndiyo wanaozalisha asilimia 66 (66%) ya chakula Ulimwenguni. Na Tanzania wakulima wadogo wanazalisha 90% ya chakula nchini.

Huko Marekani (USA) ambako wamekumbatia kilimo cha viwanda (Industrial agriculture) pamoja na wendawazimu wa GMO, watu milioni hamsini, ‘are food insecure now’.

Hawa watu wa TARI huko Makutupora wanawezaje kuliambia Taifa kuwa GMO ndo utakuwa mwarubaini wa kutibu njaa nchini? Kwa nini mwarubaini huu haukutibu njaa Marekani?

Mheshimiwa, hivi sasa, ni wewe peke yako unaweza ku-‘avert disasters’ za GMO hapo nchini.

Mheshimiwa Magufuli, nilikuangalia mubashara wakati unachangia kwenye Kongamano lililofanyika Nkrumah Hall, Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam.

Kwenye mada ya Stiegler’s Gorge ulimtolea mfano Profesa wetu aliyetoa ‘recommendations’ za ‘environmental impact’ za ajabu ajabu kwa sababu alikuwa anatilia maanani maslahi ya “waliomfadhili” na siyo maslahi yetu sisi Watanzania.

Kwenye kilimo cha uhandisi jeni au GMO - Genetically Modified Organism - nasikitika kusema kuwa wengi wa Washauri wako pamoja na hao wanaoitwa “Local Scientists” ni watu ambao wanatumiwa na makampuni ya kigeni ya mbegu na madawa ya kilimo dhidi yetu. Ushauri unaopewa wewe kuhusu kilimo hiki unawanufaisha “Wao” siyo “Sisi”.

*Kwa nini ninasema hivi*.

Kwa sababu madhara ya kilimo cha uhandisi jeni yapo dhahiri kupita maelezo (consipicuosly overwhelming) kiasi kwamba hao washauri au Wataalamu wetu iwapo hawajui basi hawatufai; na kama wafahamu basi ni ushahidi wa kuwa wanatumiwa. Siyo wetu hao.

*•MADHARA YA KISIASA*.•

Haya makampuni yakisha miliki soko la mbegu, kesho na kesho kutwa wakitaka kumpindua Kiongozi fulani hawatatumia majeshi kama walivyofanya Iraq na Libya. Watamnyima mbegu au kumpandishia bei ya mbegu Kiongozi mwenye kulengwa ili awe “unpopular” wananchi wake wenyewe wamtimuwe.

Wakulima wa India walipandishiwa bei ya mbegu kwa asilimia alfu nane (8,000%).
Hapo ziongezwe gharama za madawa yanayoendana na hizo mbegu zao. Hatimaye wakulima waliposhindwa kununua wakawa wanakopeshwa.
Madeni hayo ndiyo yaliyosabisha watu kunyang’anywa mashamba yao na mali zao zingine na haya makampuni.

Matokeo yake: wakulima wadogo 300,000 kujiua katika muhula wa miaka 20.
Nasi tunataka watu wajiue ndio tujiepushe na hii balaa la GMO?

- Burkina Faso kilimo hiki kimepigwa marufuku kuanzia mwaka huu (2018); kilimo kilichozinduliwa kwa vifijo na nderemo mwaka 2003.

- Mexico hiki kilimo na matokeo ya mkataba wa NAFTA - North American Free Trade Agreement umesababisha wakulima wadogo wapatao milioni 2.3 kupoteza mashamba yao.

- Huko Afrika ya Kusini Monsanto walilipa fidia kimyakimya ili kukwepa ‘publicity of a court case’. Na hayo mahindi yanayojaribiwa huko Makutupora, ya WEMA - Water Efficient Maize for Africa - ndiyo hayo yaliyoleta madhara Afrika Kusini. Yalijaribiwa huko kwa muda wa miaka 15. Sasa sisi sijui tunajaribu kitu gani!!

Mh. Rais, mambo ya kuyaongelea kwenye hii mada ni mengi sana. Naona niishie hapa kwa leo.

Mimi ninaishi hapa Uingereza tangu mwaka 1982, lakini bado ni raia wa Tanzania na ni mwanachama hai wa CCM.!

Wasalaamu.
HARID MKALI.
(Author & Journalist).
3rd November, 2018.

Michael Neligwa

Coordinator rural tourism program, June 2015 to date| Former volunteer MNRT Selous Project 2013 -2015| Agro-ecology & social justice enthusiast|