Togolani Mavura
6 min readJan 27, 2021

#SikilizaTogolani

“Usikate Tamaa, hata Waliozaliwa Uingereza nao Hujifunza Kiingereza”.

Mimi na kiingereza tumekuwa na urafiki wa muda mrefu usiopungua miaka 35. Urafiki wetu umekumbana na mitihani mingi na mashaka mengi. Kumekuwepo na kusalitiana, kuumbuana, kunafikiana na hata kuchukiana nyakati zingine. Bahati mbaya kila nilipojaribu kufuta nacho urafiki, nimejikuta mara zote kuwa mimi ndio nakihitaji zaidi kuliko kinavyonihitaji mimi.

Misukosuko ya urafiki wetu bila shaka unatokana na ukweli kuwa tumekutana barabarani. Hatuna udugu wa asili ama wa damu kama mimi na Kiswahili. Kiswahili nimetoka nacho mbali zaidi. Ndio nilianza nacho nilipopata tu utambuzi na ndio natumia nacho muda mwingi zaidi katika maisha yangu ya kila siku.

Kiingereza nimekutana nacho kwa mara ya kwanza nikiwa katika shule ya ‘vidudu’ ya St. Joseph. Kilitambulishwa kwangu na Mwalimu wa ‘Ki-goa’ aliyeitwa ‘Teacher Greater’. Ticha Greta kama ambavyo inapendezea kwa Kiswahili alitufundisha namna ya kujenga urafiki na Kiingereza kwa kujua alfabeti zake, matumizi ya alfabeti hizo, sentensi fupi fupi na nyimbo za kukiimbia hicho Kiingereza. Tatizo nililokuja kuligundua, nikitoka nje ya darasa, hakikutosha kuniwezesha kucheza na rafiki yangu Kiingereza. Hivyo urafiki wetu ulikuwa ni ndani ya darasa la Ticha Greta tu. Yaani, tulikuwa tunaunganishwa na Mwalimu tu.

Nikaanza darasa la kwanza na kupoteana na Kiingereza hadi nilipofika darasa la tatu nikiwa na miaka 10 katika shule ya Msingi ya Forodhani wakati huo. Nikakutana tena na rafiki huyu kupitia Mwalimu Mama Shirima na baadae Mwalimu Mama Nyalika kuanzia darasa la 5 hadi 7. Nikaja kujua kumbe Kiingereza naye alikuwa na marafiki katika Shule ya Msingi Mtakuja wanaitwa Neema na Baraka ambao ni watoto wa Mzee Daudi. Bado tatizo likawa lile lile tu, tunakutana mara moja au mbili tu kwa juma kupitia kwa walimu hao. Ila kidogo maneno ya kuzungumza naye yakaongezeka hata kama si kwa kusema walau tuliweza kuandikiana. Tuliweza hata kuwa na madaftari tunayoandika nyimbo za kiingereza za wanamuziki maarufu wa kipindi hicho (hatukuwa na youtube ya kuangalia nyimbo na lyrics zake kama ilivyo sasa).

Mfarakano mkubwa wa kwanza kati yangu na Kiingereza ulitokana na Baba yangu Mzee Mavura kutuchonganisha. Nilikuwa msomaji mzuri wa magazeti, hususan habari za siasa na michezo, wakati ambapo njia pekee ya kufuatilia msimamo wa ligi na maamuzi ya FAT (TFF ya enzi zetu) na BMT kuhusu rufaa mbalimbali, ilikuwa ni kusoma magazeti ama kusikiliza kipindi cha michezo Radio Tanzania saa mbili kasoro robo usiku.

Siku moja (nikiwa darasa la 5 na umri wa miaka 12), dingi (kama tulivyokuwa tukimuita) alirejea kutoka kazini na magazeti yake, kama kawaida nikanyoosha mkono kuchukua gazeti la Uhuru nisome zangu habari za siasa na michezo. Baba akaninyang’anya lile gazeti na kunipatia gazeti la Daily News ambalo limeandikwa kwa lugha ya rafiki yangu Kiingereza. Kusema ukweli, siku ile niliambulia patupu. Niliweza kutambua maneno machache na viunganishi tu kama ‘the’, ‘and’, ‘of’ na ‘that’. Mara nisikie joto, mara jasho, mara kuwashwa mwili, alimradi tu. Kiingereza akanitia aibu tena mbele ya baba.

Bahati nzuri sikukata tamaa. Nikasema wacha nitafute mbinu nyingine. Nikastuliwa kuwa njia nyingine ya kujenga uhusiano na Kiingereza ni kupitia binamu yake Kamusi (Dictionary) ambaye yeye pia ana ujamaa na ndugu yangu Kiswahili. Nikawa nachukua Daily News na Kamusi yangu pembeni. Mwanzoni ilikuwa ngumu ila baadae nikagundua urafiki wetu kupitia kamusi unaimarika siku hadi siku. Hata hivyo, kiu yangu ilikuwa siku moja niwe na urafiki na Kiingereza wa moja kwa moja bila kupitia kwa mtu kati.

Kupitia kwa Kamusi, idadi ya maneno ya kuzungumza na rafiki yangu Kiingereza ikaongezeka sana. Ikafika wakati sasa tunaweza kuwasiliana vizuri kwa maandishi na tukaelewana. Ila bado akawa ananiweza weza katika maarifa ya sarufi (grammar). Hili ni eneo ambalo bado naendelea kujiimarisha nalo na najifunza kila siku. Nikapata faraja kuwa hata wale marafiki wa kudumu na ndugu wa Kiingereza, hili nalo linawasumbua pia. Nao wanadai ni rahisi kuwa rafiki wa Kiingereza kwa kuzungumza kuliko kuandikiana.

Sitakisahau Kiingereza kwa namna kilivyonifedhehesha siku moja mbele ya binti mrembo ambaye alinivutia sana. Wakati huo nilikuwa nasoma sekondari ya Wavulana ya Azania. Nikajitutumua zangu nikaona nimkoge kwa kumuonyesha kuwa Kiingereza ni rafiki yangu sana. Nikakuta kumbe Kiingereza ni rafiki yake mkubwa kuliko mimi. Si kikanikana mbele yake! Maneno yakagoma kutoka na sauti ikapotea. Nashukuru Mungu ndugu yangu Kiswahili akaja ghafla kunifariji na kunitia moyo. Uzuri Kiswahili hajawahi niacha nadhalilika ama mpweke mahala popote. Nikatia nadhiri nianze kusoma vitabu vya Kiingereza ili nimjue zaidi.

Wakati nikiwa nimeshapata ahueni kubwa kwa upande wa kumsoma na kumuandikia, Kiingereza bado akabaki kunitesa sana katika kuzungumza haswa mbele ya watu. Nikiwa mwenyewe nikimpanga mbona anapangika kirahisi tu. Akitokea tu mtu mwingine au watu wengine ananisaliti. Mateso niliyapata zaidi katika mwezi wa kwanza nilipoanza kidato cha tano katika Shule ya Sekondari ya Shabaan Robert. Pale nikakutana na Walimu wa kutoka India kipindi hicho ambao hawakuwa wakijua Kiswahili. Kwao Kiingereza walifanikiwa kukijua mpaka kukibadilisha na lafudhi.

Katika darasa langu lile, tuliokuwa hatuna mazoea na Kiingereza katika kuongea hatukuzidi 5. Waliobaki wengi walitoka shule ambazo Kiingereza alikuwa mwenyeji. Wengi walishacheza nae na walikua naye. Nikiri kuwa nilipata unyonge sana. Nikawa kimya sana siku za mwanzoni. Baadae nikaona hamna namna lazima nipige moyo konde. Nikajenga urafiki na wenzangu ambao walikuwa karibu zaidi na Kiingereza na pia kuanza kulazimishana nacho urafiki wa mazungumzo. Nikalazimisha mpaka tukaanza kuzoeana.

Kuanzia hapo, kilichobaki ikawa ni kuimarisha mahusiano yetu kwa kuhakikisha tunakuwa na muda mwingi wa pamoja. Nikaongeza usomaji wa vitabu na kupenda kushiriki katika mijadala na uanaharakati kupitia asasi moja ya vijana iitwayo Youth of the United Nations Association of Tanzania (@YUNA_Tanzania). Nikaja kugundua kuwa kadri unavyojitoa ufahamu na kujiamini, na kuwa na ujasiri wa kukubali kuchekwa na kukosolewa, ndipo Kiingereza anakukaribisha karibu na yeye. Nikagundua ndio siri ya wengine pia si kuwa wanamjua sana, ila wanajitahidi kumkumbatia tu na wanaendelea kujifunza kila siku. Sikuona aibu, nikaenda kujiandikisha kusoma Kiingereza cha Kuandika Rasmi (Professional English Writing Skills) pale British Council Dar es Salaam.

Nilipofika elimu ya juu na baadae kuanza kazi tulikuwa tayari tumeshajenga uhusiano mzuri sana. Kule kazini hata hivyo nikaja kugundua kuwa Kiingereza naye ana sura nyingi na anajibadilisha badilisha kutokana na mazingira. Huko kazini ukimuongelesha au kumuandikia kwa lugha ya mtaani (informal), au ile inayotumika kwenye miziki na sinema au katika mazingumzo ya kawaida, anakugeuka kama hakujui. Nikajikuta nalazimika kuendelea kujifunza kumjua katika mazingira tofauti tofauti ili kwenda naye sambamba. Kazi nilizozifanya zikanilazimu nijifunze kuzungumza na kuandikiana Kiingereza kwa lugha ya diplomasia. Nafarijika kuwa nilipofanya mtihani wa kupima urafiki wangu na Kiingereza (IELTS) kama sharti la kukubaliwa kusoma katika Chuo Kikuu nchini Uingereza mwaka 2018, nilifaulu vizuri. Si haba!

Nashukuru kuwa baada ya miaka mingi sana, tumefikia mahali ambapo walau naweza kusema kuwa mimi na Kiingereza tunaishi kwa kuelewana na kuheshimiana kwa kiasi kikubwa. Tunaweza kupitiana na kusindikizana muda wowote na mahala popote. Tumefikia hatua ambayo hata wakati mwingine Kiingereza anaweza kutuingilia katika mazungumzo yetu na ndugu yangu Kiswahili (zamani ilikuwa kinyume chake). Hata hivyo, bado sijafikia uwezo wa kuota kwa lugha yake, kusisimka kwa lugha yake, kusali kwa lugha yake wala kukasirika kwa lugha yake. Bado nikizungumza naye kwa lugha yake muda mrefu nachoka taya na kuna saa najikuta sijisikii (mood) tu kuzungumza nae.

Sina shaka kuwa simulizi yangu si ya kipekee kabisa. Wengi wana simulizi tena za kusisimua sana za uhusiano wao na Kiingereza. Wengine wana simulizi chungu sana. Wako ambao kimewaengua katika usaili (interview), kimewafelisha kwenye mitihani, ama kimewakosesha fursa mbalimbali. Wengine wanakatishwa tamaa tu na kuwaona wengine wanacheza nacho tu wakati wao wanakihitaji zaidi katika mambo ya muhimu na kinawanyanyapaa. Hawa nawatia moyo kuwa inawezekana kabisa kujua rafiki wa kiingereza ukiweka jitihada na ukajitoa aibu. Usikate tamaa, hata waliozaliwa Uingereza nao hujifunza Kiingereza. Ni lugha tu kama lugha ingine yoyote na mtu yoyote anaweza kujifunza.

Nilichojifunza na nachoweza kusema ni kuwa, Kiingereza ni kama mbwa koko, ukimkimbia anakukimbiza, ukimkomalia, anaufyata. Mbaya zaidi katika dunia ya leo na ile ijayo jamaa hakwepeki. Takribani nchi 60 wanamtumia kama lugha yao ya kwanza na watu zaidi ya bilioni 2 duniani wanamtumia. Anatumika sana katika biashara duniani na katika elimu na taaluma mbalimbali. Chaguo pekee tulilo nalo ni kukomaa nae tu na kulazimisha kuzoeana nae. Tatizo lake hapendi unafiki wala urafiki vuguvugu. Ukimkimbia, jiandae na yeye kukukimbia siku na saa utakapomhitaji zaidi. Ukifanya jitihada za kumuweka karibu, naye atakuwa karibu nawe siku za uhitaji wako.