Dar, Mimi & Wewe

Ng'winula Kingamkono
Dar, Mimi Na Wewe
Published in
6 min readMay 24, 2021

Adhuhuri ilianza vyema tukiwa bado tupo sote kitandani, mimi na Sophia. Ilhali tulilala kwa shari baada ya malumbano makali jioni ile ila miili yetu ilitafuta namna ya kusameheana tukaamka tukiwa tumeshikana hasa kama luba akinatana na ngozi.

Tena niliamshwa na vile alivyokuwa akinipapasa maungoni na nikampa busu zito la shavuni. “Umeamkaje?” nikamuuliza, naye pale ajivute kwanza hata asinijibu kisha akanipandia na kuegesha kichwa chake kifuani kwangu na kwa sauti ya chini na ya kudeka akaniambia “bwana sijaamka bado” nikatabasamu huku nikimpapasa mgongoni kwa kupitisha mkono kwenye nguo yake nyepesi ya kulalia.

Ikanijia kumbukumbu ya siku ya kwanza mie na Sophia kuonana.

Mwanzo Wetu

Sophia binti mrembo, mwenye mvuto, ustahimili na uwezo wa kuchambua mambo kwa uyakinifu ambaye ni binti yake na Mzee Abdul. Sasa hayupo tena duniani tangia Sophia akiwa na miaka mitano asikumbuke mengi ya babaye zaidi ya yale ya kuhadithiwa. Tulikuwa kwenye warsha ya vijana na namna ya kujiajiri mwaka 2014 jijini Dar es salaam nikiwa sina mbele wala nyuma baada ya kusota zaidi ya miaka miwili nikitafuta ajira. Nilishakata tamaa ya kupata kazi ya maana basi nikawa dalali wa vitu vya teknolojia mara ipite simu leo nitauza kesho ikwapuliwe ‘kompyuta’ mie nae nimo ilimradi nipate ‘danga chee’ maisha yaendelee pale mtaa wa Samora.

Kwenye warsha nilivutwa na rafiki yangu, Jamila, ambaye yeye kenda masomoni Uchinani akafanya na stashahada kabisa. Akarudi kajaa bashasha na hamasa kedekede akitafuta mahala vijana wanapatiwa fursa na aliposikia hiyo warsha akaniambia “twende ukasikilize bwana huwezi jua kumbe bahati yako ndo iko huku”. Nami nikamsikiliza na kumsikia nikaunga ‘tera’ kwenye warsha sababu tu kulikuwa na vyakula vya bure maana siku hiyo hali ilikuwa tete kweli kweli.

Majira ya saa nne na ushee nikafika pale nikakuta warsha ilikwisha anza basi nikatafuta pahala pa kukaa huku nikipepesa macho hata nisimuone mwenyeji wangu Jamila. Nikakaa nyuma huku washehereshaji wakitamba na hadithi kadha wa kadha za namna mabilionea wa Kimarekani walivyoanza biashara bila ya kuwa na mitaji na leo hii si haba maisha yamewanyookea. Huyo bwana mmoja mwenye kitambi cha kurundika na sauti ya kati akatoa mifano kedekede kwa lugha ya Kiingereza. Basi aliwasifia na kuwatukuza wafanyabiashara wa nchi nyingine kuhusu mafanikio yao. Moyoni nikajionea makelele tu “hao mnaosema hawana mitaji sijui huyo Bill Gates katoka familia ya kitajiri na mama yake alimsaidia kupitia bodi ya wakurugenzi wa kampuni ya IBM iliyompa mwanae tenda iliyomtajirisha”. Mara simu yangu ikatetema kwenye mfuko nami nikaingiza mkono kuitoa na kukuta ujumbe wa Jamila “unasikia mambo hayo? naona umekaa nyuma yangu angalia mstari wa pili katikati” nikainua macho kufata maelekezo na kweli nikamuona Jamila nikatabasamu na kurudisha simu mfukoni. Warsha ikaendelea wazungumzaji wakija na kuondoka pale kwenye jukwaa huku wote wamevalia maridadi mpaka ulipohitimu muda wa kupata maakuli.

Sophia akajigeuza pale kifuani nami nikafumbua macho kisha akainuka akaniweka busu la shavuni na kuelekea msalani huku nyuma nikimuangalia maungo yake vile yakitoa mtetemo kwenye nguo yake laini. Kama vile alikuwa yuko akilini mwangu maana aligeuka kisha akatabasamu “muone nilijua tu unaniangalia” na mimi nikatabasamu na kujigeuza kisha nikarejea kwenye ulimwengu wangu nikijikumbushia tulivyoonana.

Jamila alinijia nilipokaa akiwa amejaa bashasha usoni akafungua mikono ishara ya kutaka kunikumbatia “vipi unaonaje? wako vizuri eh?” nikasimama kupokea mualiko wake na tukakumbatiana “kawaida tu..” nikamjibu “eh kawaida? we nae sijui ukoje em twende tukale mie njaa imenishika” akaongoza nami nikafata nasi tukajikuta kwenye foleni ya kusubiria kupata chakula. Zamu yetu ikafika nami bila hiyana nikapakua pale sahani nikaishibiza tele. Huku viazi, wali mweupe, pale pilau, huku ndizi na nyama za kila aina maana kidume nimefika.

Nikakomelea na shurbati ya maembe iliyochanganywa na tikiti “haya ndiyo maisha sio matajiri sijui nini” nikawaza huku sasa nikimtafuta mwenyeji wangu Jamila yeye keshapakua na kukaa akiwa ananisubiri. “watu wa majuu bwana mna tabu..” nikaanza na zoga pale alipo Jamila “kwa hiyo wewe vikachumbari kachumbari tu..” akacheka bila kunijibu. Nikawa kama niko peke yangu sijali mtu nafukia tu maakuli mdomoni hata nisisikie kitu mara nikatingishwa begani na Jamila “wewe jamani hata hunisikii” nikagutuka “niambie vipi?” Jamila akaguna “mh…yaani una vituko wewe” nikacheka pale hata sielewi vituko gani nimefanya safari hii. Jamila akaniambia “nakutambulisha rafiki yangu hawa ndiyo waandaaji wa hii warsha” basi nami ndio kuinua macho kutazama ninayetambulishwa. Niliganda kwa punde kadhaa bado nikitathmini binti aliyesimama mbele yangu.

Alikuwa amevalia suruali ya kitambaa cha rangi ya ugoro iliyomshika vyema mpaka mchoro wa umbo lake ukaonekana. “Naam” nikajisemea kimoyomoyo huku nikitikisa kichwa na kuendelea kumtizama nikipanda mpaka usoni, nikatabasamu huku nikiwaza “mambo yangu haya”. “Funga mdomo basi” sauti ya Jamila ikanirudisha kwenye uhalisia “maana umemzubalia dada wa watu mpaka naona aibu”. Nikafunga mdomo na kuinuka ghafla ili kumpa mkono nimsalimie. Yule dada akaniambia “kaa tu usijali..” nikadakia “mama alinihasa nisisalimiane na mtu nikiwa nimekaa” wote watatu tukacheka. Nikampa mkono kwa kuubinua “Naitwa Mwendo” nikajitambulisha huku nikimalizia kumeza chakula. “Nafurahi kukufahamu kaka” huku akinigusa ni kiganja chake laini kama upepo. “hapana sio kaka niite tu Mwendo” nikajichekesha naye akanijibu “karibu kwenye warsha yetu” Nikaendelea “asante sana na wewe unaitwa nani mwenzangu?” Jamila akacheka na kuchomekea “kachelewa kuingia huyu hajasikia madini yako”. Bila kuongeza neno akajibu “Sophia”. Jamila nae akainuka “jamani mie narudisha sahani nimeshiba”.

Hata sikumsikia Sophia kama ametoka uani mpaka alivyonipandia na kunilalia mgongoni akagusisha vichwa vyetu. Nikageuza kichwa kumuangalia naye akanibusu na kuniambia kwa sauti ya chini tena kwa kimombo “I am sorry Mwendo” yeye hubadili lugha akitaka kuonesha mahaba. “Sorry ya nini?” nikahoji “si jana jioni tulivyogombana” akanijibu huku akitabasamu. “Ah ya jana yameisha wala usijali kipenzi” nikamwambia huku najaribu kuinuka. “Unataka uende wapi mwenzio nimefika hapa?” nikamwambia kwa sauti ya upole “tukilala sote nani ataandaa ‘breakfast’ sasa?” alivyosikia hivyo tu akainuka haraka hata sikupata shida ya kumuhimiza akawa tayari kaniachia na mimi nikainuka.

Nikapiga mwayo kwa sauti huku nikijinyoosha. Nikatafuta fulana moja kwenye kabati la nguo safi na kujisemea kimoyomoyo “mh itabidi nimpigie simu yule mtu wa usafi aje” basi utafikiri tumeunganishwa akili zetu maana Sophia nae akasema hapo hapo “yule mtu wa usafi sijui atakuja leo acha nimpigie simu sasa hivi”. Sophia nami tulikubaliana kupanga nyumba pamoja kupunguza gharama za maisha na pia ili tusiwe mbali. Tulipata nyumba ya vyumba viwili maeneo ya Sinza yenye jiko na bafu ndani kwa ndani.

Sophia akiwa ameajiriwa shirika linalotoa elimu mbadala kwa vijana wanaoishi kwenye mazingira magumu wakifanyia kazi Mikocheni. Mara nyingi yeye huwa wa kwanza kutoka nyumbani kwa sababu huhitajika kufika kazini mapema. Lakini siku hii tulivu ilikuwa Jumamosi nasi tulikuwa ndiyo kwanza tumeamka. Ugomvi wa jana ulianzia tulipoenda kuruka kwanja na vijana wenzetu maeneo ya Masaki. Yeye akawa amepata ulevi kidogo basi akawa hataki hata turudi nyumbani jinsi ulivyomchukua. Juu ya hapo tulikutana na marafiki zake walisoma pamoja chuo na alikuwa akicheza nao muziki.

Mimi sikufurahia ile namna yao ya uchezaji na ukizingatia hao marafiki sijui nani nani mimi siwafahamu. Nikawa nimeghafirika tu na kugubikwa na wivu usio kifani hata kupelekea kugombana tulivyofika nyumbani.

Nisichokiweza ni kukaa na hasira juu ya Sophia. Basi nikaenda jikoni na kikaptula nilicholalia na ile fulana niliyochukua pale kwenye kabati naandaa maakuli huku nasikiliza muziki kupitia ‘earphones’ zangu.

Nikachukua nyanya, hoho, mayai na vitunguu kutoka kwenye jokofu. Nikaanza kuandaa viungo pale na baada ya kumaliza kukatakata vile vitu nikachukua kikaango na kuwasha jiko la gesi na kukiweka jikoni kichemke. Wakati huo huo nikasogeza mafuta na kuweka kidogo kisha nikavunja yale mayai bila kuyachanganya. Ughaibuni huita ‘sunny-side-up’ sisi tunaita ‘jicho la ng’ombe’ na ndivyo Sophia hupendelea ila yasiwe teketeke. Nilivyoivisha mayai nikapika na vile viungo vingine.

Nikachukua mkate na shurbati ya machungwa kutoka kwenye jokofu, tayari Sophia alikamua machungwa jana yake kabla hatujatoka nami nikamimina kwenye bilauri mbili. Nikajiwazia “hili joto la Dar nani achemshe chai muda huu” Nikapakua lile ‘rosti’ na mayai kwenye sahani moja nikaweka na ile mikate na siagi pembeni. Nikaweka vitu vyote kwenye sinia kubwa pamoja na vijiko na maji ya kunawa na kuelekea chumbani. Nasi tukala.

(Inaendelea kila Jumanne & Alhamisi)

Ungependa kushauri au kuwasiliana? → bofya hapa @KneeNjure

--

--

Ng'winula Kingamkono
Dar, Mimi Na Wewe

a mellow fellow. tech-ish. arts. writer-ish. Works @ellipsisdig