Uthubutu: Kipimo cha Utayari Wetu - 1

Kutoka Arusha Kuja Dar, Kujiandaa na safari. 28th June — 1st July 2020

Justus August
Hatua Zangu | Mapito Yangu
5 min readMay 3, 2024

--

Wakati wa wimbi la kwanza la Covid-19 mwaka 2020 nilibaki nyumbani kwa zaidi ya miezi 3 huku nikifanya kazi kwa njia ya mtandao, sikuwa tena na wateja wa kwenda kuhudumia wala kwenda kuogelea jioni na siku za mwisho wa juma. Muda mwingi nilikuwa nyumbani na familia, tulizoeana, tulifurahiana na kufundishana katika mengi. Zilikuwepo nyakati za kutofautiana na nyakati za kufaana pia.

Photo by Ambitious Studio* - Rick Barrett on Unsplash

Baada ya kukaa nyumbani muda mrefu, mwanzoni mwa mwezi June nilikuwa naongea na Charles Wisize (rafiki yangu wa muda mrefu) na nikamfahamisha namna ambavyo nilijihisi kuchoka kukaa nyumbani. Katika maongezi hayo akaleta pendekezo kwamba tupange safari itakayotuweka nje ya nyumbani lakini itakayotupatia uzoefu mpya katika maisha yetu. Mimi na Charles tunaufanano mwingi na mambo kadhaa yanayotuleta pamoja katika eneo la taaluma, misimamo, shughuli za uzalishaji, vyombo vya usafiri, nk.

Mwezi Januari mwaka 2020, Charles alitangaza kuuza pikipiki yake aina Shineray katika ukurasa wake wa facebook. Nikamtafuta kwenye simu kumuuliza kwanini anauza na kama ina shida yoyote ya kiufundi (maana ninamjua namna ambavyo ni mtunzaji mzuri sana wa vitu). Akaniambia sababu za kuuza na nikamuuliza kama yupo tayari kuniuzia, alikubali. Nilimpatia hela na akaisafirisha kutoka Arusha hadi Dar es Salaam kunikabidhi. Hapa ilikuwa ni mwishoni mwa mwezi wa pili. Baada ya hapo akanunua pikipiki nyingine ya aina sawa na ambayo aliniuzia.

Baada ya kuwa amependekeza tupange safari ya kutuweka nje ya nyumbani, akaja na wazo kuwa tusafiri na pikipiki zetu kwenda Tabora ambako tulikuwa tumenunua vipande vya ardhi mimi, yeye na marafiki wengine. Tukakubaliana kuwa tujipime kama kweli tunao uthubutu wa kulifanya hili. Baada ya kukubaliana mimi na yeye, tukawashirikisha marafiki zetu kuwa tunapanga kwenda Tabora na wakaunga mkono wazo, wasifahamu namna (ya ajabu) ambayo sisi tungeenda. Tukakubaliana kukutana Tabora tarehe 2 July, wapo waliosafiri kwa ndege, wengine kwa magari na sisi tukaamua kujipima pumzi na stamina.

Ili kupata uhakika wa safari na uwezo wa pipipiki ilibidi Charles atoke Arusha aje Dsm na akishafika ataniambia ameionaje safari, na hapo ndipo tutahitimisha maamzi yetu ya kwenda ama kutokwenda na pikipiki. Mimi sikuwahi kuendesha pikipiki umbali mrefu zaidi ya 50km au kwa saa zaidi ya tatu mfulurizo. Saa kumi alfajiri ya Jumapili tarehe 29 June Charles alianza safari kutoka Arusha kuja Dsm. Saa tisa za mchana tulikuwa wote Ukonga (nilikokuwa nikiishi kwa wakati huo)

Juu: Charles baada ya kufika Dsm: Chini: Wakati tunaenda kufanya Kufanya marekebisho kwa ajili ya safari

Sasa tulikuwa na uhakika kwamba safari inawezekana. Jumatatu tulipeleka pikipiki kufanyiwa ukaguzi na marekebisho ili ziwe timamu kwa ajili ya safari. Tulifanya manunuzi na maandalizi ya vitu vyote ambavyo tungehitaji wakati wa safari na baada ya kufika huko (ninao uzoefu wa kufanya camping). Tulikuwa na vyakula, vifaa vya huduma ya kwanza, vifaa vya matengenezo ya pikipiki, mahema ya kujihifadhi, kiberiti, kisu, vifaa vya kupikia, vitu vya kugawa huko tutakapokuwa, hela ya matumizi nk. Baada ya kukamilisha maandalizi tukapanga kulala mapema ili tuanze safari kabla ya saa kumi ili kuepuka vurugu za mabasi ya abiria. Hatukufanikiwa kulala mapema. maongezi yalikuwa mengi.

Saa kumi alfajiri tarehe 1 July tumeshavalia kwa ajili ya safari (suluali ngumu 3, majeketi mawili, gloves na viatu vigumu), Shukuru (mke wangu) na Dada Sarah (binti yetu) wakatukusanya na kutushika mikono tukasali, ile sala ilikuwa na mguso, ilibeba hisia za ndani sana. Kwa namna tulivyoshikana mikono wakati wa kusali nilihisi hofu iliyokuwa akilini mwa kila mmoja wetu. Ile sala naikumbuka hadi sasa ninaposimulia. Baada ya sala tulijitahidi kuwa wachangamfu na wenye matumaini lakini Mke wangu alionekana kuwa na hofu na woga kwamba tunaenda kufanya kitu hatarishi. Tulipanda kwenye pikipiki, tukapiga picha na kufunguliwa geti. Nina uhakika tuliacha fikra mchanganyiko kwa Mke wangu. Tulipita petrol station moja pale maeneo ya Majumbasita tukajaza mafuta na safari ikaanza rasmi kupitia Ubungo na kunyoosha na hiyo barabara ya Morogoro. Mimi nilikuwa mbele huku Charles akinifuata.

Hatukufika mbali, kabla hata ya kufika Kibamba, ajali hii hapa. Barabara ya Mororgoro ilikuwa kwenye upanuzi, uendeshaji ulikuwa mgumu sana, mara unahama upande mmoja, kufika mbele kidogo unalazimika kuhamia upande mwingine. Ili kupunguza usumbufu ilibidi niwe nyuma ya daladala. Kuna sehemu tulifika kulikuwa na kigema kidogo cha kupandisha ili kuhama upande wa barabara; nipo nyuma ya daladala, mwendo haukuwa mkubwa kama 50kph (pikipiki yangu ilikuwa haisomi speed). Gurudumu la mbele lilipanda kile kigema, la nyuma likashindwa ila kwa kuwa mimi ni mrefu, na sikuwa mwendo mkali nilikanyaga chini na kufanikiwa kukipanda huku pikipiki ikiwa kwenye mwendo. Ila sasa Charles alishindwa kukipanda kile kigema.

Pikipiki zetu zilikuwa na taa zenye mwanga mkali, nilishtuka sioni tena taa za pikipiki iliyokuwa nyuma yangu. Nilisimama hapohapo, kugeuka nyuma nikaona taa zikiwaka chini kwenye lami, nikajua tayari. Nilishuka na kukimbia kwenda kumtoa Charles, nilikuta ameshanyanyuka, alisogea pembeni nikayanyua pikipiki, usukani ulipinda, ngao ya kulinda injini na mguu wa mwendeshaji ilipinda pia, Charles suluari zote tatu zilitoboka na kwenye goti la mguu wa kulia ngozi ya goti ikachubuka. Haraka haraka nikaona lile siyo eneo salama, tunaweza kupata ajali nyingine tukiwa tumepata ajali. Nilimwambia Charles aende kuendesha pikipiki yangu mimi niendeshe ya kwake iliyopinda usukani, tulisogea mbele kidogo kiasi cha mita kama 500 tukapaki sasa nikaanza kumuhudumia, kufunga kidonda na kuweka dawa.

Hapa ndiko safari ilianza kuwa ngumu, Nikawaza kumwambia turudi nyumbani ila nikasema ngoja nisubiri aseme yeye, tulishirikiana kuunyoosha usukani ila ngao ilishindikana, baada kama ya dakika 5 nikamsikia akisema ‘twende kazi’. Tukaziwasha tena, nikarudi kwenye chombo yangu naye akapanda yake, tukakubaliana kwenda taratibu hadi kutakapokucha. Tulipita Chalinze saa kumi na mbili kasoro, nikiwa namuwazia Charles yupo na hali gani, ghafla huyo kanipita na yupo nduki, kumeshapambazuka sasa, tunaweza kuona vizuri nami nikaanza kumkimbiza. Kuna eneo pana mteremko wa kawaida na msitu, pale niliona kamnyama fulani kakiingia kwenye gurudumu la pikipiki ya Charles, kichwa kilitengana na kiwiliwili. Kabla ya saa moja tulikuwa Msamvu Morogoro, tukajaza mafuta tena na kusema tuendelee kusogea, chai tutakunywa huko mbele ya safari.

Tulipofika Turiani Tulipata sehemu yenye baa amabko kulionekana wanapika supu, tulenda tukanunua supu, vitafunwa tulikuwa navyo, tulianzisha maongezi ya utani kwa wahudumu, wakatufurahia, tukawafundisha ambavyo tunatengeneza sandwichi tulizotoka nazo nyumbani, wakafurahi sana. baada ya hapo tulikagua jeraha kwenye mguu wa Charles na kugundua dawa niliyomuwekea imefanya kazi. tukaamsha tena.

Sisi hao tunapandisha kwenye kale kamwinuko ka Dumila, Msala mwingine huu hapa… Hapa tulikaa kuanzia saa tatu hadi saa kumi… ilikuwaje…Itaendelea sehemu ya pili.

--

--

Justus August
Hatua Zangu | Mapito Yangu

Psychology Tutor | Behavioral Modification Therapist | Retreat Camp Facilitator | Husband | Father | Friend | Swimmer | Introverted | Youtuber