Nilikataa kwanza, Nikakataliwa Badae: - 1

Sikuwa na msukumo wa ndani wa kuendelea kuwepo

Justus August
Hatua Zangu | Mapito Yangu
4 min readMay 15, 2024

--

Tunapopoteza moja tunapata jingine vivyo hivyo pale tunapopata tunakuwa tumepoteza pia. Zipo nyakati ambazo tunaamini kuwa tumepoteza yaliyo ya maana na umuhimu kwetu. Binafsi najiambiaga kuwa linapoondoka moja yanakuja mengine zaidi kwa ukubwa na thamani. Hii imenisaidia kubaki mwenye tumaini na kiu ya kusonga mbele huku nikifurahia niliyojaliwa kuwa nayo hata kama yamepita.

“Kaka, hivi umeona barua ya kuongeza mkataba?”
Ni swali nilipokea kutoka kwa mtu tuliyeshirikiana kwa ukaribu kwenye eneo la kazi usiku wa tarehe 20 April 2022.
21 April asubuhi tukiwa tunatembea kutoka eneo la maegesho kazini nilimfahamisha kuwa nilipokea email hiyo. Kwa kuwa tulikuwa na ukaribu nilimwambia nilivyojihisi "Kaka, ninasita kusaini hii form ya kuongeza mkataba maana kutoka ndani kabisa sijioni kama ninatosha kuendelea kufanya kazi hapa kwa miaka mingine 2 au 3".

Alinisihi kuijaza hiyo fomu na kwamba tuendelee kuwepo kwenye ajira hiyo wakati tukiimarisha misingi nje ya ajira. Nilimjibu kuwa nitafanya hivyo tukaagana na kuendelea na majukumu ya asubuhi hiyo. Sifahamu aliwaza nini lakini badae aliniletea nakala ya fomu hiyo na kunitaka niisaini na kuirejesha kwa HR.

Nilijaza taarifa husika na pamoja tukaenda kurejesha fomu. Sikuwa na msukumo wa ndani wa kuendelea kuwepo. Nilijaza fomu hiyo kwa kumuheshimu rafiki yangu.

Ijumaa 29 April mchana nikiwa ofisini kwangu na huyo rafiki yangu alikuja mfanyakazi mwenzetu ambaye mimi na yeye tulikuwa idara moja, alionekana kuvurugwa na akatufahamisha kuwa; Ameitwa ofisini kwa HR na kupewa barua ya kwamba hawataendelea nae baada ya mkataba kuisha 31 July 2022. Sikuamini lakini pia sikukataa. Badae nilipotoka nje nikaanza kusikia habari za hapa na pale kuwa watu wanaitwa na kupewa hizo barua.

Ikiwa ni saa tisa dakika 37 zikiwa zimebaki dakika 23 ufike muda wa kuondoka kazini, nilipokea simu kutoka namba mpya na kuambiwa niende ofisini kwa HR.
Nilipofika kuna mtu alikuwa ameingia nikaambiwa nisubirie. Nilishtuka kuona mmoja wa watu tulioelewana sana akiwa ananiangalia kwa hisia fulani. Nikamuuliza kuna amani huku au ni mambo ya ajabu? Akajibu kwa ufupi, ni maumivu tu Kaka yangu.
Nikaelewa kuwa imeisha hiyo.

Niliingia ndani nikakutana na HR msaidizi, akiwa mwenye aibu akaniambia 'Pole kaka, kuna barua yako hapa nimepewa nikupe'. Nikamuuliza imetoka wapi akaniambia kwa CEO. Niliipokea na kuisoma na haikuwa na maelezo ya kwanini zaidi ya kwamba mkataba wangu unaisha July 31 na hakutakuwa na mwendelezo wa mkataba. Nilipomuuliza majibu yake yalikuwa ya kufikirisha... 'Sifahamu nini kimetokea mimi nimeambiwa niwapigie simu na kuwapatia.'

Nilimpa pole yeye na kumwambia kuwa kama hiyo ndiyo namna anavyofanya kazi, basi wakati wake ni mgumu sana kazini kuliko anavyoonekana. Wakati namwambia hiyo akaingia HR mwenyewe, nae akaniambia pole Kaka Justus. Sikuona sababu ya kuendelea kuwepo wala kuendeleza maongezi nikasaini kopi yao na kuchukua yangu na kuondoka.

Nilimpigia simu rafiki yangu nikamwambia tayari imeshakuwa kama ilivyokuwa, hakuamini ila hakukataa pia. Alikuja ofisini kwangu nikampa hiyo barua akaisoma na kutafakari kwa sekunde kadhaa. Kisha akaniambia "pole kaka" na kuongeza "ninafahamu unao uwezo mkubwa wa kulipokea na kulimudu hili, ila ninachojua linaweza kukuyumbisha na pengine baada ya muda litakuumiza akili na hisia. But Kaka please be strong na usipoteze imani."

Tuliagana, ile barua niliiacha ofisini nikaenda kumpokea rafiki yangu mwingine aliyekuwa ametokea Arusha na tukaenda nyumbani. Njiani nilikuwa nikiwaza namna ya kulimudu kwa usahihi bila kutengeneza maumivu kwa wengine.
Kabla ya kusema kwa wanafamilia niliwasiliana na Mshauri wangu mkuu Mr. Kiwali na kumweleza kilichotokea na akanitaka kukutana nae mapema sana kesho yake ili tuweke mmbo sawa. Jioni ile aliniambia kuwa katika matukio kama haya ninatakiwa kujiangalia mimi na familia yangu siyo mimi na kama sehemu ya wengi walioko kwenye huo mkumbo.

Jumamosi asubuhi saa nne tulikutana ofisini kwake, alionekana mwenye tabasamu, hakuniangalia kwa uzuni wala mashaka. Tulisalimiana kwa kukumbatiana huku akinipikapiga mabegani na kuniambia "Karibu kaka".
Ofisini kwake pale tulianza kwa kusali, Mr. Kiwali aliongoza sala, sala hii ilikuwa ya mguso wa hisia na akili, ilijaa maneno ya kuonesha imani na tumaini kuu kutoka kwenye mistari ya biblia. Kipekee ninakumbuka namna alivyoutaja msitari wa 25, 26, 27 na 28 kutoka sura ya 8 kwenye kitabu cha Warumi.
Tulikuwa na maongezi mengi ya kina ambayo yalijikita kwenye kuiangalia kesho kuliko yale yaliyopita.
Mr. Kiwali alinieleza mtazamo wake na akanipa uhakika wa namna alichowaza kilitokana na namna anavyonifahamu.
Tulimaliza kwa kupeana jukumu la kurudi mbele za Mungu na kuongea nae ili atuongoze njia katika ambayo yangefuata (jukumu hili lilikuwa na utaratibu maalumu wa kufuata katika kulitekeleza)

Tofauti na ilivyokuwa kwa wengi wa waliopokea barua za aina ile niliyopokea mimi pale kazini (takribani watu 16 wote wenye asili ya wazawa) Mimi nilipita njia nyingine ya kwenda mbele za Mungu kwa ajili ya kutafuta faraja na utambuzi wa hatua ifuatayo.
Wengi walipania kwenda kuonana na wanasheria na hatimaye kwenda mahakamani, wengine walienda kulalamika kwenye vyombo vya habari, baadhi wakaamua kuanzisha mgomo na hata kuwashawishi wanafunzi kuandamana n.k

Tuliendelea kuwa na vikao vya mara kwa mara na Mr. Kiwali huku tukipeana mrejesho juu ya maendeleo ya sala maalum ambayo tulikubaliana kufanya.
Wakati sala ikiendelea nilipata ujasiri na utayari wa kumfahamisha mke wangu juu ya ukomo wa mkataba wangu kazini (nilimfahamisha hili alfajiri wa siku ya jumanne May 10 2022 na hakushtuka tofauti na nilivyotarajia). Siku iliyofuata aliniuliza kama kuna mpango wa kazi sehemu nyingine nikamjibu kuwa kwa wakati huo hakukuwa na mpango wowote zaidi ya kusali na kutafuta muongozo kutoka kwa Mungu. Niliongeza kwa kusema, Kazi zipo nyingi sitakosa cha kufanya.
Jioni ya siku hiyo aliniambia kuwa sasa tunatakiwa kuweka mpangilio mzuri wa matumizi yaliyohitaji hela kwa kiwango kikubwa ikiwemo ada za watoto, kodi za majengo na leseni za biashara. Haya tuliyapangilia vizuri na kuyakamilisha kabla mkataba haujafikia ukomo.

Itaendelea…

--

--

Justus August
Hatua Zangu | Mapito Yangu

Psychology Tutor | Behavioral Modification Therapist | Retreat Camp Facilitator | Husband | Father | Friend | Swimmer | Introverted | Youtuber