Nilikataa Kwanza; Nikakataliwa Badae: -2

Nilivyoondoka na Maisha nje ya ajira: Kazi zipo nyingi sitakosa cha kufanya…

Justus August
Hatua Zangu | Mapito Yangu
5 min readMay 16, 2024

--

Mwezi May uliisha ikafika June. Mwezi ambao ulijaa vurugu za kila aina kazini pale, migomo ya hapa na pale, vikao vya kila mara, wageni kutoka taasisi mbalimbali za kiusalama na serikali kuu kuchunguza kinachoendelea, uvumi kwamba Justus amehongwa ili asiwe mshiriki wa moja kwa moja kwenye harakati zile na mengine mengi.
Kubwa katika mwezi ule wa June ninakumbuka tulivyoitwa kikao kwa CEO na aliongea kwa tambo za kila aina. Katika kuelezea uhalali wa maamzi ya 'ajabu' aliyofanya akanitaja kama mfano: nilijihisi kukabwa na kuamua kumwambia asileze upuuzi wake kwa kuhusisha jina langu. Alibaini ambavyo ningefichua ambayo asingependa yafahamike kwa wengine. Katika kumalizia kikao hicho niliona ni wakati muafaka wa kumfikishia kilichokuwa akilini kuwa alipata nafasi kubwa ambayo haikuendana na maandalizi ya akili yake.

Baada ya yote yaliyojiri kwa nia ya kuilinda hadhi na ustawi wa afya ya akili ilibidi kufanya mchakato wa kukabidhi na kuondoka rasmi. Hili lilikamilika Jumatano June 15 2022 mchana. Nilikabidhiwa hundi ya mshahara wangu wa mwezi June, July na posho ya utumishi wa muda mrefu (miaka 5). Nilikabidhi funguo za ofisi na kulekea penye maegesho nikiwa na begi langu dogo na kuondoka.

Nilipofika nje ya geti nilijihisi aliyetua mzigo mkubwa ambao ulinielemea kwa kipindi kirefu, nilijiona mwepesi, njiani nilikuwa nikiimba maneno yaliyoko kwenye wimbo fulani "... ni jema aliloanzisha, ni jema alilomaliza..."
Nilienda kanisa kuu la Mt. Joseph mjini. Nilipofika nyumbani nilikuwa na amani. Kesho yake niliwasindikiza watoto wetu shule na maisha yaliendelea.

Mwezi July nilianza maandalizi ya warsha kwa ajili ya walimu na wanafunzi wa shule ya sekondari Msindo iliyoko Namtumbo mkoani Ruvuma.

Nikiwa huko Msindo nilipata wakati mzuri wa kukaa na kuongea na Balozi Salome Sijaona (miongoni mwa watu wachache sana ambao imani yao kubwa juu yangu inanifanya niendelee kujifunza namna ya kuwa bora zaidi katika kuishi na watu).
Nilipata nafasi ya kutembelea maeneo makuu mawili ambayo kwangu yanabeba maana ya pekee sana kwenye maisha ya kiimani nilipanda kwenye Kilele cha Msalaba Mkuu (ipo siri kubwa juu ya eneo hili kwa ufupi ni kwamba parokia hii ipo na vipande halisi vya msalaba alioubeba Yesu Kristu)
Pia nilienda kwenye nyumba ya Watawa wa kike Ruhuwiko ambako kuna watawa wa ndani ambao niliambiwa kuwa jukumu lao kuu ni kusali na kuomba.

Moja ya Vikao vingi ambavyo nimekaa na Mh. Balozi Sijaona

Tarehe moja August nilirejea Dar na kuanza maandalizi ya Hatua Boot Camps ambazo zilipangwa kufanyika maeneo tofauti kwenye kipindi cha likizo ya Sensa. Nilifanya camp 4 ndani ya mwezi wa huo
Madale washiriki 46; Kigamboni washiriki 21; Kiluvya washiriki 87 na Ukonga washiriki 16. Huu ulikuwa mwezi ulionikutanisha na wengi wenye hali tofauti kuanzia kwa wale wasiojua shida hadi wale wasiofahamu kwao wala ndugu zao. Hizi camp zilibeba ujumbe maalum kwangu kuwa bado ninatakiwa kuwa wa manufaa kwa jamii ya wengi.

Kuanzia June 15 hadi September 15 nilipata nafasi ya kukutana na kufanya maongezi na waanzilishi wa taasisi kadhaa na wote walionesha nia ya kutaka tufanye kazi wote. Kote nilipata nafasi ya kuwepo kwa siku kadhaa lakini sikupata msisimko wa kuendelea kuwepo ama kufanya nao kazi. Pia ilikuwepo taasisi nyingine moja ambayo nilifanya usahili na kufikia majadiliano ya malipo hadi wakaniambia siku ambayo wangeniita kusaini mkataba lakini nao hatukuendelea zaidi ya hapo.

SIJUTII KUONDOKA/KUONDOLEWA😄!
Miaka 5 niliyokuwa kwenye taasisi hii inabeba alama isiyofutika katika maisha yangu binafsi, familia yangu, majirani zangu, taaluma yangu na mwenendo wangu. Ilikuwa miaka yenye ukuaji, mafunzo, fursa na nafasi za kuyagusa maisha ya watu huku nikiendelea kuwa bora zaidi. Hapo ilikuwa rahisi kupata ukaribu na viongozi wakubwa wa kitaifa na kimataifa, wafanyabiashara, n.k

Kuondoka kwangu kulikuwa na hisia mchanganyiko ambazo zilichagizwa na namna ya kuondo kwangu! Niliwaona wanafunzi wangu wakinililia huku wakiniomba angalau nibaki mwaka mmoja zaidi, wadau mbalimbali walinitafuta kuhoji kwanini naondoka na wengine wakipendekeza namna ya kufanya ili niendelee kuwepo. Wafanyakazi wenzangu nao wapo walioona haikuwa mmamzi ya hekima kufikia hali ile. Itoshe kusema kuwa ulikuwa ni wakati mgumu sana siyo tu kwa hao niliotaja bali hata kwangu mwenyewe.

Familia yangu, baadhi ya marafiki na washauri wangu walibaki kusimama pamoja nami; kunipa faraja na kunipa matumaini kwamba hatua hiyo ilikuwa ya kuniandaa kwa makubwa zaidi. Baada ya hapo niliendelea na kazi zangu za kuhudumu kisaikolojia kwa makundi na maeneo mbalimbali hadi mwezi Sept. 2022.

Mwanzoni mwa September nilipata fursa ya kwenda kufanya kazi China; ila sikuwa na utayari wa kwenda huko, Sept. 12 nikapata wito wa kazi Dubai, nikaongea na familia wakaniambia wapo tayari kuniruhusu niendelee na taratibu zilizohitajika. 26 September nilianza kazi (online). Tofauti na ilivyokuwa kwenye interview, session yangu ya kwanza (online) ilihudhuriwa na wakubwa wengi wakiwemo viongozi wenye nyadhfa za kimataifa/diplomasia. Niliendelea na online sessions (15hrs per week) hadi Oct. 21 siku ambayo nilisafiri na 24 Oct. nikaanza kazi hapa Dubai.

Mimi ni mmoja wa wale wenye kukubali matokeo bila kulaumu wala kushangaa. Katika kukubali kwangu huwa nipo tayari kuachia na kuachana na ambayo muda wake umepita au yale ambayo mimi sitoshi kwayo au yenyewe hayatoshi kwangu (hii ni hekima inayopatikana kwa gharama kubwa na maumivu makali). Baada ya mimi kuja Dubai, imewafungua watu macho na fikra; nimefuatiwa na wengi kutoka kwenye taasisi hiyo ambao sasa wanaendelea kuzijenga kesho zao katika mataifa mbalimbali. Sijinasbu kwamba nimeshiriki kwenye hatua zao, bali ninafurahia hatua zao.

Hii imekuwa nafasi ya pekee na kubwa zaidi. Nimekuwa kwenye hii taasisi ambayo inanipa kukua zaidi na kunifungulia milango ya kujifunza na kuwafundisha wengi. Uwepo wangu hapa umenipa fursa ya kupata nafasi nyingine ya kufanya kazi na Taasisi tanzu ya Oxford - London.

Endelea kufuatilia ukurasa huu ili upate kusoma mengi ya kimaisha. Ufahamu unaoupata kwenye haya ninayoyaandika unaweza kukufaa wewe au mwingine huko mbele ya safari.

--

--

Justus August
Hatua Zangu | Mapito Yangu

Psychology Tutor | Behavioral Modification Therapist | Retreat Camp Facilitator | Husband | Father | Friend | Swimmer | Introverted | Youtuber