Kuogelea kumebadilisha Maisha Yangu.

Justus August
Hatua Zangu | Mapito Yangu
3 min readApr 24, 2024

--

Niliyeogelea na mwanae, miaka kadhaa badae ndiye alipokea barua yangu ya maombi ya kazi.

Katika maisha haya tunakutana na watu wa kila aina kwenye kila mazingira. Tunakutana na fursa kila tunapokuwa. Zipo ambazo zinatupita kwa kudhani ni ndogo au siyo za kwetu au namna tunavyohusiana na watu. Kila nafasi unayopata inakuandaa kwa jambo jingine.

Wakati ninapeleka barua hiyo sikuwa ninafahamu kama nitakutana na mtu anayenifahamu wala ninayejuana nae. Fuatilia unaweza ukaondoka na linalokutosha.

Nikiwa mwanafunzi (undergraduate UDSM) December nilienda kumtembelea aliyekuwa mwalimu wangu wa Makongo High school, na huyu ni miongoni mwa walimu wengi waliokuwa wakinikubali sana. Baada ya maongezi akapendekeza twende kuogelea, kwa mara ya kwanza naingia kwenye swimming pool, Nilinogewa.
Baada ya hapo nikapanga kila jumamosi na jumapili nitakuwa naenda kuogelea (nilikuwa naenda kuchezea maji), taratibu nikaanza kujenga ukaribu na waogeleaji wa club ya chuo waliokuwa wakifundishwa na Mwana-Olympic Khalid Rushaka. Na kweli walikuwa wanayapiga maji haswa. Baadhi ya waogeleaji wa club nilikuwa nawafahamu kwa majina, kila walipomaliza program yao alikuwa anakuja kunifundisha na mimi angalau kuelea na kupumua (floating and breathing) na mbinu nyingine za kwenye maji. Taratibu nikafahamu zile basics.
Kufikia mwezi February mwakanuliofuata, nikafanikiwa kusajiliwa kwenye club ya chuo kama muogeleaji. Na maisha yakaendelea, nikaongeza muda wa kwenda kwenye mazoezi ikawa ni kila siku kuanzia saa tisa hadi kumi na moja jioni bila kujali kuna lecture au lah, mimi na pool. Ilikuwaje nikajiunga na club, soma hapa chini:

Jumamosi moja baada ya mazoezi Coach wa club aliitisha kikao cha waogeleaji wake, kwa sababu nilishakuwa nao karibu wakaniambia nijoin, coach hakumaind wala nini, pale kwenye kikao yalijadiliwa mengi, nilipopewa nafasi ya kuchangia mjadala niliona hapa ndipo penyewe... Nikaanza kwa kumpongeza Coach pia nikawapongeza waogeleaji na kuwahamasisha kuendelea kumtia moyo coach wao. Nikaongelea faida za kuheshimu muda n.k
Coach akaona huyu siyo wa kuacha akaniambia atanifanyia mpango wa kujoin club ili niswim bila malipo... kikubwa kujituma. Hivyo tu.

Mwaka mmoja badae siku ya jumamosi, alikuja mdada ambaye alikuwa na mtoto wa takribani miaka 2.5 au 3. Yule dada alionekana kufahamiana na baadhi ya waogeleaji wa club, wakati anapiga nao story nikamchukua mtoto yule ili nicheze nae kwenye maji. Mtoto alinikubali sana na kufurahi.
Baada ya kutoka kwenye maji, nilibadilishana namba na mama wa mtoto. Baada ya miezi alinipigia akiniomba amlete mtoto niogelee nae na nikimaliza atamuagiza driver aje kumchukua. Nilifanya hivyo na badae alinitumia Tsh.15,000 kwenye simu. Hatukuwasiliana tena kwa miaka.

Nilimaliza chuo, nikaendelea na mambo mengine, ikiwa ni pamoja na kuogelea, siku zikapita, miaka nayo ikapita. Jumatatu moja muda wa asubuhi nikapeleka barua ya kuomba kazi kwenye taasisi fulani, nilipofika mapokezi nilipokelewa na yuleyule mdada ambaye alinikumbuka kwa jina. Safari ikalainika. Tulisalimiana nikamweleza kilichonileta, maelezo hayakuwa mengi. Alinielewa na kuipokea barua yangu akaniambia amefurahi kukuona nami; tukaagana kwa kusema barua yako imefika na itamfikia mhusika. Nikaondoka kwa tabasamu na matumaini... Matumaini yalizaa matunda mema. Niliendelea kumheshimu na kumuita dada. Hakuwahi kukosa imani na mimi wala kutilia shaka uwezo wangu. Popote alipoona taaluma yangu inaweza kufaa hakusita kunipa majukumu nami niliendelea kutetea imani yake kwangu kwa kutenda sawa na alivyotarajia

Katika maisha haya tunakutana na watu wa kila aina kwenye kila mazingira. Tunakutana na fursa kila tunapokuwa. Zipo fursa ambazo zinatupita kwa kudhani ni ndogo au siyo za kwetu au namna tunavyohusiana na watu. Kila nafasi unayopata inakuandaa kwa jambo jingine. Usidharau.
Mwisho

--

--

Justus August
Hatua Zangu | Mapito Yangu

Psychology Tutor | Behavioral Modification Therapist | Retreat Camp Facilitator | Husband | Father | Friend | Swimmer | Introverted | Youtuber