Uthubutu: Kipimo cha Utayari Wetu - 2

Dumila Morogoro: 1st — 2nd July 2020

Justus August
Hatua Zangu | Mapito Yangu
5 min readMay 5, 2024

--

Safari yetu ilipambwa na muonekano sawa wa pikipiki zetu; kubwa, zenye mchanganyiko wa rangi, nyekundu, nyeusi, bluu na fedha. Pia zilifungiwa maboksi meusi nyuma ambayo yalibeba zana za safari, mingurumo ya kushtua n.k. Mapambo mengine kwenye safari hii ilikuwa ni pamoja na kusimama njiani kwa sababu za kibinadamu au za kiufundi, sababu hizo zilihusisha hizi zifuatazo; pikipiki imeharibika au kuchoka na kuamua kupumzika popote tulipokuwa. Safari nzima, tulifurahi, tulitaniana, tulijifunza masuala kadhaa ya kimaisha na kupanga malengo mengi ambayo kwa kiasi kikubwa tulianza kuyafanyia kazi.

Muonekano wa pikipiki zetu wakati wa safari

Baada ya kuwa tumekunywa supu na kula sandwichi zetu, tulikunywa maji ya kutosha na kuhakiksha tumeweka sawa mifumo ya mawasiliano yetu ya walkie talkies (radio calls). Hatukuwa tumeziweka sawa baada ya ajali ile ya Mbezi. Sasa tukakubaliana safari iendelee na kituo cha kusimama kingine kitakuwa Gairo, vyombo vikawaka na safari ikaendelea. Nilendelea kuwa nyuma ya Charles na sasa tulikuwa tumeanza kupishana na mabasi ya safari ndefu za mikoani na nje ya nchi.

Dumila baada ya pikipiki kuharibika

Baada ya kuipita njia panda Dumila, mbele kulikuwepo na kilima cha kawaida na hapa Charles alikuwa amelipita lori la mizigo lililokuwa linapandisha taratibu, mimi nilichukua tahadhari kwanza nijiridhishe kama kuna usalama. Baada ya kujiridhisha nikaanza kulipita lile lori ghafla nikasikia chombo yangu inaishiwa nguvu, nikabadili gia ili niweke gia namba 3, ikazorota tena, nikashuka mbili hadi moja ila bado chombo ilizidi kukata moto, kwavile nilikuwa kwenye usawa wa lori ilibidi nikatishe barabara niende upande wapili. Hapa chombo ilizima mazima. Nilichungulia mafuta, nikakuta yamo ya kutosha, nikaangalia mfumo wa remote ya kuzima na kuwashia sikuona tatizo, nikachomoa waya wa plagi na kuurudishia, bado hamna kilichofanya kazi.

Kwa vile Charles alikuwa ametangulia, na mchakato huu ulichukua dakika kama 4 alikuwa ameshafika mbali kiasi kwamba mfumo wetu wa mawasiliano ulishindwa kufanya kazi (walkie talkies zinafanya kazi ndani ya umbali wa 3km kwenye maeneo ya wazi). Baada ya muda kama dakika kumi baada ya Charles kushtuka hanioni kwa muda mrefu, alisimama akajaribu kuniita lakini mawasiliano hayakupita ikabidi anipigie simu. Nikamwambia nilikokwamia, aligeuza na kurudi akanikuta niliko. Sasa tukafungua maboksi ya spana nasi tukaanza kujaribu ufundi wetu, ambao hatukujua tunajaribu nini na hatukufanikisha chochote.

Tuliamua kukaa kwanza tupumzike, tulikokuwa ni barabarani, walipita waendesha pikipiki wengine kadhaa hadi walipopita wenyeji wakatuuliza shida nasi tukwambia hatuelewi, walipiga simu kwa mafundi kutoka Dumila wakaja na plagi wakabadili ila pikipiki haikuwaka. Tulikuwa na kamba nzito ambayo tuliibeba kwa ajili ya dharura, sasa ikapata kazi, pikipiki ikavutwa (fundi mmoja anaendesha waliyokuja nayo, mwingine anaongoza iliyozima, na mimi na Charles tukapakizana kwenye pikipiki yake) kwenda hadi gereji. Hii ilikuwa majira ya saa nne. Baada ya kufika huko fundi akasema pikipiki imeunguza valve.

Mtu kalala hapo

Fundi alitwambia angekuwa amekamilisha kuirekebisha ndani ya saa moja, matendenezo ya hapa yalichukua zaidi ya saa tano. Valvu zilitafutwa kwenye maduka kadhaa bila mafanikio, badae wakapata wazo la kununua valvu za pipipiki aina ya GN na zikasagwa kwa muda mrefu ili zitoshe. Baada ya kusubiri matengenezo yakamilike kwa muda mrefu, mwili ulipoa tukaanza kuhisi uchovu, na usingizi. Hatukuwaamini mafundi, tulikuwa tunalala kwa zamu. Ni hapa ambapo tulipata hata nafasi ya kunyoosha usukani na ngao kwa pikipiki ya Charles baada ya ile ajali ya Mbezi. Saa kumi jioni tunaambiwa sasa chombo imetengamaa na tunaweza kuendelea na safari. Hatukupoteza muda, tukajijaradia tena na kuamsha. Tulikubaliana kutoachana kwa umbali ambao hatuonani.

Hapa tulienda vizuri bila kupata shida yoyote, humo njiani tuliwapuuza wengine waliokuwa wanatupita kwa mashindano, tuliipita Gairo bila kusimama, tulifika Kongwa tukasimama na kunywa maji na kuambizana sasa twende hadi Dodoma. Tulikubaliana hatutaingia mjini kati, giza lilitukuta maeneo ya Chamwino, na badae majira ya saa mbili tulikuwa Puma petrol station Nanenane Dodoma. Hapa tulipumzisha vyombo, badae tukasogea maeneo ya St. Gasper tukatafuta malazi na kukubaliana safari ianze saa kumi na moja kamili

Usiku baada ya kufika Dodoma: siku ya kwanza ya safari

Baada ta kuoga, kula na kuingia kitandani, ilikuwa wakati sasa wa kupiga simu na kuwajulisha wanafamilia kuhusu maendeleo ya safari, sikumbuki kama nilikata simu maana usingizi ulikuwa mwingi sana. Alfajiri tukaamka, tukawasha vyombo na kuianza safari sasa ya kuitafuta Bahi, Manyoni, Itigi, Tura hadi Kizengi.

Kilometa chache kufika Bahi nikiwa nyuma ya Charles nilishtuka pikipiki yangu inapiga kelele sana kwenye mnyororo kuashiria kuwa kuna kitu hakikuwa sawa, nilianza kupoteza uelekeo, mbele kulikuwa na basi linakuja, na pembeni kulikuwepo wanafunzi wanatembea na mbele yao kulikuwa na wanawake wakiwa na majembe begani. Kwenye kingo za barabara kulikuwa na korongo hivyo nikaona ni bora niingie kwenye korongo kuliko kugonga watu au kugongwa na gari, niliimudu pikipiki nikashuka nayo nikiwa nimejiandaa kuruka endapo nitaona hatari zaidi. Niliwasikia wale wanawake na wanafunzi wakisema ‘Mungu wangu hiki ni nini…’ nilifanikiwa kwenda hadi sehemu tambalale kwenye vichaka nikasimama. Nilimuita Charles kwenye mawasiliano akaitika na kurudi. Kilichotokea hapa ni kwamba sproketi ndogo ya mbele (inayozungusha mnyororo na gia) ilichomoka.

Tulisaidiana kuitoa pikipiki kwenye hilo Korongo, tukavutana hadi pale Bahi, tukaenda walikouza vifaa vya pikipiki, fundi hakuwepo ila tukanunua hicho kifaa na kutengeneza wenyewe, safari ikaendelea. Tulipofika Manyoni tulikunywa supu tena, tukajaza mafuta na kuendelea hadi Itigi. Barabara ya Itigi kwenda Tabora hakuna changamoto ya wingi wa magari, Barabara imenyooka, unavipita vijiji vidogo sana vyenye majina mazuri na mengine yanachekesha, kuna mapori umbali mrefu.

Katika barabara hii isiyo na changamoto binafsi nilianza kusinzia nikiwa naendesha, kuna wakati niliamshwa baada ya kupitwa na basi la Kisbo. Hii ilikuwa hatari, nikaanza kuimba nyimbo za tenzi za rohoni humo ndani ya helmet. Nilipozidiwa usingizi nikamuomba Charles kuwa sasa tuendeshe kwa kupishana mchezo wa zigzag ili tusisinzie, akaniambia kuwa nae alishasinzia mara kadhaa. Tulifika kijijini Kizengi Uyui Tabora majira ya saa nane mchana, watu wakaanza kushtuka na kutukimbia, badae tulikuja kuambiwa kuwa walisema hawa jamaa wameta chanjo ya korona.

Safari ya kuendesha pikipiki katika barabara isiyo na vitu vya kuichangamsha akili ina changamoto zake. Ukiwa makini sana unasinzia na ukijiachia pia ni hatari. Katika baadhi ya mazingira tulipojihisi kuchoka, tulipaki na kupumzika kidogo, maeneo mengine tulikopaki hakukuwa na watu wala makazi, kuna wakati tulilazimika kusimama maeneo yenye makizi ya watu na tukawa tukianzisha mijadala ya hapa na pale. Ili kuepuka adha ya kupungukiwa au kuishiwa mafuta kila tukikofika na kukutana na eneo linalouza mafuta tulijazia. Pale ilipotulazimu tulisimama na kusimika mahema yetu na kupumzika kidogo.

Moja ya maeneo tulikolazimika kupumzika porini

Baada ya Kufika Kijijini Kizengi-Uyui-Tabora, Tulikaa hapa kwa siku Tano, Yalijiri yapi huko, kwanini watu walikuwa wakitukimbia, Tuliishije, waliokuwja walifikaje, Itaendelea sehemu ya tatu.

--

--

Justus August
Hatua Zangu | Mapito Yangu

Psychology Tutor | Behavioral Modification Therapist | Retreat Camp Facilitator | Husband | Father | Friend | Swimmer | Introverted | Youtuber