Uthubutu: Kipimo cha Utayari Wetu -3

Kizengi, Uyui — Tabora 2nd — 5th July 2020

Justus August
Hatua Zangu | Mapito Yangu
6 min readMay 10, 2024

--

Ilituchukua saa 34 kutoka Ukonga Dar es Salaam hadi Kizengi, Uyui-Tabora (ama twaweza kusema siku mbili). Fatuma aliyeokea Zanzibar alitumia saa takribani 6 kutoka Zanzibar kwa ferry, kuja Dar akapanda ndege hadi Tabora mjini na kusafiri kuja hadi kijijini tuliokuwa. Mwingine aliyetokea Dar kwa basi alitumia saa takribani 16, na mwingine alitokea Dodoma kwa takribani saa 4. Sote tulifika eneo la tukio kwa nyakati tofauti, tulianza safari kwa majira tofauti na pia tulisafiri kwa namna tofauti; kikubwa ni kwamba tulifika.

Kijijini Kizengi kuna nyumba kadhaa za ndugu yangu, kwenye eneo nililonunua limejitenga nje kidogo na makazi ya watu, kuna njia ya kuelekea mashambani na vijiji vingine. Tuliamua kufikia na kukaa kwenye hilo eneo langu kwa sababu linazungukwa na maeneo ya hawa wote tuliokutana hapo, hivyo tuliamua kufikia kwenye eneo letu.

Mimi na Charles tulitangulia kufika, tulifanya usafi wa haraka kwenye eneo husika, tukafunga mahema (camping tents) kwa ajili ya kulala na kukubaliana kuwa ndani ya nyumba watalala wasichana wawili ambao walikuwa sehemu ya mkutaniko huo. Tulikusanya magogo na visiki vya miti kwa ajili ya kukoka moto kuashiria kwamba tupo kambini (huu ni utamaduni wetu (moto unawashwa siku ya kufika na unazimwa siku ya kuondoka).

Maisha ya Kambini yalikuwa hivi

Tulipofika pale kijijini tulielekea uelekeo wenye shule na zahanati, huko ndiko alikuwa akikaa ndugu yangu Datius (wote tulimuita Kaka Dati) ambaye alikuwa akifanya kazi katika mradi wa ujenzi wa barabara ya Itigi-Kigwa, na kijijini pale ndiko palikuwa na kambi ya kandarasi hiyo. Tulienda moja kwa moja nyumbani kwake, hatukumkuta, alikuwa bado kazini, tukageuza hadi eneo la kambi.

Kwa vile watu waliona ‘mapikipiki makubwa’ yenye maboksi nyuma na watu waliovalia kama ‘maninja’ wanaelekea sehemu yenye shule na zahanati wakaanza kusambaza taarifa (ambazo hatujui walizitoa wapi) kwamba sisi ni watu wa kusambaza chanjo ya korona. Kaka Dati alipotoka kazini akaambiwa kuna watu walikuja kwako wanatisha, wameelekea huko kwenye nyumba ya ndugu yako. Kijijini pale mtandao wa mawasiliano uliokuwa unapatikana kwa uhakika ni Halotel, sisi hatukuwa na line za mtandao huo, hivyo hakukuwa na namna ya kutupigia na kutupata (hili ni kosa la kimaandalizi). Kaka Dati aliamua kuja kambini na alifurahi sana kutukuta pale.

Tulendelea kusubiri wengine walikuwa safarini bado wakati huo tukiweka mazingira sawa. Ile kamba ya dharura tuliyoibeba kwenye pikipiki ilitumika kufungia bembea ambazo zilitumika viti kwenye mti wa mkorosho wakati wa vikao na maongezi ya hapa na pale. Kaka Dati alikaa nasi kwa kitambo kidogo kisha akaondoka na mnyama (pikipiki) moja na tukabaki nayo moja, alipoondoka ndipo tulitambua ukubwa wa mlio wa pikipiki zetu hasa ikiendeshwa kwa mbwembwe. Badae tuligundua eneo ambalo mtandao wa tigo ulikuwa ukipatikana chini ya mti hivyo Charles akaweka simu yake hapo na kuwafahamisha waliokuwa safarini kuwa wanaweza kuwasiliana nae. Kila aliyeshuka alienda kupokelewa. Yupo aliyeshuka saa kumi nambili, mwingine saa tatu na mwingine saa tano (huyu wa saa tano, tutakuja kusimulia kilichomtokea kwenye basi alilopanda kutoka Dar).

Usiku tuliolala kwenye mahema tulikoma, baridi ya hali ya juu, umande na upepo. Hema lilikuwa linadondosha matone ya umande, mashuka ya kimasai na namna zingine tulivyojijaradia bado baridi ilipenya. Nilimsikia Charles akihamisha hema kulipeleka karibu na moto nami nikafanya hivyo. Ila hakuna kilichofaa. Tukaamka na kukaa kwenye moto maana kulikuwa na afadhali. Wasichana walilala ndani, sisi tuliteseka nje. Kwenye majira ya saa kumi, wote tulilala na kuamka saa moja, ratiba nyingine zikaanza.

Usiku wakati tukimsubiri msafiri wa mwisho nilikaa kwenye moto na Fatuma tukaongea mambo mengi ambayo hayakuwa na mpangilio maalum ila kubwa ninalokukmbuka ni kuhusu suala la kuwahi au kuchelewa kuoa au kuolewa. Maongezi haya yalikuwa ya kina sana, nilipata nafasi ya kumuuliza yeye anajionaje, wazazi wake wanamchukuliaje na hali ikoje kwa wanawake na wanaume wa umri wake wenye au wasio kwenye ndoa (kwa wakati ule alikuwa hajaolewa na sikuwa nimewahi hata kusikia tetesi za kwamba ana mchumba). Ningekuwa na kibali cha kuandika majibu yake, aisee ningeandika baadhi ambayo ninayakumbuka hadi leo.

Tukijaliwa nafasi nyingine nitakuja kueleza nilikotoka na huyu Fatuma.

Fatuma hakuwa na ruhusa ya kuwa nje ya kazi kwa wakati huo, na alitoa taarifa kuwa hatakuwepo ofisini ila alitakiwa kushiriki vikao kwa njia ya mtandao. Sasa amekuja Kizengi akijikuta mtandao siyo wa kuaminika, kuna wakati tulimsogezea hema pale kwenye mti ambako kulikuwa na mtandao wa tigo ili aweze kushiriki kwenye kikao.

Fatuma akishiriki Kikao: Usiku akaenda bembea

Tulikuwa na mpango wa kuchinja mbuzi asubuhi tutakapoamka, mtu tuliyempa kazi ya kututafutia mbuzi hakufanikiwa hadi mchana hatukuwa tumepata mbuzi. Jioni tukaamua kuelekea vijijini kutafuta mbuzi. Haikuwa kazi rahisi, tulitembelea maboma kama manne tofauti na kote hawakuwa tayari kutuuzia. Badae mwalimu mmoja wa Shule ya Sekondari Kizengi akasema anafahamu sehemu ambako tungeweza kupata, kijiji kingine (mbali zaidi ya dakika 45) Tukawasha vyombo na kuongozana; tulipita porini, hamna njia rasmi zaidi ya zile za kupitishia ng’ombe. Hatimaye tukafika, hapa tulikuta kuna nyumba kama nne na watu wengi kidogo, ilionekana ndiko wanakijiji wanakutana.

Tulisimama, Mwalimu akaingia kwenye moja ya nyumba iliyokuwa na mziki na kelele za watu, hii ilikuwa ni baa. Pale nje zilikuwepo pikipiki mbili aina ya SunLG zinaunguruma, wakati tunamsubiri mwalimu tukawa tunaongea na vijana na wazee waliokuwa pale nje wanasema pikipiki zile zilikuwa kwenye mashindano ya wababe (matajiri) wa pale. Wanasema huwa wanashindana kwamba ambaye pikipiki yake itazima huyo ni maskini hana hela. Dakika 15 akatoka na chupa ya bia, sasa anaongea kingereza na anataka tuingie ndani, tulikataa na kumsihi tujikite kwenye kilichotupeleka. Aliingia ndani akaja na mzee mmoja akasema atatuuzia mbuzi, ila tumpe hela kwanza, tusubirie mifungo warudi kutoka machungani ndipo twende zizini na kuchagua beberu tumtakae.

Wakati tunavuta muda, tulikaa pale nje huku tukiendeleza maongezi, walikuwa ndani wakaanza kukusanyika nje tulipo, mmoja akasema anataka tumuuzie moja ya pikipiki zetu, akasema kama tupo tayari, twende kwenye zizi tuchague ng’ombe watatu na tubadilishane kwa pikipiki. Hakuna biashara iliyoendelea kwenye hili.

Taswira mbalimbali eneo la zizini

Badae tukaenda zizini, tuliowakuta hawaongei kiswahili, mawasiliano ilikuwa ni kisukuma tu, watoto wa miaka 2 wanaswaga ng’ombe, vijana wakubwa walionekana kuwa na kazi maalum ya ulinzi wakiwa na mikuki na sime. Wanawake na wasichana walikuwa na shughuli za kuandaa chakula, kunyonyesha n.k. Tulimchagua mbuzi, kwa vile ilikuwa inaelekea machweo tukubaliana achinjwe na tukaondoka na nyama kwenye maboksi ya pikipiki. Ulikuwa wakati mzuri sana. Tukarudi kambini, tukafanya sherehe ya kuchoma nyama, iliyobaki tukaining’iniza kwenye mti juu ya moto. Siku ikaisha. Siku iliyofuata tukaitembelea ofisi ya serikali ya kata na kijiji, tukafanya vikao na kumaliza. Watu wakaanza kujiandaa kuondoka.

Zoezi la kuchinja ili tuondoke na nyama.

Mimi na Charles tulibaki. kwa siku mbili zaidi, tuliweka alama za mipaka katika maeneo yetu na kuendelea kushirikiana na jamii ya pale. Tarehe 6 July 2020 tukaanza safari ya kurejea kutoka Tabora, kuja Dodoma ambako tungeachana, mimi nirudi Dar na Charles aelekee Arusha.

Ilikuwaje, safari ya kurudi? Yalitukuta yapi? Tutarudia tena? Tumejifunza nini? Itaendelea sehemu ya 4.

Matukio mbalimbali katika picha

--

--

Justus August
Hatua Zangu | Mapito Yangu

Psychology Tutor | Behavioral Modification Therapist | Retreat Camp Facilitator | Husband | Father | Friend | Swimmer | Introverted | Youtuber