Uthubutu; Kipimo cha Utayari wetu - 4

Dodoma; Kutengana hapa Charles kurudi Arusha na mimi kurudi Dar 6th -7th July 2020

Justus August
Hatua Zangu | Mapito Yangu
4 min readMay 11, 2024

--

Baada ya wote tuliokuwa nao kuwa wameondoka, tulibaki Mimi na Charles, Kaka Dati aliendelea na majukumu yake. Tulibaki pale Kizengi, hapakuwa tena na uchangamfu kama uliokuwepo kipindi tukiwa wote 6. Usiku wa tarehe 5 mwezi Julai tulienda pale ilipokuwa kambi yetu tukauzima moto, tukafunga mahema yetu, tukashusha bembea na kuingiza kila kitu ndani ya nyumba, tukakusanya zana zetu za safari na kwenda kulala kwa Kaka Dati. Kitendo cha kuzima moto kiliashiria kuvunjika rasmi kwa kambi yetu.

Jumatatu tarehe 6 Julai, saa kumi na moja na nusu alfajiri tuliamka na kuanza maandalizi ya kuanza safari ya kuondoka Kizengi kuelekea Dodoma. Kiwewe cha safari ndefu kilirejea tena, sikutamani tena kuendesha umbali mrefu lakini sikumwambia Charles. Tulishikana mikono Kaka Dati, Charles na Mimi tukamshukuru Mungu kwa yote yaliyofanyika, tukaibariki safari, tukapiga picha na mnamo saa kumi na mbili na dakika 20 tukaanza safari. Tuliondoka wanyonge, tuliwapita watu wakienda mashambani, wanafunzi wakienda shuleni na wengine wakiwa wanaelekea walikokujua wao.

Majira ya saa tatu na nusu tulifika Manyoni, tukapiga picha kwenye vibao vya barabarani, tukafika sehemu na kuagiza supu, tukanywa na kujiambia kuwa sasa tuamshe hadi Dodoma. Hapa Manyoni nakumbuka tulizunguka sana kuna kitu tulikuwa tunatafu, sikumbuki ni kitu gani, kama sikosei tulikuwa tunamtafuta fundi wa kurekebisha king’ora cha pikipiki ya Charles. Safari ilikuwa nzuri, haikuwa na changamoto yoyote; tuliipita Bahi, tukafika Nala na hatimaye tukaingia Dodoma mjini majira ya saa saa sita na nusu mchana.

Hatukuwa tumefahamu kwamba wakati huo kulikuwepo na mkutano mkuu wa CCM wa kuchagua mfombea Urais Zanzibar. Tulipofika maeneo ya Bahi Road tulianza kutafuta sehemu ya kupumzika, nyumba nyingi za wageni tulizotarajia kufikia zilikuwa zimechukuliwa na washiriki wa mkutano mkuu wa CCM. Tulizunguka sana bila mafanikio, hadi wakati tulipofika sehemu moja, muhudumu akatuuliza mnataka kukaa siku ngapi tukasema moja, akasema basi atatupa vyumba ambavyo vilikuwa vinasubiri wageni wa kufika siku ambayo inafuata. Kama tungekosa sehemu ya kulala, binafsi nilishafikiria kuendelea na safari ili nipunguze urefu wa safari ya Dodoma kuelekea Dar.

Pale hotelini tulipumzika mchana ule kila mmoja chumbani kwake, tuliamshana majira ya saa kumi na moja ambapo tulitoka kwenda kutafuta sehemu wanakochoma nyama, tulikula tukarudi na kulala mapema ili kuuandaa mwili kwa kumalizia safari. Tuliamka majira ya saa kumi na mbili, hatukuwa na haraka sana, tukapata kifungua kinywa, tukajiandaa, tukawasha vyombo, tukasimama nje, tukashikana mikono (mara hii ni mimi na Charles tukamshukuru Mungu na kuibariki safari. Hapa ndiko tulikotengana. Tuliagana katika eneo hili.

Huu ulikuwa ni wakati mgumu sana kwangu na kwa Charles. Kuagana kulikuwa kugumu, kila mmoja anatengana na mwenzie, sasa ninaenda kuendesha zaidi ya 450km peke yangu sina wa kusimama na kutaniana nae, sitakuwa na mtu wa kushindana nae wala wa kumtanguliza pale nitakapojihisi kuchoka.

Nilikuwa wa kwanza kupanda chombo, nikiwa nimevalia kofia ngumu na gloves tulishikana mikono na kuambiana maneno ambayo badaye tulikuja kuelezana tulijisikiaje wakati wa kuagana. Ndani ya kofia ile, nilitokwa machozi, rafiki yangu nae anasema alipata hisia za uchungu kuona ninaondoka na alisikilizia mlio wa pikipiki hadi ukapotelea mbali, ndipo akabaini kuwa kuna matone ya machozi yalimtoka.

Nilisafiri vizuri sana bila na shida hadi Morogoro nilisimama kwa muda kupisha msafara wa kiongozi uliokuwa ukielekea Dodoma kutokea Dar, nilitumia nafasi hii kuipeleka pikipiki kwa fundi aikague kama iko sawa ili nipate uhakika wa kuikamilisha safari. Baada ya kutoka Morogoro nilisimama njiani nikanunua matunda na majira ya saa tisa na nusu nilikuwa nipo nyumbani, nilipokelewa na binti yangu Jeanne ambaye ndo alikuwa anajifunza kuongea, alifurahi sana na alinishangaa pia. Mke wangu alirudi alinikaribisha nyumbani alifurahi nimerudi.

Niliwasiliana na Charles nikiwa Morogoro alinifahamisha amebakiwa na kama 100km afike nyumbani kwake Usariva Arusha, nami nilikuwa nimebakiwa na kama 180km. Baada ya kufika nyumbani nilimpigia simu Charles akanifahamisha kuwa amefika. Tulifurahi na kumshukuru Mungu pamoja. Tuliwaadithia wanafamilia yaliyojiri safarini, yapo yaliyowafurahisha, yaliyowashangaza, yaliyowaumiza na yaliyowapa wasiwasi. Nilipoenda kupima uzito nilikuta nimepungua karibu kilo tatu.

Hongera! Kama wewe ni mmoja wa waliosoma haya masimulizi kuanzia sehemu ya kwanza hadi hii sehemu ya nne. Sina uhakika kama umepata la kujifunza au la kukusisimua. Nia ya kuandika masimulizi haya ilikuwa ni kuweka kumbukumbu ya yale ambayo nimewahi kufanya na zaidi yakiwa ni yenye kuogofya au kutia wasiwasi kwa wale wanaonitakia mema. Katika masimulizi haya kuna kipimo cha kuaminiana na kukubaliana na kuyaishi makubaliano. Utakuwa umeweza kuona namna urafiki ulivyo na nguvu katika kushawishiana.

Tunao uthubutu, tunao utayari, tunao msukumo wa kufanya makubwa, tunachohitaji ni nafasi. Hatuna woga unaoweza kutukwamisha kufanya yaliyo makubwa, ya pekee na wakati mwingine ya ajabu. Gharama tulizotumia kwenye safari hii (kwa upande wa pesa) ni mara tatu zaidi ya tungetumia usafiri wa umma, Kuna gharama ya hisia, fikra, muda, kuaminika, kutumainiwa, kueleweka, nk.

Ushirikiano wetu upo kwenye mengi, siyo kwenye hili tu, tunakutanishwa na mengi na ama hakika Justus R. August na Charles F. Wisize wanayo mengi ya kusimulia.

Kipekee kabisa ninarudisha fadhira kwa Mwenyezi Mungu aliyeturuzuku uhai, uzima na usalama, maarifa na utashi. Pili ninamshukuru Mke wangu Shukuru J August kwa kunivumilia, kuniombea, kunitakia mema na kunipimia kiasi kinitoshacho. Uzao wa familia ya August, Mama yangu na ndugu zangu kwa upendo wenu mkubwa. Mke wa rafiki yangu Charles (Loveness) na uzao wenu, washiriki wote katika safari hii ambao wametajwa na wale ambao sijawataja. Iendelee kuwa heri katika yale mnayokimbizana nayo na tukutane tena katika mengine yenye picha kubwa na utukufu zaidi.

Justus August

--

--

Justus August
Hatua Zangu | Mapito Yangu

Psychology Tutor | Behavioral Modification Therapist | Retreat Camp Facilitator | Husband | Father | Friend | Swimmer | Introverted | Youtuber