Kuomba Msamaha Wa Kweli

Sandrahope Msigwa
Love Shack
Published in
4 min readAug 20, 2023

Ni zaidi ya kusema “Samahani”

Tunavyokuwa kiumri tunafundishwa kuomba msamaha tunapowaumiza ndugu, jamaa na marafiki, huwa tuna ambiwa tuseme “Samahani” na maisha yanaendelea lakini tukiwa wakubwa hiyo haitoshi. Neno “Samahani” haitatui unyanyasaji, usaliti, wizi au makosa tunayoyafanya.

Kuomba msamaha ni zaidi ya kusema “Samahani”

Msamaha una lugha tofauti na kama lugha nyingine kuongea na kuelewana ni tofauti. Ni kama Kiswahili na Kifaransa haijalishi uongeze sauti kiasi gani mswahili hawezi kuelewa kifaransa na mfaransa hawezi kuelewa kiswahili bila kujifunza.

Tunapo omba msamaha kwa lugha anayoelewa mtu tuliye mkwaza, watapokea na kuona msamaha tulio omba ni wa kweli na tuta samehewa kirahisi.

Lugha 5 Za Msamaha

1.Kuonyesha Majuto; kwenye lugha hii ya msamaha unaeleza unaomba msamaha kwa ajili ya nini kwasababu mtu anaelewa hii lugha ya msamaha zaidi anahitaji kujua kama unaelewa kwa kiasi gani kosa lako limemu umiza. Mfano: “Samahani kwa kuchelewa kurudi nyumbani, najua nilitakiwa kuwahi ili kukusaidia na watoto na ninafahamu nimekuangusha sana.”

2. Kukubali wajibu; kwenye lugha hii ya msamaha unakiri kuwa ulikosea, uliemkosea anahitaji wewe kukubali wajibu wa ulichokifanya.

Mfano: “Kutokuwa na mipaka na mfanyakazi mwenzangu ni kosa, Najua tuliongelea kuhusu kujenga mipaka na sikutakiwa kuachilia ifike mbali kote huku. Nakubali wajibu kwa nilichokifanya na naelewa nimekosea”.

3. Kufanya marekebisho; hii lugha ya msamaha inahusu kuweka mambo sawa. Kwenye lugha hii ya msamaha unaweza kuunganisha na lugha yao ya upendo (matendo ya huduma, zawadi, mguso wa mwili, maneno ya uthibitisho na muda bora).

Mfano: Kama ulisahau siku ya kumbukumbu ya ndoa yenu ili kuomba msamaha unaweza kusema “Najua nimezingua na siwezi kutengua nilichokifanya lakini naomba unipe nafasi kuliweka hili sawa” kisha — mpele katika mgahawa aupendao kwa ajili ya chakula cha usiku(muda bora), mpelekee maua au kitu chochote akipendacho (zawadi), panga mambo vizuri kwa ajili ya muda wenu kitandani (mguso wa mwili), pika chakula kizuri / saidia kazi za nyumbani (matendo ya huduma), nunua kadi/ andika meseji ndefu ikielezea upendo wako kwake (maneno ya uthibitisho).

4. Panga Mabadiliko; kwa mtu mwenye hii lugha unahitajika kutoa mpango wa jinsi utakavyo fanya ili kosa lisijirudie tena. Mfano: “Nahitaji kuacha tabia yangu ya kusahau mahitaji ya nyumbani, sipendi hii tabia yangu na ili kuacha hii tabia nitaanza kuandika vitu vya kununua ili hii tabia isijirudie tena.”

5. Kuomba msamaha; kwa watu wenye hii lugha ya msamaha wanafurahi wakisikia maneno “Naomba Unisamehe”. Kwa hawa watu ukiwapa ombi la msamaha basi wana imani umeomba msamaha wa kweli.

Unaomba msamaha kwa kuwa unathamini mahusiano na unatakiwa kujua kuwa haijalishi kama umekusudia au haujakusudia kumuumiza mtu inabidi kuomba msamaha wa kweli kwasababu itapelekea mahusiano kusonga mbele.

Tusipo omba msamaha katika lugha sahihi, tuliemkwaza anaweza kufikiria kuwa hatujaomba msamaha wa kweli na hii inaleta matatizo zaidi kwenye mahusiano.

Kabla hatujajua lugha za msamaha, mume wangu alikuwa akiomba msamaha kwa kusema “Samahani” na kwangu mimi sikuona kama ni wa kweli kwasababu alikuwa hajaomba msamaha lwa lugha ninayo elewa mimi na kibaya zaidi sikuwasiliana nae ambacho kilifanya mambo yawe mabaya zaidi, siku au wiki chache zikipita najikuta nalipuka kwa kuweka vitu moyoni na yeye atasema “lakini nilisema samahani” na mwishoni nitasamehe ila nakuwa siamini kuwa aliomba msamaha wa kweli.

Baada ya kujua lugha za msamaha sasa najua kuwa alikuwa anaomba msamaha wa kweli atakama haikuwa kwa lugha ninayoelewa mimi. Sasa kwa kuwa wote tunaelewa lugha za msamaha wa kila mmoja wetu basi ndoa yetu imekuwa rahisi zaidi kwa kuwa tunaomba msamaha vizuri ambacho kinapelekea kusaameheana mapema zaidi.

Jinsi ya kujua lugha yako ya msamaha: 1. Chunguza jinsi unavyo omba msamaha kwasababu mara nyingi hiyo inakuwa ndo lugha unayotamani kupata. 2. Andika malalamiko na maombi yako mtu akikukosea kwasababuu hapo ndipo hitaji lako lilipo. 3. Jaribu kuchukua jaribio kwenye tovuti hii, Jua Lugha yako ya Msamaha Hapa

Kusamehe

Kusamehe ndo jibu pekee zuri baada ya mtu kuomba msamaha. Mara nyingi tuki kosewa na kuumizwa tunakosea kwa kufikiri kuwa tukiwa tumesamehe kweli ndipo maumivu yanaisha papo hapo. Lakini “Kusamehe sio hisia ila ni maaumizi”.

Kusamehe ni maamuzi ya kutoa fadhila badala ya kudai haki. Ni kusamehe tu ndo kutapeleka kukua kwa mahusiano. Kukosekana kwa kusamehe kunapeleka kifo cha mahusiano.

Pamoja na Hayo Kusamehe hakufanyi haya:

Kusamehe hakufuti kosa; na ata ile kumbukumbu ikija haimaanishi haujasamehe ila tu wewe ni binadamu ambae anakumbuka tukio la kuumiza lakini hii haimaanishi ndo uzidi kulifikiria kwasababu ukifanya hivyo ni kama unarudi eneo la tukio na inaleta tena maumivu na inaweza kukusahaulisha kama aliekukosea aliomba msamaha.

Kusamehe hakurudi imani; kwasababu kusamehe ni maamuzi ila imani ni hisia, imani ni kuamini kuwa utafanya ulisemalo bila kusita. Imani unapata kwa matendo yako ya kuthibitisha unastahili mtu akuwekee hiyo imani.

Kusamehe hakufuti matokeo ya kosa; mfano kama kulikuwa kuna kuchepuka kwenye ndoa na mtoto alizaliwa, kusamehe hakumfuti huyo mtoto au gonjwa la zinaa au matokeo yoyote ya kuumiza moyo yaliyotokana na maneno ya kuumiza. Matokeo huwa yanachukua muda kidogo kurudisha mahusiano yalivyokiwa zamanai kwahiyo aliekosea na aliekosewa wanahitaji kuwa na uvumilivu.

Fikiria dunia yetu ingekuwaje kama kila mtu angejifunza kuomba msamaha wa kweli na kila mtu angejifunza kusamehe.

Kwa Upendo,

Sandrahope M.

Rejea

The 5 Apology Languages by Gary Chapman and Jennifer Thomas

--

--