Kuwapenda Kwa Mbali

Sandrahope Msigwa
Love Shack
Published in
3 min readApr 16, 2024

Sio ubinafsi au roho mbaya ni moja ya njia ya kujipenda na kujiheshimu.

Tunawakata watu kwenye maisha yetu na kuwapenda kwa umbali kwasababu kuwachukia kama walitukosea haitasaidia haswa kama ni watu ambao hatuwezi kuwaepuka kama ndugu. Naamini kuwa chuki inahusiana na kutokusamehe au kuweka vinyongo kitu ambacho ni kama kunywa sumu na kutegemea imuue mwingine, ndio maana ni bora kuwasamehe, kuwapenda kwa umbali huku tukikata ukaribu nao.

Kuna video kwenye mtandao wa tiktok ambayo dada anauliza “nichukue kiasi gani cha kutokuheshimiwa hadi kumkata mtu kwenye maisha yangu?” na Baba mmoja akajibu “Utakunywa sumu kiasi gani hadi ikuue?”

“Ni sawa kuwakata ndugu wenye sumu katika maisha yako kwasababu damu inaweza kuwa nzito kuliko maji lakini damu sio nzito kuliko amani ya akili” — Radhika Bose

Kuna sababu tofauti zinazopelekea watu kukata mawasiliano na ndugu au jamaa kwenye maisha kama; usaliti, kuendeshwa, kupotoshwa, umbali, ukuaji, kujiweka upaumbele, kujilinda na unyanyasaji. Na hii huleta faida kama afya bora ya akili, kujiheshimu, kujipenda, uponyaji, amani ya moyo, kupata mahusiano bora.

Huwezi kudhibiti upepo ila unaweza kudhibiti matanga. Hii ina maanisha maisha sio kinachokutokea ila ni jinsi unavyolipokea na kuchukulia hatua linalokutokea. Mfano huwezi kudhibiti ambacho watu wanakuongelea, wanachokuambia lakini unaweza kudhibiti jinsi unavyolichukulia.

Nyoka anapokung’ata, hurudi kumuelezea kwanini hakutakiwa kukung’ata au ambavyo haukustahili kutendewa hivyo, unaenda hospitalini kushughulikia kupona kwako.

Kupona kwako kunaweza kuchukua muda mrefu kwasababu kukata watu kwenye maisha yako sio rahisi na inaumiza kwasababu kumuacha mtu uliempenda na kumjali sio rahisi.

“Kumuachilia mtu aende haimaanishi haumpendi au haumjali, ni kutambua kuwa mtu pekee unaeweza kudhibiti ni wewe mwenyewe.” — Deborah Reber

Jinsi Ya Kumpenda Mtu Kwa Umbali

  1. Sali juu ya iyo hali, na yeye pia; Muombe Mungu abadilishe mtazamo wako kwa kinachokukera kuhusu hao watu. Muombe Mungu akusaidie kuwapenda jinsi Yeye anavyowapenda, na kuwaelewa.
  2. Kaa Mbali; unaweza kumpenda mtu na kutotaka kuwa na urafiki wa karibu nae ambayo ni sawa pia, wasalimie vizuri ukiwaona, sio lazima mpige stori haswa kama unajua maneno yao yanaweza kukusononesha , kukumiza au kukushusha chini.
  3. Weka Mipaka; mipaka ni mwongozo wa jinsi wengine wanavyotakiwa kukutedea na kuwaonyesha ambacho ni sawa kwako na kisichosawa kwako.
  4. Jiweke Bize; kwasababu kupona kwako kutakuwa kugumu na unaweza ukajikuta unawamiss kwahiyo jiweke bize ili kuepuka kurudi kwa wanaokuumiza au kukunyanyasa. Hata wanaporudi jitahidi kutokuingia mtegoni. Ikifika mbali, wanapitiliza mipaka au hawaelewi umbali wako na wanakusumbua kwenye simu wablock tu.

“Mtu akikuonyesha jinsi alivyo, muamini mara ya kwanza”. — Maya Angelou

5. Usiwaseme Vibaya; kuwa mtu wa hali ya juu, usiwaongelee vibaya hatakama walikukosea na pia jua kuwa kuna nafasi kubwa ya wao kukuongelea wewe vibaya, na kukufanya uonekane mbaya au watakusema zaidi kuwa umebadilika lakini wewe potezea kwakuwa unajua ukweli wako.

Watu wengi wanaokatwa wanatabia ya kujifanya wanyonge na kukufanya ujiskie vibaya kwa maamuzi uliyofanya ila usiwaruhusu wakufanye ujihisi we ndo mbaya.

Kama unajua kabisa wewe sio mtu mbaya au mwenye roho mbaya ya kuumiza mtu kwa maksudi, Usiache kujisimamia, haki yako ya kuheshimiwa na kuweka mipaka yako.

Kuwakata watu haimaanishi huwapendi, inamaanisha unajiheshimu. SIO KILA MTU NI WA KUKAA MAISHANI MWAKO!

Kwa Upendo,

Sandrahope M.

--

--