Mahusiano Mengi Yana Maadhimisho Lakini Machache Hukua Kweli

Sandrahope Msigwa
Love Shack
Published in
5 min readDec 7, 2023

Yako ni Mahusiano Mengi au Mahusiano Machache?

Ukuaji wa mahusiano unaanza na fikra, fikra dumavu au fikra za kukua. Fikra dumavu ni fikra za kuamini hali haiwezi kubadilika huku fikra za ukuaji ni fikra za kuamini hali inaweza kuimarika kwa jitihada.
“Huwa tunapotezea ukuaji kwasababu tunaona toka tunazaliwa miili yetu inakuwa pamoja na umri wetu na tunahisi tunakuwa ila ukuaji wa kweli unafanyika kwenye fikra” — Jocelyne Msigwa

Hivyohivyo na kwenye mahusiano pia, sio kwasababu tunasherekea maadhimisho ya miaka ya mahusiano/ndoa basi mahusiano yetu yanakua, Tunahitaji kuwa wanafunzi wa maisha ili tuweze kukua.

Iwe mmeanza mahusiano hivi karibuni au mmeoana kwa miaka 30, Kukua ni lazima ilii kuwa na mahusiano bora.

Kama wachumba hawakui pamoja, basi watakua mbali mbali. (Wanandoa Pia)

“Mapenzi na Mahusiano ni vitu vizito hivyobasi kila mtu anahitaji kuendelea kujifunza na kukua” — Castory Mrisho.

Ukuaji wa Mahusiano

Ukuaji wa mahusiano sio maadhimisho lakini ingekuwa vyema kama tukiadhimisha miaka mingi huku tukikuwa kimahusiano. Takwimu zinaonesha kuwa mahusiano ya kawaida yana urefu wa miaka 2 na miezi 9 huku ndoa zikiwa na urefu wa miaka 8. Tunaweza kufanya mahusiano au ndoa zetu zidumu zaidi? Labda tukijifunza kitu kuhusu ukuaji kutoka kwa ndege aina ya tai.

Tai ana uwezo wa kuishi miaka 70 na ili kufikisha miaka hiyo inabidi anapofikisha miaka 40 afanye mabadiliko au atakufa. Ndege hawa wanapofikisha miaka 40 kucha zao haziwezi kukwapua mawindo (chakula chao), mdomo wao unakuwa mrefu na unainama, na manyoya yanaganda kwenye kifua kitu ambacho kinafanya iwe vigumu kupaa. Haya yakitokea tai anabaki na chaguo mbili aidha afanye mabadiliko au afe.

Mchakato wa mabadiliko haya ni wenye maumivu na mrefu. Katika kipindi hiki tai anarudi juu ya milima katika kiota chake, anajipiga mdomo wake kwenye mwamba mpaka unapotoka kisha anasubiria uote mwingine, baada ya hapo anatumia mdomo huo kung’oa kucha zake kisha kucha mpya zikikuwa tena anatumia kucha hizo kunyofoa manyoya ya zamani. Baada ya mchakato huu anakuwa kama amezaliwa tena.

Kuiweka kiurahisi Tai anakuwa, anaachisha ukuwaji kisha anakuwa tena. Sisi binadamu tunaweza kujifunza, kufuta tulichojifunza na kujifunza tena. Mahusiano ni kama maisha ambapo ina bidi kujifunza, kufuta tulichojifunza na kujifunza tena kila baada ya muda kwasababu mahusiano pia yanahitaji ukarabati wa hali ya juu.

Tunakuwa Tunapojifunza.

KUJIFUNZA; jifunze kuhusu mwenza wako, jifunze njia mpya za kuongeza spaki kwenye mahusiano yako, jifunze njia za meneji hisia zako, jifunze njia za kuonyesha unampenda mwenza wako, jifunze za kuishi kwa tabia nzuri, jifunze njia tofauti ya kuomba msamaha, jifunze njia tofauti za kukabiliana na migogoro, jifunze njia mpya ya kujenga mahusiano bora.

Kuna sehemu nyingi unaweza kujifuza kuhusu yote hayo na zaidi kuhusu mahusiano. Unaweza kujifunza kwa kuwasaliana na mwenza wako, unaweza kujifunza kutoka kwenye vitabu, semina, mahusiano mengine yenye kipaumbele cha Mungu, hivi sasa tunaishi katika wakati wa data iayopatikana mikononi mwetu (intaneti/mtandao) rasilimali hii sio ya kutumia vibaya kwasababu pamoja na kwamba inaweza kujenga lakini inaweza kubomoa pia, kwahiyo kuwa mwangalifu na chanzo chako cha mtandao. Sehemu ambayo tunaweza kujifunza kuhusu kukuza na kujenga mahusiano bora ni kwa Muumbaji wa mahusiano na dunia ambae ni Mungu kupitia Neno lake.

“Ni Ujinga kujaribu kuendesha ndoa bila kusoma mwongozo wake , Biblia” — Dkt Myles Munroe.

Kimakosa wengi wetu tuna amini kuwa na fikra za ukuaji ni ishu ya “mazoea”. Tamko kama “Mimi sio msomaji” au “mimi sio mtu wa semina” au chochote ambacho unajiambia wewe sio ndicho kinachofanya usikuwe kifikra. Nakuhakikishia hakuna aliezaliwa anasoma. Una mamlaka juu ya fikra zako kwahiyo unaweza kuwa msomaji, mkimbiaji au chochote utakacho. Habari njema ni kwamba mtu yoyote anaweza kuwa na fikra za ukuaji kama akitaka.

KUFUTA ULICHO JIFUNZA; watu wengi hawataki kubadilisha mahusiano yao ya muda mrefu kwasababu wanasema wanamjua mwenza wao na hawahitaji kujaribu vitu vipya. Misemo kama “Namjua mwenza wangu, anapenda nikifanya hivi” au “hichi ndo kinachofanyaga kazi kwenye mahusiano yetu” ndo sentensi zinazopelekea mahusiano kufika kusema “sijui kiliktokea nini, tulijikuta tu kama tumetengana” ila kilichotokea ni kwamba hukutaka kufuta ulichojifunza mwanzo kuhusu mwenza wako na hatimaye mkatengana. Tunahitaji kufahamu watu wanabadilisha vitu wavipendavyo muda wowote.

Usiwe kikombe kilichojaa. Kuna msemo “Kikombe kilichojaa hakihitajiki” hii ni kwasababu huweza kuongeza chochote kwenye kikombe hicho.

KUJIFUNZA TENA; tumesikia watu wakisema “mahusiano yapo hivi hivi kila siku” hayo ni maneno yanayo watoka watu ambao vikombe vyao vimejaa na ukiwa kikombe kilichojaa utampoteza mwenza wako kwenda kwa mwingine au utakuwa na huzuni na mtazamo hasi juu ya mahusiano yako.

Umeshawahi kujaribu kuongeza kiungo kwenye chakula unachokula kila siku, kama umewahi basi utakuwa ulisema “hivi kwanini sikufikiria hichi kabla?”. Fikiria mchakato huu kama hivyo.

Kukua ni mchakato usioisha.

Hata nyoka wanajivua ngozi yao baada ya muda kidogo ili wakue na kuondoa vijidudu waliojiambatanisha na ngozi yao ya zamani.

Kama Mwenza Wako Hana Fikra Za Ukuaji

Ni changamoto kuwa kwenye mahusiano na mtu asie na fikra za ukuaji kwakuwa inachosha kushusha viwango vyako ilikuwa nae sawa au kutumaini mwenza wako atapata fikra za ukuwaji na kujifanyia kazi. Vifyatavyo vinaweza kusaidia mahusiano yako kama yapo hivi.

Sala; mimi naamini “Sala hubadilisha kila kitu”. Sala inaweza kubadilisha fikra za mwenza wako lakini zaidi Sala inaweza kubadilisha mtazamo wako wewe ili kumkubali na kumpenda jinsi alivyo pasipo kujali fikra zake. Mark Batterson anasema “Sala hubadilisha kilakitu kutoka ndani mpaka nje”.

“Sala ndio tofauti kati ya kisichowezekana na kinachowezekana, Sala ndio tofauti kati ya kile tunaweza fanya na ambacho Mungu aweza fanya” — Mark Batterson

Ishi Unachosema; Kuwa mabadiliko unayotaka kuyaona kwenye mahusiano yako. Inabidi uwe unachotaka mwenza wako awe kwasababu ukifanya hivyo utakuwa unaongoza kwa mfano na kwa kuhamasisha na sio kwa hotuba na ushauri kitu ambacho kinaweza kufanya mwenza wako asitake kabisa kuwa hivyo.

Muache Aende Polepole; Mwenza wako anapoanza kuwa na fikra za ukuaji muache afanye kwa kasi awezavyo kwasababu huu mchakato hauishi kwa hiyo muache aende pole pole awezavyo na hata hivyo haijalishi kasi yake cha muhimu anasonga.

Jua Kinachochea Ukuaji Wake; Mume wangu alikuwa sio msomaji na huwa nilikuwa najaribu kumwambia asome lakini hiyo haikuwahi kusaidia. Mimi napenda kusoma vitabu vya ndoa & mahusiano, siku moja nilijaribu kusoma kitabu cha biashara na tukiwa tunapiga stori nae nikaongelea vitu nilivyo jifunza kutoka kwenye hicho kitabu sikushangazwa alivyofanya utafiti kuhusu hicho kitabu kwasababu yeye ni mfanya biashara, na aligundua kitabu hicho kina mlolongo wa vitabu vingine lakini nilishangazwa siku alipoenda kunua vitabu vyote 7 kwenye huo mlolongo wa hicho kitabu. Na sasa yeye anasema amekuwa kibiashara kwasababu ya hivyo vitabu.

Kinacho chochea ukuaji kwako sicho kinacho chochea ukuaji kwa mwenza wako.

Mimi na mume wangu tupo tofauti sana (napenda kujifunza zaidi kuhusu ndoa na mahusiano na yeye anapenda kujifunza zaidi kuhusu biashara) hivyo basi tuna siku ya kujifunza kila jumatano ambapo tunashirikishana tulichojifunza kutoka kwenye vitabu au video za kwenye mitandao ili wote tuweze kuwa na uelewa sawa kwenye mada tofauti. Hii inatusaidia kukua kwa pamoja katika mambo tofauti na pia inatuweka kuwa karibu zaidi.

Ndoa ni rahisi zaidi ikiwa wanandoa wote wa fikra za ukuaji.

Ndio maana ni muhimu kwa ambao bado hawana ndoa kujua ikija kwenye kuchagua mwenza wako wa ndoa, mapenzi pekee hayatoshi kuna mengi ya kuzingatia na kimoja wapo kikiwa fikra za ukuaji kwa mwenza wako.

Kwa Upendo,

Sandrahope M.

--

--