MUNGU AMETENDA

Sandrahope Msigwa
Love Shack
Published in
4 min readFeb 19, 2024

Ni Mungu tu anaeweza kubadilisha Shida kuwa UJUMBE, Mtihani kuwa USHUHUDA, Jaribu kuwa USHINDI, Mwathriwa kuwa MSHINDI.

Pale tu nilipofikiri kuwa nimeanza kufanya kazi na kukua kiafya kutoka kuwa mama wa nyumbani kwa mwaka na nusu na miezi 9 ya kabla ya hapo ya ujauzito wa kupumzika kwa kitanda (bed rest). Nikapata ujauzito mwingine ambao sikupanga kupata ila nilipenda kuwa nao na mara hii nikajua huenda ujauzito huu hautakuwa wa bed rest, nika anza kupata viashiria vya mimba kutaka kuharibika kwa hiyo ikabidi tu nikae tena nyumbani kwa ajili ujauzito huo wa bed rest lakini nikajiambia bora sasa hivi nimeshauriwa nikae bed rest miezi 5 ambayo sio muda mrefu kuliko ule ujauzito wa nyuma ambao ulikuwa miezi 7 kupumzika kwa kitanda kabisa na miezi 2 ya mwisho ambayo napumzika kwa kitanda kwa sehemu.

Katika mwezi wa pili wa huo ujauzito maumivu mgongo wa chini yalizidi na daktari akasema “unachokoza uchungu” huku akinipa elimu ya kuharibika kwa mimba, vifo vya watoto wakiwa tumboni mwa mama zao, na watoto waliozaliwa kabla ya muda. Inashangaza kuna muda mwingine kuzungumza na mtu ambae akachagua maneno hasi yanaweza kubadilisha moyo wenye matumaini kuvunjika, mazungumzo hayo yalinivunja moyo sana na kunipa msongo wa mawazo zaidi. Nilijihisi kama kuna kitu hakiko sawa kwangu kwasababu mbona mimi sina ujauzito mzuri na nyororo kama akina mama wengine, ni kwamba kila nikishika mimba zitakuwa za bed rest? na kujiuliza maswali ndiyo yalichimba shimo kubwa la msongamano wa mawazo mpaka nikaanza kuwa na fikra za kujiua, kifo na nilikuwa ninaota ndoto mbaya kila siku.

Ilichukua Maombi mengi sana kutoka kwa ndugu na marafiki wa karibu kutoka kwenye hilo shimo. Na pia maneno mengi ya kujitia moyo kutoka kwenye Neno la Mungu.

  1. Naweza kufanya yote kupitia Yeye anitiaye nguvu — Wafilipi 4:13
  2. Bado nina karama ya kuitumia kuhudumia — 1 Pet 4:10
  3. Mungu ana mipango mizuri, ya amani na yenye matumaini juu yangu — Yeremiia 29:11

Mahusiano yangu na Mungu yalinisaidia kupita katika kipindi cha kwanza cha ujauzito wa mapumziko lakini kiukweli baada ya hiyo miezi 5 sikukaa karibu sana Mungu kama nilivyokaa hapo mwanzo.

Nilivyofika miezi 6 ya ujauzito, nililazwa hospitalini kwa ugonjwa wa hyperemisis gravidarum ( ambao ni kutapika kupitiliza wakati wa ujauzito). Sikuipenda hii hali kabisa kiasi cha kwamba nilikuwa kila nikumuona mume wangu namwambia “Nakupenda sana ila huyu ni mtoto wa mwisho kwahiyo jitayarishe kuwa na watoto wawili tu” hii ilikuwa sentensi ya kila siku hadi kama siku sijamwambia lazima aniambie “leo kuna kitu umesahau kuniambia 😅”

Nilipofikisha miezi 7 nilipata dalili za kujifungua kabla ya muda na ilibidi nichome sindano za kusaidia kupevusha mapafu ya mtoto kama akizaliwa njiti na ilibidi nirudi tena mapumziko ya kitanda. Hapa sasa nikarudisha tena mahusiano yangu na Mungu kama yalivyokuwa.

Nilivyofikisha wiki 35 ya ujauzito huo ambao ni kama miezi 8 na wiki kadhaa, Nikapata dalili za mshono kuchanika kwa ndani kwasababu niliwahi kushika mimba baada ya kujifungua kwa upasuaji mara ya kwanza na hapa ikabidi tena kufanyiwa upasuaji wa dharula. Nashukuru ulienda vizuri lakini mwanangu Samantha alizaliwa na ugonjwa wa shida ya kupumua kwasababu mapafu yake yalikuwa bado hayaja pevuka.

Samantha alilazwa chumba cha joto, aliwekwa kwenye mashine ya oksijeni ili kumsaidia kupumua kwa siku 5, alinywehswa maziwa yangu niliyokuwa nakamua kwa mpira unaoptia puani kwa siku 6. Sikiruhusiwa kumnyonyesha kifuani kwangu na nilikuwa sina maziwa ya kutosha kwa kipindi kile nahisi kwasababu ya stresi za kuwepo hospitalini na msongo wa mawazo wa baada ya kujifungua. Ilikuwa ngumu sana kwangu kumuona katika maumivu na kutokuweza kumsaidia.

Nakumbuka ilifika kipindi ambacho nilikuwa sijui nisalie nini, nisalije na nilimuomba mume wangu, ndugu zangu, marafiki zangu kumuombea Samantha maana niliona sina maneno ya kuweka katika sala, nilikuwa nasema tu “Mungu, naomba tatua hili, naomba umponye”.

Nililia kila siku kule hospitalini. Nilijisi dhaifu lakini nilijua nguvu za Mungu zinafanya kazi bora kwenye udhaifu wangu. “Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu.” — ‭‭2 Kor‬ ‭12‬:‭9‬ ‭SUV‬‬

Kuna kipindi ambacho nilikata tamaa kabisa na nikahisi nitarudi nyumbani bila mwanangu na nikamwambia mume wangu na alifunga na kusali kwa ajili yetu na Mungu wetu mwaminifu alijibu sala zake siku hiyo hiyo Samantha aliendelea vizuri na siku iliyofata alitolewa katika mashine ya oksijeni.

Tunapopitia wakati mgumu shetani anaweza kutufanya tuhisi kama maumivu na shida hazitoisha na ata ikitokea usumbufu kidogo tu inaweza kuongeza maumivu zaidi kwenye maumivu ambayo tayari unayo lakini yote yataisha hatakama ni vigumu kuamini ila “Hamna Kinachodumu” maana yake ata maumivu uliyonayo sasa hayatodumu.

Biblia inasema katika Warumi 8:18 “Kwa maana nayahesabu mateso ya wakati huu wa sasa kuwa si kitu kama utukufu ule utakaofunuliwa kwetu.” Shikilia mstari huu kama unapitia majaribu.

Nashukuru Mungu leo mwanangu Samantha, jina lenye maana ya (Mungu amesikia) ametimiza mwaka mmoja. Hakika Mungu amesikia.

“Nalimtafuta BWANA akanijibu, Akaniponya na hofu zangu zote.” — ‭‭Zab‬ ‭34‬:‭4‬ ‭SUV‬‬

P.S: Kuhusu idadi ya watoto, labda nitajaribu mara 1 tena 😂. Natania! Nitakuwa na watoto idadi atakayo penda Mungu niwe nayo. “Moyo wa mtu huifikiri njia yake; Bali BWANA huziongoza hatua zake.” — Mit‬ ‭16‬:‭9‬ ‭SUV‬‬

Kwa Upendo,

Sandrahope M.

--

--