Undani Wa Kweli Ni Nini?

Sandrahope Msigwa
Love Shack
Published in
4 min readMar 15, 2024

Kuhisi Undani na Ukaribu Kwenye Mahusiano Yako

Undani ni hali ya kuhisi ukaribu wa kihisia na mwenza wako. Undani ni kiungo kikubwa cha kuwa na ndoa yenye furaha, ustahimili, ya muda mrefu na mahusiano bora. Undani ni kiwango cha juu cha ukaribu na uwazi kati ya wapendanao ambacho kinapelekea kuwa na uhusiano usiovunjika.

Undani ndio unaofanya wapenzi kuwa wenza wa roho. Kuwa na ukaribu wa aina hii na mtu umpendae inaweza kuwa zawadi kubwa sana kwenye mahusiano yenu.

Kutoka kwenye kitabu cha “Mahitaji 5 ya kimapenzi ya Wanaume na Wanawake” kilichoandikwa na Dr Gary na Barbara Roseberg. Waandishi hao wanasema wanawake wanafafanua undani kama “Maongezi” huku wanaume wakifafanua ukaribu kama “Tendo la Ndoa”. Na kwamba undani ni haja ya pili ya kimapenzi kwa wote wanaume na wanawake ya kwanza ikiwa upendo bila masharti.

Undani unachukua muda, juhudi & uvumilivu kujengeka na kudumisha. Undani usipodumishwa mahusiano yanapitia wakati mgumu. Kuna sababu tofauti zinazo pelekea undani kwenye ndoa kupotea kama; uzazi, malezi ya watoto, ubize wa maisha kupelekea umbali, msongo wa mawazo unaoletwa na mambo tofauti kama matatizo ya kazini, ya kifedha na wajibu nyinginezo.

Haijalishi sababu yenu ya kutokuwa na undani kwenye ndoa yenu ni nini, kukosa undani kunapelekea madhara kwenye mahusiano kama;

  1. Kukataliwa; mtu akijiskia hali ya kukataliwa na mwenza wake inapelekea yeye kujitenga na kutokea na kupelekea wenza kujihisi upweke kama hawapo kwenye mahusiano.
  2. Kutokujiamini; hii inatokana na kujisikia kama mwenza wako havutiwi na wewe tena ambayo inapelekea kutokujithamini pia.
  3. Chuki; kukosekana kwa ukaribu kunapelekea migogoro isiyoisha, vinyongo ambao inaleta hasira ata kwenye mambo madogo.
  4. Usaliti; sisi kama wanadamu tuna haja kubwa ya ukaribu na wenzetu sasa hiyo haja isipofikiwa na mwenza ndipo wengine wanapo anza kutafuta sehemu nyingine. Usaliti sio lazima uwe wa kimwili tu ata kihisia mtu anaweza kumsaliti mwenzie.

Mfano pale mwanamke anapojiskia kama hapendwi/hausikilizwi na mwenza wake anakuwa mrahisi sana kuingia mtegoni kwa mwanaume mwingine ambae ataonesha hata kusikiliza kidogo mawazo na hisia zake na vivyo hivyo kwa wanaume akikosa haja yake ya ukaribu anakuwa rahisi kuingia mtegoni kwa kutafuta tendo la ndoa au kutamani wanawake wengine au kuanza kuangalia ponografia. Sisemi kwamba ndoa yako ikikosa ukaribu basi ni sawa kutafuta kwingine au kumlaumu mwenza wako kwa madhara au matokeo hasi, ninacho kisema ni kwamba inafungua mlango kwa haya kutokea.

Noti: Wewe ndio una wajibu na maamuzi yako ya kimaadili.

Kama nyote hamjali ndoa yenu basi hamtojali kukosekana kwa ukaribu kunaweza kuleta madhara gani kwenye ndoa yenu na mtaishia kuwa na maadhimisho ya ndoa na sio ndoa nzuri yenye furaha ambayo Mungu alikusudia juu yenu.

Ukaribu ni muhimu ili ndoa iwe nzuri na nyororo. Kama ambavyo kifaa chako hakiwezi kupata intaneti bila kuunganisha data. Mahusiano hayawezi kuwa bora au kukua bila ukaribu na undani.

Ukaribu unaenda sambamba yani mwanamke asipopata maongezi anaanza kuona tendo la ndoa kama kazi na mwanaume asipopata tendo la ndoa inakuwa ngumu kwake kuungana na mke wake na kufanya mawasiliano na maongezi nae.

Ukaribu kwenye ndoa unategemeana. Wanaume wengi wanajibu haraka kihisia kama hitaji la kimwili likifikiwa na wanawake wanajibu haraka kimwili kama hitaji lao kihisia likifikiwa.

Unaweza Kufikia Hitaji La Mume Wako La Undani Kwa:

✅ Kutazama hali yenu kwenye kipengele cha tendo la ndoa ikoje na sehemu nzuri ya kuanzia ni kwenye maongezi na Mungu juu ya hilo. Utashangaa ambavyo unaweza kufunuliwa na kuona huenda ulikuwa unatumia haja ya mume wako kujinufaisha au ukiwa unahitaji kitu kwake, ukilijua hilo itakusaidia kujua wapi pakubadilika.

✅ Safisha Moyo Wako; ikiwa una maumivu yoyote kwasababu maumivu ambayo suluhishwa italeta ugumu katika kujifungua moyo na kimwili kwa mume wako.

✅ Jifunze Kinachomridhisha Mume Wako; tazama, muulize anachokipenda, na kinamfurahisha zaidi ikija kwenye haja yake ya undani.

✅ Jizatiti kufikia hitaji hilo; chochea penzi lenu, cheza na kutaniana na mume wako.

“Ndoa yenye tendo lake ambalo ni la kusisimua na kufurahisha ni sehemu ya mipango ya Mungu juu ya ndoa njema”, “Kutana na mume wako njia nzima sio nusu njia” — Dr Gary Roseberg.

Unaweza Kufikia Hitaji La Mke Wako La Undani Kwa:

✅ Kumsikiliza Mkeo; kwa umakini bila kuwa na mambo mengine akiwa anaongea na wewe na usijaribu kutatua tatizo lake kama hajaomba suluhu muda mwingi mwanamke anahitaji kusikilizwa tu atoe yaliyopo moyoni.

✅ Elewa Moyo Wake; hata kwenye kitu kidogo sana usimhukumu kwa maneno au mitazamo. Unaweza ukamuombea au ukaomba nae ili umuelewe zaidi. Anapokwambia vitu avipendavyo, aviogopavyo, vinavyomuumiza jitahidi kuelewa vinatokea wapi kwenye hisia zake hapa jitahidi usitumie logic nenda nae polepole kwenye mambo ya kihisia.

✅ Muoneshe unampenda; weka juhudi ya kumpa muda wako, mbusu, mkumbatie, msapraiz kwa kumtoa out na mpe zawadi azipendazo.

✅ Tatua Migogoro; migogoro ambayo haija tatuliwa inapelekea kuwa na umbali hivyo ikitatuliwa kunakuwa hamna kinyongo na kupelekea kuungana kihisia na mke wako.

✅ Jilinde na Linda Ndoa Yako; usiendekeze matani, kugusana, maongezi ya undani, kuchekeshana na wanawake wengine kwasababu haijalishi ni mema kiasi gani mke wako akijua ataumia sana na kuvunjika moyo na pia unaweza ukateleza na kuangukia mtegoni. Kama mke wako anakuonya kuhusu mwanamke fulani muamini kwasababu anajua urahisi kwa mwanaume kushika moyo wa mwanamke bila hata yeye kugundua/ kukusudia.

“Kama mwanaume anataka tendo la ndoa zuri chumbani kwake, basi inabidi ajue jinsi ya kuhusiana na mke wake nje chumba” — Barbara Roseberg.

Kama wapendanao wekeni juhudi za kutengeneza fursa za undani; tengeni muda kwa ajili yenu tu mbali na watoto kama mnao na wajibu nyingine na zingatieni mahusiano yenu na kuelewa kiundani zaidi haja ya ukaribu kwenu.

Hamjachelewa sana kwa wote kuamsha undani na ukaribu kwenye ndoa yenu.

Kwa Upendo,

Sandrahope M.

Rejeo:

“The 5 Love Needs of Men & Women” Kimeandikwa na Dr Gary & Barbara Roseberg.

--

--