Uzao Baada Ya Kuharibikiwa Na Mimba Kadhaa

Sandrahope Msigwa
Love Shack
Published in
2 min readFeb 6, 2024

Lakini Mungu kanitendea.

Ushuhuda Wangu

Nilitaka sana kuwa mama toka 2019 lakini sikujua kuwa watoto ni zawadi kutoka kwa Mungu na Mungu ndio anajua lini upo tayari kuwa mzazi na Mungu anajua mengi zaidi, Biblia inasema “Kichwani mwa mtu mna mipango mingi, lakini anachokusudia Mwenyezi-Mungu ndicho kitakachofanyika.” — ‭‭Methali‬ ‭19‬:‭21‬ ‭BHN

Niliharibikiwa na mimba mbili 2019 na moja katika mwaka 2020, mimba hizo zilizoharibika ziliniumiza sana kihisia, kiakili na kimwili. Iliniumiza kihisia na kiakili zaidi kwasababu nilihisi ni kosa langu lakini halikuwa kosa langu ilikuwa mipango ya Mungu.

Baada ya kuharibikiwa na mimba hizo nilitaka kuwa mama bado lakini nilikata tamaa hata kujaribu tena kushika mimba kwasababu kila nikipima nilikuwa sipati majibu ninayoyataka kuwa ni mjamzito. Kuna Sala hii niliandika katika App ya Biblia ya YouVersion

Niliandika Sala hii kwa ajili ya siku ‬‬maombi yangu yakijibiwa kwakuwa nilikuwa nina imani siku ya mimi kuitwa mama itakuja. Niliendelea kuomba kuna siku nika amua kufunga kwa maombi kwa siku tatu na nilipo maliza mfungo huo nilipopima nilikuta nimepata mimba.

Kwasababu ya kuharibikiwa na zile mimba za nyuma niliwekwa kwenye mimba ya kupumzika kwa kitanda (bed rest) kwa miezi sita na kuruhusiwa mapumziko ya sehemu kwa miezi mitatu. Kwa kipindi hiki nilikuwa kiimani nilitumia kipindi hiki kama Elisabeti kwenye kipindi cha mafichoni “Baadaye Elisabeti mkewe akapata mimba. Akajificha nyumbani kwa muda wa miezi mitano, akisema: “Hivi ndivyo alivyonitendea Bwana; ameniangalia na kuniondolea aibu niliyokuwa nayo mbele ya watu.” — Luka‬ ‭1‬:‭24‬-‭25‬ ‭BHN‬‬

Kuna muda nilikuwa najiuliza nitakuja kupata mimba kubwa had tumbo liwe kubwa?, nitasherekea kuzaliwa kwa mwanangu? nitakuja kushuhudia ata akitimiza mwaka mmoja? lakini moyoni nilijua Mungu analijua hitaji la Moyo wangu na anasema katika neno lake “Uitafute furaha yako kwa Mwenyezi-Mungu, naye atakujalia unayotamani moyoni.” — ‭‭Zaburi‬ ‭37‬:‭4‬ ‭BHN‬‬.

Leo hii nafurahi kusema mtoto huyu ana miaka 3 na pia ana mdogo wake wa mwaka 1. Mungu aliijua haja ya moyo wangu akanibariki na watoto wawili baada ya kupitia hili na kupitia mengine pia. Maumivu niliyopitia yamekuwa ushuhuda wangu.

Mungu hapotezi maumivu na hata wewe maumivu yako yatakuwa ushuhuda.

Naomba nikutie moyo leo kuwa chochote unachopitia, Mungu anakiona, anaona maumivu yako, Anataka ukue kupitie maumivu hayo na hawezi kukupa jaribu usiloliweza.

Ukiona imani yako haijakaa sawa basi kasome Waebrania 11 ili uweze kukua kiimani, muombe Mungu akuzidishie imani na amani unapopitia kwenye shida.

Kwa Upendo,

Sandrahope M.

--

--