Niliyojifunza Katika Miaka 5 Ya Ndoa
Ndoa ni safari iliyojaa mafunzo yasiotarajiwa. Kuwepo kwenye ndoa kwa miaka 5 kuna machache niliyojifunza kwetu na kwa wanandoa wengine ambayo yamejenga mtazamo wangu na ningependa kukushirikisha.
1. Matendo Yana Matokeo
Kila tendo lina matokeo liwe la muda mrefu au mfupi, hasi au chanya. Tunayowaambia na kuwafanyia wenzi wetu liwe jema au la kupuuzia, kusapoti au kuumiza inawaathiri na inaathiri ndoa kwa ujumla. Matendo chanya kama kuonyesha upendo, heshima, shukrani, sapoti, maelewano yanaimarisha ndoa lakini matendo hasi kama kutokuwa mwaminifu, usaliti, kutokuwa na heshima, kutokuzingatia hisia za mwenzi wako yanapelekea umbali wa kihisia, ndoa kukosa uaminifu, migogoro na talaka.
Rafiki zangu John & Jane wapo kwenye ndoa kwa miaka 10 sasa na mwanzoni mwa ndoa yao walianzisha biashara pamoja na kufanya vitu vyote kwa upamoja lakini baada ya miaka 7 ya ndoa yao John alianzisha familia nyingine nje ya ndoa hio, Jane alibaki kwenye ndoa baada ya John kuomba msamaha lakini haikuwa kama zamani, Jane alijianzishia biashara zake pembeni na kuanza kutafuta mali zake kisirisiri. Ndoa iliyo anza Mtazamo mmoja ilisambaratika nakuwa na maono tofauti ambacho kimefanya ndoa hiyo kutokustawi.
Mwenzi wako ni binadamu na ukimuumiza haswa kihisia tegemea kupata matokeo hasi kutokana na kosa ulilofanya. Ndiyo maana ni muhimu sana kuwa makini na tunachosema kwa mwenzi wetu au tunalofanya kwa mwenzi wetu.
Kila tendo lina matokeo, kabla haujafanya zingatia kitakacho kugharimu kwasababu maji yakishamwagika hayazoleki.
2. Migogoro Haikwepeki
Migogoro haikwepeki kwenye ndoa kwasababu kadri unavyozidi kuishi na mwenzi wako lazima mtapishana. Tunakosea na kufanya jambo liwe gumu zaidi pale ambapo tunajaribu kukwepa migogoro au tunapoanza hali ya mashambulizi kwa mwenzi wetu hali ambayo inapelekea mwenzi wetu nae kuanza kujitetea au na yeye kushambulia pia. Kutokuelewana ni sehemu ya kila ndoa kwasababu tunatofautiana kihisia, kimaslahi na kibinadamu.
Ni muhimu kuelewa jinsi mnavyotofautiana na mwenza wako ili kuweza kuchukuliana katika ndoa.
Kila tatizo lina suluhu. Mnahitaji kuchunguza nini kilienda vibaya na kukisuluhisha kabla hamjachelewa zaidi kwasababu migogoro ambayo haikusuluhishwa kabla huwa ndio inajirundika na kupelekea milipuko ya hasira na maumivu kwenye ndoa.
Kitu kikubwa na kizuri unaweza kufanya kwa ajili ya ndoa yako ni kujifunza jinsi ya kufanyia kazi masuala yenu kivyenu.
Migogoro inapotokea na hasira inapozidi ni heri 1. Kujipa muda kidogo wa kupoa kisha kuongea vizuri baadaye kuhusu tatizo liko wapi? Au lilianzia wapi?, huenda tatizo ni la nyuma kidogo na mpaka hilo lisuluishwe hamuwezi kusonga mbele. 2. Sikiliza upande wa mwenzi wako; najua hili ni gumu haswa ukiwa unahisi umekosewa, mimi pia likinikuta naomba kwa Mungu anisaidie kusikiliza na inasaidiaga kwa kuwa kuna pande mbili katika kila stori. 3. Kama umekosea kiri na kama ulikosewa kisha ukakabiliana na hilo suala vibaya kiri pia. 4. Jifunzeni katika hilo kosa, sameheni kisha songeni mbele.
3. Kusamehe Sio Rahisi
Kusamehe ni rahisi kwa maneno lakini sio rahisi kwa vitendo. Wanandoa lazima wataumizana kwenye maisha ya ndoa hivyo kupelekea kusamehe kuwa kitu kigumu na pia kurudisha upendo, uaminifu ni ngumu pia.
Pamoja na ugumu wa kusamehe, lakini hiyo ndiyo njia pekee ya kusonga mbele kwasababu hakuna ndoa isiyo na makosa au kipindi cha maumivu. Bila kusamehe ndoa huharibika kwa chuki na makosa ambayo hayajasamehewa. “Upendo hauhesabu mabaya” — 1 Kor 13:5 SUV.
Kusamehe haimaanishi kusahau kilichotokea lakini kuchagua upendo, kujiponya na kujenga yajayo kuliko kung’ang’ania uchungu na maumivu. Kusamehe kunachukua muda na haitokei siku moja lakini ni muhimu sana kwa furaha ya muda mrefu na uponyaji wa ndoa.
Ndoa njema ina muunganiko wa wasameheaji wawili
4. Majeraha/Mapito Ya Nyuma Yana Athiri Ndoa
Majeraha ya mapito yanayotokana na matukio ya kuhuzunisha. Majeraha hayo yapo aina tofauti na kila mtu ana ya kwake mfano majeraha katika ukuaji, ukatili / unyanyasaji wa kijinsia, kuzaa, kutelekezwa utotoni, ajali, majeraha ya kuomboleza, kushuhudia mauaji, maafa na mengineyo.
Baba yangu aliondoka na kutuacha mimi na mama yangu nikiwa nina miaka 5 na alituambia anasafiri kikazi atarudi baada ya miezi 3 lakini haikuwa kweli alirudi baada ya miaka 12 na kwa miaka yote hiyo tuliwasiliana si zaidi ya mara 5 hata alivyorudi hakurudi kwetu. Baada ya kuolewa, mume wangu alikuwa akipata safari za kikazi napatwa hofu ya hilo jambo kujirudia na kwasababu nilikuwa sijawahi kuunganisha matukio hayo basi sikuweza kukabiliana na hilo vizuri, kitu ambacho kilikuwa kinapelekea migogoro ndani ya ndoa yetu.
Mume wangu amekuwa akiona wazazi wake wakiwajiuguza ugonjwa wa kisukari kitu ambacho kilimfanya awe makini na kufanya mazoezi na kula vyakula vya afya sasa akiniona nakula vitu ambayo sio vya kiafya huwa anaongea sana kitu ambacho kilikuwa kinafanya nihisi kama kuhukumiwa kwa kufanya kitu nikipendacho ambapo pia ilikuwa inapelekea mikwaruzo midogo mindogo.
Ilituchukua muda mrefu sana kuelewa kuwa migogoro ilikuwa miitikio ya mapito yetu. Uzuri tulipata muda wa kutafakari, na kuongea kwa kina na ukweli, tulijua pia vichochezi na mapito mengine lakini pia tulitenga muda wa Sala kitu ambacho kilitusaidia sana katika kuelewana zaidi.
Wewe na mwenzi wako mnaweza kujaribu kuandika vitu 3 ambayo ni majeraha ya nyuma kisha kulinganisha na mambo yanayo endelea kwenye ndoa yenu na hatimaye kupata muda wa kuyaongelea kiundani zaidi.
Nimeona pia ndoa nyingi ambapo wanandoa wanaendesha ndoa zao kama walivyo ona ndoa za wazazi wao zikiendeshwa, kitu ambacho hupelekea migogoro sana kwenye ndoa zao. Somo kubwa la kujifunza ni kwamba hakuna ndoa inayofanana kwasababu kila mtu ni wa kipekee kwa hiyo hata kwenye ndoa ni hivyo hivyo. Mungu analeta wawili pamoja akiwa na dhumuni na mpango ambao ni zaidi kuridhisha mahitaji ya kihisia, kimwili na kiakili.
Hakuna ndoa zinazofanana, ndoa zinaweza kuwa na vitu vinavyo endana lakini zina utofauti mkubwa.
5. Mawasiliano Ni Ufunguo
Mawasiliano ni ufunguo ili kutengeneza mahusiano bora. Mawasiliano bora yanasaidia katika kuelewana, kueleza mahitaji yako kwa uhuru, kutengeneza undani, ukaribu, kuheshimu mipaka, kusulihisha migogoro. Mawasiliano bora yanafikika kwa kuanza na kutaka kumuelwa mwenzi wako kabla ya mwenzi wako kukuelewa wewe, kuchukuliana, kuanzisha mipaka na kuepuka kudhania.
Kutokuwasiliana kuna achia nafasi ya kudhani ambayo inapelekea migogoro.
Kutokuwasiliana na migogoro ndio chanzo kikubwa cha milipuko ndani ya ndoa. Maamuzi makubwa au madogo msipo shirikishana inapelekea pia migogoro na kutokuelewana, pia hata hisia, hofu na vya zamani yasipo wasilishwa vizuri yanapelekea migogoro.
6. Huwezi Kumbadilisha Mwenza Wako
Kosa kubwa nililofanya mwanzoni mwa ndoa yetu ni kufikiria kuwa naweza kumbadilisha mume wangu na yeye anaweza kunibadilisha mimi ila si kweli hatuwezi kubadilishana kwasababu mabadiliko yanayo dumu yana anzia ndani. Hata mimi nilipokuwa nikijaribu kubadilika kwasababu yake mabadiliko hayo hayakudumu kwasababu kubadilika kwa ajili yake haikuwa sababu sahihi ya mimi kufanya mabadiliko.
Kubadilika kwa ajili Yako ndio mabadiliko yanayodumu.
Ni Mungu tu anayeweza kutufungua macho katika mambo tunayo hitaji kubadilika. “Ndiyo maana ni muhimu kusali sala ya “Ee Bwana, Badilisha Tabia Zangu”, Naelewa ni sala ngumu lakini ni bora kuliko “Ee Mungu, Baadilisha tabia za Mwenzi Wangu”- Stormie Omartian. Tukiamua kumuachia Mungu afanye apendalo ndani yetu, tuta shangazwa na atakalo lifanya.
Mume wangu asipo okota nguo chafu chini ni rahisi zaidi mimi kuokota na kuziweka kwenye tenga la nguo chafu kuliko kuanza kulalamika na kupelekea migogoro isiyo na misingi wakati ni kitu naweza kumsaidia kufanya.
Kwenye ndoa jifunze kuchagua vita yako. Hayo mauzi / mapungufu ya mwenzi wako hayatoisha hivyo basi chagua utaiitikia nini.
Ndoa ni kumkubali mwenzi wako kama alivyo, mazuri yake na mabaya yake. Kuliko kuzingatia katika kumbadilisha ni bora kufanyia kazi kuelewana, kusapotiana na kuhimiza ukuaji bora.
7. Ndoa sio 50/50
Ndoa inahitaji kufanyiwa kazi na wanandoa wote. Ndoa haitakiwi kuwa “natoa 50% na wewe toa 50%” ijapokuwa kiuhalisia kuna muda mwenza mmoja anatoa 70% huku mwingine 30% na hii inaweza kuwa kwasababu ya ubinafsi au sababu zilizo nje ya uwezo wa wanandoa lakini bado ni jambo la kusuluhisha ili kuepuka ndoa kuwa mbaya inabidi wanandoa wote watoe 100%.
Ndoa ni jukumu la pamoja ambalo linahitaji kazi ya timu. Timu inahitaji ushirikiano ambao ni muhimu na inafanya mwenza ahisi kusikika, kuthaminiwa na kuungwa mkono. Kazi ya timu inaenda zaidi ya ushirikiano, ni kuwa na malengo ya pamoja (ya kiroho, kifedha, ukuaji, kimwili), majukumu yaliyofafanuliwa vizuri (ya kibinafsi na ya kimahusiano, mwelekeo wazi, mipaka, sheria, uwajibikaji wa pande zote, utofauti, mawasiliano ya kweli na huru, maamuzi ya pamoja, utatuzi wa migogoro na uaminifu.
8. Ndoa Ni Sadaka
Ugumu wa ndoa pia unatokana na kuwa ndoa inakuhitaji kutokuwa mbinafsi. Mara nyingi inatubidi tuipe kipaumbele ndoa zetu kabla ya maslahi yetu binafsi kwa ajili ya ustawi wa mwenzi wetu au familia.
Wanandoa wote hawatikiwi kuwa na ubinafsi ila wanatakiwa kufikiria zaidi kujitolea kwa upendo na heshima na si kwasababu wanawajibika kufanya hivyo ili kuepuka chuki.
Ndoa njema ni ile yenye wanandoa wawili wanaopenda kuhudumia na sio kuhudumiwa.
Kutokuwa mbinafsi haimaanishi kuwa unapuuzia mahitaji yako. Ndoa njema ina usawa kati ya kutokuwa mbinafsi na heshima ya pamoja. Usawa huu unafanya ndoa kuwa ya viwango vya juu kwa kuwa kufanya wanandoa wote kuhisi kuthaminiwa, kupendwa, kuheshimiwa, furaha na kusapotiwa.
9. Msiache Kuchumbiana Na Mwenzi Wako
Nimejifunza ambavyo ni rahisi kwa ule utamu wa mahusiano kupotea katika ndoa. Kuna kipindi mimi na mume wangu tuliacha kabisa kufanyiana mambo mazuri ikapelekea hata tenki za hisia zetu kuwa tupu kitu kilichopelekea migogoro ya kila siku. Kiukweli kwa hicho kipindi hata furaha ya ndoa haikuwepo. Ilitubidi tuanze upya na hali ilibadilika baada ya kuanza kuhudumiana kwa moyo wote tena.
Ukiacha wewe na Ndoa Yako Inajiacha.
Kile mlichokuwa mnakifanya wakati wa kuchumbiana au wakati wa fungate msikiache. Msiache kupeana muda, zawadi, kutoka out, kutaniana, msiache kuambiana “Nakupenda”, chochote kilicho kuwa kikiwapa furaha.
Ndoa ambayo wanandoa wanaendelea kuchumbiana ina manufaa makubwa kwa watoto (kama mnao), kwasababu upendo mlionao unasaidia kuwakuza watoto katika mandhari tulivu na yenye afya. Upendo kati ya wanandoa ukiwa imara inaathiri vyema watoto kwakuwa wanashuhudia upendo na ulinzi ambacho kinapelekea ustawi bora wa kihisia kwa kaya nzima na pia inasaidia huko mbeleni watoto kujua nini cha kuangalia wakiwa wanatafuta wenza wao.
Pia inahuzunisha dunia tunayoishi sasa wajane ni wengi na wana achwa wakiwa wapweke mapema sana. Kuna mwimbo wa Meghan Trainor & John Legend — Like I’m gonna loose You (Kama nakupoteza). Kuna sehemu waimbaji hao wanasema “Hatuja ahidiwa kesho, nitakupenda kama vile nakupoteza, nitakushika kama nasema kwaheri, kokote tutakapo kuwa sitakuchukulia poa kwasababu hatujui lini tutaishiwa na wakati”.
“Nimejifunza kuwa nina mengi ya kujifunza” — Maya Angelou
Ndoa ni safari ya mwendelezo ya kujifunza na kukua. Hata waliopo kwenye ndoa kwa miaka mingi bado huendelea kujifunza. Na inabidi tuendelee kujifunza kwa kuwa sisi kama binadamu tunabadilika kila baada ya muda, tunapitia mapito tofauti katika maisha, tunajifunza kutokana na makosa, tunajigundua upya na tunaelewana kiundani zaidi.
Asante kwa kusoma makala hii mpaka mwisho, ni vizuri kuona unathamini kuendelea kujifunza kuhusu ndoa na maisha.
Kwa Upendo,
Sandrahope M.