Katika Kipindi cha Covid-19 watoto wa kike walipata athari gani?

WanaData
WanaData Africa
Published in
7 min readNov 2, 2020

Na Jackline Kuwanda, Dodoma, Tanzania

Octoba 2020

Tanzania ni miongoni wa nchi barani Afrika ambazo zilikumbwa na ugonjwa wa Covid-19.

Licha ya ugonjwa huo kusababisha mdororo wa uchumi kote ulimwenguni, watoto wa kike ni miongoni mwa makundi ambayo yaliathiriwa janga hilo ikiwemo ukatili wa kingono kama vile kubakwa, kupewa mimba, mashambulio ya aibu na kuendelea.

Thelesia Mdendemi, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi na wa la Jinsia na Watoto Mkoani Dodoma anakiri kuwa ni kweli katika kipindi cha korona watoto wa kike walikumbana na athari nyini.

“Ninaposema ukatili wa kingono ni masuala yale yote yanayohusisha mambo ya kingono kwa mfano watoto wengi walibakwa, kulawitiwa, kupewa mimba, mashambulio ya aibu, kujaribu kubakwa hizo bughuza nyingine za kiongono kwa mfano mashambulio ya aibu kujaribu kubakwa na vitu vinavyo fafanana hivyo na kibaya zaidi watoto wengi walikatishwa ndoto zao kwa hiyo sababu,’’ Thelesia alieleza.

Thelesia anabainisha kuwa katika kile kipindi cha mwanzo ambacho walikuwa wamefungua shule walikuwa wakipokea watoto watano kwenye shule moja wakiwa wamepewa ujauzito.

“Matukio haya yameendelea kuripotiwa hadi sasa unaona idadi inakuwa kubwa tofauti na pale awali kwa hiyo kutokana na kipindi kile ambacho walikuwa hawaendi shule walikosa kitu kile ambacho kingewafanya wawe. Tunajua kwamba kwa sasa hivi wazazi wengi wanaondoka asubuhi wanarudi jioni kwa sababu ya kuwahangaikia hao watoto. Sasa kutokana na wazazi kuwahangaikia watoto wakati ule nyakati za mchana watoto wakajikuta wako huru kwa hiyo wakawa wanaweza kufanya kitu chochote kutokana na hilo wengi wamewza kupata ujauzito,’’ Thelesia alieleza.

Anasema kipindi kile ambacho walimu walikuwa hawako na wanafunzi, wanafunzi ni kama walijilea wenyewe kutokana na wazazi wengi majukumu yao wakati huo. Kisha ikasababisha watoto wa kike kuwa na mimba zisizotarajiwa.

“Shule ni sehemu ya malezi. Walimu wanaporudia rudia baadhi ya mambo wanawakumbusha watoto pia. Ila mtoto anapokuwa nyumbani malezi ya sasa ni tofauti kidogo. Kwa sababu hiyo yamekuwa nusu. Wazazi wao wanafikiria kwa ajili ya kuhudumia familia na kutoa vitu vya msingi kwa watoto na wanasahau jukumu lao la malezi kama wazazi,” Thelesia alieleza.

Afisa wa Maendeleo ya Jamii katika Wilaya ya Bahi Mkoani Dodoma, Monica Chosongela, anasema changamoto kubwa ambayo wameiona katika jamii kwa wakati huo ni kuongozeka kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa watoto wa kike kama vile ubakaji, ulawiti wa watoto, mimba za utotoni na ndoa za utotoni.

“Kipindi hicho kwa sababu watoto wengi walikuwa majumbani na kama tunavyojua ulinzi wa mtoto kwa asilimia kubwa shule zinapokuwa zimefunguliwa mtoto anatumia muda mrefu sana akiwa shuleni tunaamini kuwa walimu ndio huwalinda lakini katika kipindi ambacho wako nyumbani kuna uzembe ambao wazazi wanaufanya na watoto wanakuwa huru mitaani. Kwa kipindi hicho ukatili wa kijinsia umekuwa ni mkubwa lakini pia maswala ya ndoa za utotoni yametokea kwa kiasi kikubwa. Ukizingatia kwa sasa wazazi wanaondoka asubuhi kurudi jioni kwa hivyo ukatili wa aina hiyo umekuwa mkubwa kutokana na maisha jinsi yalivyo kuwa kwa sasa,’’ Chisongela alieleza.

Sara Mwaga, Mkurugenzi wa Shirika la AFNET linaloshughulika na haki za wanawake, watoto, ukatili wa kijinsia, Afya ya uzazi, na ujinsia Utawala Bora amesema anakiri kutokea kwa changamoto nyingi kwa watoto wa kike katika kipindi cha korona.

“Kuna kesi tulisikia ya kijana ambaye aliwapa mimba dada zake wawili kwa wakati mmoja. Hiyo ni kwa sababu kipindi hicho walikuwa wamekaa nyumbani kama unavyojua vijana kwa kukosa uangalizi wakajikuta wanajiingiza katika vitendo vya ngono. Lakini wasichana wengine walibakwa na kunajisiwa na ndugu wa karibu. Wengine na wazazi. Mimba ziliongezeka lakini kwa taarifa zisizo rasmi nimezipata kwa mfano Wilaya ya Chamwino, zaidi ya watoto themanini (80) wa shule za msingi na sekondari walipata ujauzito katika kipindi cha korona kwa hivyo athari ni kubwa,” Sara alieleza.

Kwa upande wa Wilaya ya Tarime Mkoani Mara, kama anavyoeleza Afisa Mradi wa Jukwaa la Utu wa Mtoto (Children’s Dignity Forum — CDF), Jovitha Alphonce anasema watoto wa kike walipitia changamoto mbalimbali ikiwemo baadhi yao kupata mimba, kutoroshwa huku akibainisha kuwa kulingana na taarifa iliyotolewa na polisi kwa kipindi cha miezi minne hadi juni mimba zilikuwa zaidi ya kumi na saba (17).

“Hizo ni kesi ambazo zimeripotiwa katika kituo cha polisi, lakini pia kulikuwa na kesi 25 za ubakaji kwa kipindi cha mwezi wa nne na wa sita, lakini pia kulikuwa na kesi 36 za kutorosha wanafunzi ambazo zote hizo zimetolewa na polisi,” Jovitha alieleza.

Anasema tofauti na kesi ambazo zimeripotiwa polisi wao CDF kwa kushirikiana na watoa huduma, Idara ya Ustawi wa Jamii na Afya waliweza kuwasaidia watoa huduma kwenda vijijini kule ambako ni maeneo ambayo wamekuwa wakifanyia kazi hivyo waliweza kukutana na kesi mbalimbali ambazo hazijaripotiwa za ukatili wa kijinsia.

“Kulikuwa na kesi za ubakaji 34, kesi za kutorosha wanafunzi 35, ukatili wa kimwili 25 na 34 za watoto kuzurura mitaani. Kwa hivyo tunaona kuwa katika kipindi cha korona watoto wa kike walikuwa na athari kubwa,’’ Jovitha alieleza zaidi.

Akieleza sababu zilizosababisha vitendo hivyo kutokea wakati huo ni kutokana na wazazi kushindwa kutimiza wajibu wao wa kuwalinda wao. Katika kipindi kile waliamini kwamba wazazi watakuwa mstari mbele katika kutimiza majukumu ya watoto wao lakini haikuwa hivyo wengi walikuwa wanaendelea na makumu yao.

Bibi mmoja anayepatikana Mkoani Dodoma amenieleza kisa kilichomtokea mjukuu wake wa shule ya msingi inayopatikana Mkoani hapa. Mjukuu wake alikumbana na changamoto hiyo ya ukatili wa kijinsia baada ya kubakwa na kijana mmoja mwenye umri wa miaka kumi na saba.

Kwa mujibu wa taarifa aliyopokea kutoka kwa mamake msichana, binti huyo alikumbwa na janga hilo alipokuwa akimtafuta mdogo wake, aliyekuwa haonekani nyumbani muda wa saa tatu usiku. Hapo ndipo alipokutana na kijana huyo ambaye alimshika mkono na kumvutia kwenye pori dogo na kumfanyia kitendo hicho.

“Katika kumbaka akapiga kelele watu walisikia na kwenda katika eneo hilo kama ambavyo mama yake alivyokuwa akinieleza. Baada ya majirani kuenda kule, kijana huyo alikimbia. Baada ya kukimbia, watu wale walichukuwa jukumu na kumpeleka mtoto nyumbani kwao. Muda si muda mama yake alirudi nyumbani na akaelezwa kilichomtokea mtoto wake. Kilichofuatia ni walienda kwa balozi usiku huo huo kisha wakaenda polisi usiku na kumpeleka mtoto hospitali na alikutwa kweli amebakwa,’’ alisema.

Mmoja wa walimu wa shule ya Sekondari kutoka Jijini Dar es salaam anasema katika kile kipindi ambacho watoto walikuwa nyumbani walikuwa hawashughulikiwi na wazazi watoto walikuwa huru hivyo kwa baadhi ya maeneo hasa kwa watoto wa kike walijikuta wanapata ujauzito.

“Sisi hapa hatujapata kesi hiyo lakini kuna baadhi ya maeneo kutokana na watoto kuwa huru zaidi walijikuta wakipata mimba kwahiyo wengine hajaweza kurudi tena shule nilisikia mfano wa baadhi ya wilaya huko watoto walipata ujauzito katika ile likizo ya Covid-19 hiyo ni athari lakini sasa watoto walivyorudi shuleni kwa watoto wa kiume na kike walikuwa wazito sana kwenye kusoma,” amesema.

Naye Mwalimu wa Shule ya Msingi Dodoma Mlimani iliyopo Jijini Dodoma, Godfrey Abel, anasema hakuna kesi iliyojitokeza shule kwao juu ya wanafunzi kupata ujauzito ama kufanyiwa vitendo vya ukatili. Baadhi ya watoto wameshindwa kuendelea na masomo yao kutokana na vishawishi mbalimbali ambavyo vimewapeleka kushindwa kuendelea na masomo yao ikiwemo kubeba ujauzito katika kipindi kile cha likizo ya korona. Kuongezea, alisema wakati ule pia baadhi ya jamii walitumia mwanya wa korona kuwakeketa watoto.

“Kwa sababu watoto walikuwa nyumbani na baadhi wao walikuwa huru walirubuniwa na ikapelekea baadhi yao kupapata mimba ,unajua watoto wanapokuwa wanaenda shule wanaepukana na vishawishi mbalimbali tofauti na wanavyokuwa nyumbani lakini baadhi ya jamii walitumia likizo korona kuwakeketa wanafunzi wa kike,’’ alisema.

Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Mbogi iliyopo Tarime Mkoani Mara, Bhoke Chacha, (si jina lake halisi) anasema wasichana walikumbana na vitendo vya ukatili lakini baadhi yao kupata ujauzito katika likizo ya korona.

“Mimba walipata wengi tu! Nadhani jambo hili la upatikanaji wa mimba lifuatiliwe kwani wengi walikuwa wanasema kwamba sababu ya watoto wa kike kupata mimba inatokana na umasikini hivyo kupelekea wasichana kujiingiza katika vitendo vya kingono,’’ amesema.

Kwa upande wa Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Dodoma Mlimani Elizabeth David anasema katika shule yao hakuna mwanafunzi ambaye amepata ujauzito lakini kwa shule nyingine wapo ambao walipata ujauzito katika kipindi cha corona na yote ni kutokana na wazazi kuwaaacha huru watoto pasipo kuwa na uangalizi mzuri wakatio huo.

“Kipindi cha korona asilimia kubwa watoto wa kike walipata mimba. Kwa mfano kuna wazazi walikuwa wanaendelea na shughuli zao ikawapa watoto wao huru wa kujiiingiza katika makundi mabaya. Makundi hayo yalichangia kwa kupata ujauzito kwa watoto wa kike. Katika shule yetu hakuna ambaye amepata mimba,” alisema.

Kwa mujibu wa tamko lililotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Lilian Liundi Mwezi, April 2020, Kuhusu virusi vya korona na athari zake kwa wanawake na watoto wa kike alieleza kuwa watoto walikuwa katika hatari ya kupata mimba za utotoni.

Alisema takwimu zinaonesha kuwa takribani asilimia 60 ya vitendo vya ukatili wa kijinsia hutokea majumbani na wanaofanya vitendo hivyo ni ndugu wa karibu au majirani.

Aliendelea kuongeza kuwa ukatili wa kijinsia huongezeka sana wakati wa majanga kama hayo, si tu kwa watoto bali pia kwa wanawake.

Alibainisha kuwa Taarifa kutoka nchi za China, Ulaya na Marekani zilionesha kuongezeka kwa matukio ya ukatili wa kijinsia toka Covid-19 ilipoanza. Kwa mfano, taarifa za polisi nchini China zilionesha kuwa ukatili wa kijinsia uliongezeka mara tatu katika kipindi cha janga la korona ndani ya mwezi Februari pekee.

Lakini kwa mujibu taarifa zilizotolewa na Shirika la Kimataifa linalo hudumia wanawake la (UN Women) Ulimwenguni, linakadiria kuwa wanawake na wasichana milioni 243 wenye umri kati ya miaka 15 hadi 49 wamefanyiwa unyanyasaji wa kingono na / au kimwili Mwaka jana.

Linasema kuwa takwimu zilizojitokeza zinaonyesha kuwa unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana uliongezeka tangu kuzuka kwa Covid-19.

Wazazi kukosa muda wa kuwa karibu na watoto katika kipindi cha korona nayo imetajwa imetajwa kuwa sababu moja wapo ya baadhi ya watoto wa kike kukumbwa na vitendo vya ukatili na hata wengine kupata ujauzito kutokana na watoto hao kuwa huru.

Mpaka sasa kwa Tanzania hakuna takwimu halisi zinaonesha kuwa ni athari zipi ambazo walizipata watoto wa kike katika kipindi cha Covid-19 lakini kulingana na mahojiano ambayo wahusika wameelezea inaonesha kuwa ziko baadhi ya athari ambazo watoto wa kike walizipitia wakati huo.

This story was first released on Maisha FM, Dodoma on 31st October, 2020. Listen to this story on SoundCloud.

Hadithi hii iliungwa mkono na Kanuni ya WanaData Initiative ya Afrika, Twaweza na Kituo cha Pulitzer juu ya Kuripoti Majanga.

This story was supported by Code for Africa’s WanaData Initiative, Twaweza and the Pulitzer Center on Crisis Reporting.

--

--