Huduma za Mtandao zalemazwa huku Wakenya wakiandamana kupinga Mswada wa Fedha

Benchi Kuu Dotcom
5 min readJun 26, 2024

--

Ilani ya kampuni ya Safaricom kwa wateja kuhusu kukatika kwa mtandao. Picha kwa hisani

Siku moja tu baada ya Mamlaka ya mawasiliano nchini Kenya (CA) kuwahakikishia Wakenya kuhusu kutokuwepo kwa mpango wa kukatizwa kwa huduma ya mtandao ili kulemaza jitihada za maandamano ya vijana wa kizazi kipya — almaarufu Gen Z, yanayolenga kupinga Mswada tata wa fedha uliopendekezwa na serikali, Wakenya waliweza kukumbwa na tukio la kukatizwa kwa huduma hiyo.

NetBlocks, shirika la uangalizi linalofuatilia usalama na utawala wa mtandao, lilithibitisha kukatizwa huko katika chapisho kwenye akaunti ya X (Zamani Twitter): Twakimu ya mtandao ya moja kwa moja inaonyesha ukatizwaji mkubwa wa muunganisho wa Intaneti nchini Kenya; tukio hili linatendeka huku kukiwa na msako mkali wa polisi dhidi ya waandamanaji wa #RejectFinanceBill2024 siku moja baada ya mamlaka kudai kuwa hakutakuwa na uzimwaji kwa mtandao.

Kampuni ya Masawasiliano inayoongoza nchini, Safaricom, ilijitokeza na kudhibitisha hili kupitia ilani kwa wateja iliyochapishwa kwenye akaunti yake ya X. Ilani hiyo ilisema kuwa hali hii ilisababishwa na kukatika kwa nyaya za chini ya bahari zinazowasilisha trafiki ya Intaneti ndani na nje ya nchi.

Watumiaji wa X nchini Kenya walijitokeza kwenye jukwa kulalamikia kupungua kwa kasi ya mtandao, huku baadhi yao wakilitilia swala hili shaka, wakisema kuwa huenda ilikuwa ni njama ya Safaricom kuisaidia serikali kulemaza maandamano yaliyokuwa yakiendelea mnamo Jumanne.

Mtumiaji @MathuAlfred alisema: Kuwa na VPN imefanya (hali) iweze kudhibitiwa kidogo lakini mtandao bado unajikokota na sio wa kutegemewa.

Mtumiaji @LORDMWESH: Kinaya ni Safaricom, kampuni kubwa zaidi ya mawasiliano nchini Kenya kutangaza kuzimwa kwa mtandao kupitia mtandao wa X.

@JustRosalyn, mtumiaji wa X na mshawishi maarufu wa mitandao ya kijamii: Mpo kitanda kimoja na serikali wapuzi nyie.

Hata hivyo, sio Kenya tu iliyoathiriwa na ukatizwaji huu wa mtandao.
Nchi jirani kama vile Uganda na Burundi ziliathirika pakubwa pia.
Katika nchi hizi jirani, nguvu ya muunganisho wa mtandao iliripotiwa kupungua hadi 47%, huku muunganisho huo nchini Rwanda ukipungua hadi kufikia 78%.
Nchi hizi tatu wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), zinategemea nyaya za chini ya bahari zinazopitia nchini Kenya.

Waandamanaji wanaopinga mswada walizidi kupambana na polisi jijini Nairobi na miji mingine nchini. Jijini Nairobi, Maandamano hayo yaligeuka mabaya zaidi huku bunge la Seneti likivamiwa na sehemu moja ya bunge hilo kuchomwa moto, hali iliyositisha kikao cha bunge kilichokuwa kikijadili mswada huo (ambao tayari umepitishwa na bunge la taifa). Wabunge hao walilazimika kutorokea eneo salama la Bunge Towers, jengo lenye afisi za wabunge, kupitia njia ya chinichini huku waandamanaji hao wakifanikiwa kupenyeza Bunge kwa muda kabla ya polisi kupambana nao na kuwafurusha kutoka jengoni humo.

Uvamizi huu wa Bunge ulipelekea mamia ya waandamanaji kuuawa na kujeruhiwa kulingana na duru za kuaminika kutoka vyombo vya habari nchini.

Akiliongelea suala la maandamano, Jaji Mkuu Martha Koome, mnamo Jumanne alielezea wasiwasi wake mkubwa kuhusu kutekwa nyara kwa waandamanaji nchini. Koome alisema vitendo hivyo vinavyotekelezwa na watu wasiojitambulisha na bila kuwasilisha watu waliotekwa nyara mbele ya mahakama ya sheria, ni sawa na ukiukwaji wa moja kwa moja wa utawala wa sheria, haki za binadamu na ukatiba.

“Katiba yetu ya Mabadiliko inaamuru kwamba utekelezaji wa sheria ufanye kazi kikamilifu ndani ya mipaka ya Sheria ya Haki na sheria.” “Ibara ya 49 inabainisha haki za watu waliokamatwa, ikiwa ni pamoja na haki ya kufahamishwa sababu ya kukamatwa, kuwasiliana na wakili na watu wengine ambao msaada wao ni muhimu, na kuwasilishwa mahakamani haraka iwezekanavyo-na sio baada ya masaa ishirini na nne baada ya kukamatwa,” alisema.

Jaji Mkuu huyo alisisitiza kuwa mashirika yote ya serikali ndani ya sekta ya haki yanapaswa kuzingatia majukumu yao ya kikatiba na kuhakikisha kuwa matendo yao yanafuata Katiba na sheria.

Kwenye tamko la pamoja, mabalozi wa nchi za Muungano wa Ulaya, na nchi ya Marekani waliunga mkono usemi wa Jaji Mkuu Martha Koome.
Pia walielezea wasiwasi wao kuhusu vurugu zilizoshuhudiwa nchini wakati wa maandamano. Mabalozi hao walikaribisha ushirikiano wa kiraia na Wakenya wote, haswa vijana, katika kushughulikia maswala muhimu ya umma.

Kupitia taarifa ya Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) Moussa Faki kuhusu hali nchini Kenya, AU iliwataka wadau wote kuwa watulivu na kujiepusha na ghasia zaidi. Vile vile, AU ilitoa wito wa kuwepo kwa mazungumzo dhabiti ili kusuluhisha maswala tata yaliyosababisha maandamano hayo kwa maslahi ya juu ya Kenya.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres naye alisema: “Nimesikitishwa sana na ripoti za vifo na majeruhi — ikiwa ni pamoja na waandishi wa habari na wafanyakazi wa matibabu — kuhusiana na maandamano ya mitaani nchini Kenya.”

Kwenye taarifa yake, Waziri wa Ulinzi nchini Aden Duale alitangaza kuwa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) litatumwa kusaidia Huduma ya Kitaifa ya Polisi katika kukabiliana na dharura ya usalama iliyosababishwa na maandamano yanayoendelea.

Rais mstaafu Uhuru Kenyatta naye hakuachwa nyuma. Rais huyo wa zamani alituma rambirambi zake kwa Wakenya waliopoteza maisha wakati wa maandamano ya Jumanne akisema ni haki yao ya kikatiba kupiga kura.

“Ninakuja kwenyu nikiwa na huzuni kubwa ya kupoteza maisha kutokana na hali ya sasa nchini. Ni haki ya Wakenya kuandamana kama ilivyoamuliwa na Katiba ya Kenya 2010. Pia ni wajibu wa viongozi kuwasikiliza wanaowaongoza,” Uhuru alisema.

Aidha Uhuru alitoa wito wa utulivu na kuwataka viongozi kukumbatia mazungumzo na wananchi.

“Kama rais wenu wa zamani nimehisi uzito wa kuwaongoza Wakenya. Kwa hivyo naomba hekima na ustaarabu uimarishwe na amani na maendeleo yawe yetu sote kama watoto wa Kenya,” alisema.

Rais huyo mstaafu alithibitisha uungaji mkono wake kwa Wakenya na kuwataka viongozi “wazungumze na kuwasikiliza watu na sio kuzungumza bila kuwasikiliza.”

Akivunja ukimya wake kupitia mkutano na waandishi wa habari kutoka Ikulu ya Nairobi Jumanne jioni, Rais William Ruto — Zakayo kwa jina la utani, alitaja maandamano ya hivi majuzi ya kupinga mswada wa fedha kuwa ‘uhaini’ na kuviagiza vikosi vya usalama kuhakikisha usalama wa Wakenya wote.

Rais Ruto aliapa kuchunguza matukio yaliyosababisha waandamanaji kuvunja majengo ya Bunge na kuwaonya wale aliowataja kuwa wafadhili wa machafuko hayo.

Kwa kuwa uko hapa…

Iwapo umeyapenda makala haya na ungependa kuona maudhui zaidi ya Kiswahili kwenye blogu hii na au chaneli yangu ya YouTube, tafadhali fuata, penda, shiriki maoni, na iwapo itakupendeza pia, unaweza kunichangia tipu ya 50€ na au ujiunge nami kama mhisani kwa kiasi cha 200€ tu ili uniwezeshe kuendelea kujitolea muda wangu kuandika makala yenye kusisimua na yanazoelimisha.

Paypal yangu: bswitaba [at] yahoo.co.uk

Zingatia: Wahisani watapewa shukrani na sifa sufufu

--

--

Benchi Kuu Dotcom

Kitovu Cha Midahalo Muhimu kuhusu: Maisha, Historia, Utamaduni na Miondoko - hususan kwa wapenzi wa lugha ya Kiswahili, Kiingereza na Kireno