“#SikilizaTogolani”: Kwa nini tutumie ‘msuli’ ilhali njia rahisi ipo wazi kabisa?

Chambi Chachage
6 min readJan 28, 2021

Ni andiko lenye matumaini. Waraka uliojaa uponyaji. Ujumbe wa kututia moyo sisi sote ‘tuliodogoishwa’ na kunyanyasika kwa sababu ya Kiingereza.

Nazungumzia makala ya #SikilizaTogolani: “Usikate Tamaa, hata Waliozaliwa Uingereza nao Hujifunza Kiingereza” iliyochapishwa humu jana na Togolani Mavura. Kwa hakika anastahili pongezi zote. Hata yule gwiji wa uandishi, Shaaban Robert angekuwepo leo ninaamini angesema, heko gwiji Togolani!

Pongezi kemkem zinazidi kumiminika kutoka kila kona mathalan kutoka kwa mwandishi mahiri wa Kiingereza, Elsie Eyakuze, anayesisitiza kwamba laiti angekuwa mwalimu angehakikisha makala hayo yanasomwa na wanafunzi wa ngazi za juu. Na wito umetolewa ichapwe kwenye majarida ya kimataifa.

Kwa namna ya kipekee kabisa Togolani ameelezea changamoto ambazo kwa kiasi kikubwa watoto wengi wa Kitanzania waliosoma enzi zake walizipitia. Katika andiko hilo kuna sehemu anasema kwa dhati na uchungu yafuatayo:

“Sina shaka kuwa simulizi yangu si ya kipekee kabisa. Wengi wana simulizi tena za kusisimua sana za uhusiano wao na Kiingereza. Wengine wana simulizi chungu sana. Wako ambao kimewaengua katika usaili (interview), kimewafelisha kwenye mitihani, ama kimewakosesha fursa mbalimbali.”

Pasi na shaka tuna simulizi nyingi. Ninaamini simulizi ya Togolani itakuwa chachu ya kutuchochea wengi wetu tusimulie yaliyotusibu katika safari hiyo ndefu iliyojaa miiba ya mbigili na ukakasi wa majani ya mchunga. Japokuwa kimsingi huwa ninatofautiana na Togolani kuhusu suluhisho la kudumu la janga hili la kitaifa, naamini andiko lake lina chembe chembe za ufumbuzi.

Moja ya Machapisho Muhimu kuhusu Mjadala wa Lugha ya Kufundishia

Hali kadhalika naamini tukiweka tofauti zetu za namna ya kufumbua tatizo hilo tutaona kwa nini Profesa F.E.M.K. Senkoro anakiita kile ambacho wale ambao hawakuweza kuvuka ng’ambo ya pili kuwa ni ‘MAUAJI YA HALAIKI’ ya Watoto wa Tanzania Kupitia Lugha ya Kufundisha Sekondari na Vyuoni. Kabla Togolani hajauvuka kwa kasi mto huo uliojaa mamba hali yake ilikuwa hii:

“Katika darasa langu lile, tuliokuwa hatuna mazoea na Kiingereza katika kuongea hatukuzidi 5. Waliobaki wengi walitoka shule ambazo Kiingereza alikuwa mwenyeji. Wengi walishacheza nae na walikua naye. Nikiri kuwa nilipata unyonge sana. Nikawa kimya sana siku za mwanzoni.”

Togolani anaongelea Kidato cha Tano hapo juu katika shule niliyogoma kusoma Kidato cha Kwanza kisa nilitaka kusoma shule ambayo kumbe na yeye alisomeshwa pale pia, yaani Azania Sekondari. Kwa maana nyingine, pamoja na kusoma kwa miaka minne katika shule ya Umma/Serikali bado alikuwa hajavuka ule mto hadi alipoenda kwenye shule ya ‘Kulipia/Binafsi’ ambako ndipo hasa safari yake ya ‘kukimanya Kingreza’ ilipata ‘mwendokasi’.

Chambi Chachage akiwa amebeba Kitabu cha Kujifunzia Kiingereza Azania Sekondari

Kwa hiyo isitushangaze kuwa waliokuwa na nakisi ya “mazoea na Kiingereza katika kuongea” hawakuzidi 5 katika shule hiyo ya ‘kishua’. Bahati nzuri au mbaya tumepishana miaka michache, hivyo Azania aliyoipitia Togolani na niliyoipitia mimi hazina tofauti sana. Elimu ilikuwa inapitia bonde la uvuli wa mauti. Ni zama za migomo ya walimu na wanafunzi kuingia kwa zamu mbili.

Chambi Chachage na Wanafunzi Wenzake wa Azania Enzi Hizo za Uhaba na Migomo ya Walimu

Wanahistoria machachari wa Tanzania watakuambia hizo zilikuwa ni zama za mwanzo za ubinafsishaji wa elimu. Kupata tu nafasi Kidato cha Kwanza kwenye shule kama Shaaban Robert au Mzizima ilikuwa si mchezo na kukijua Kiingereza kulisaidia sana. Na huko ndiko Togolani anapakumbuka kihivi:

“Pale nikakutana na Walimu wa kutoka India kipindi hicho ambao hawakuwa wakijua Kiswahili. Kwao Kiingereza walifanikiwa kukijua mpaka kukibadilisha na lafudhi.”

Ghafla Togolani akaanza kufundishwa Kiingereza na masomo mengine kwa Kiingereza na walimu wanaokijua Kiingereza. Na huo, kama wanavyosisitiza Mwalimu Richard Mabala na Profesa Martha Qorro mara kwa mara, ndiyo msingi mkuu wa kufundishwa lugha ngeni au ya pili ama hata ya tatu na nne.

Lakini kwa kuwa nia kuu ya waraka wa kiponyaji wa Togolani ni kututia moyo kuwa hata tuwe na walimu ‘wabaya’ ama mbinu ‘mbovu’ au vifaa ‘vibovu’ vya kujifunzia Kiingereza na masomo mengine bado tunaweza kuwa ‘wasongo’ na kupiga ‘msuli’ tu na ipo siku tutafanikiwa kusema Kiingereza chetu “si haba.”

Ila ninajiuliza na kumuuliza Togolani kwa nini tutumie ‘msuli’ hivi ilhali kuna njia fupi tu na mbinu rahisi zaidi ya kufundishwa na kujifunza Kiingereza? Ni lazima tujifunze lugha hii kwa ‘mtulinga’ na bila furaha? Kwa nini safari zetu ziwe na machungu kama haya hapa chini aliyoyapitia pia katika safari yake?

“Mimi na kiingereza tumekuwa na urafiki wa muda mrefu usiopungua miaka 35. Urafiki wetu umekumbana na mitihani mingi na mashaka mengi. Kumekuwepo na kusalitiana, kuumbuana, kunafikiana na hata kuchukiana nyakati zingine….Siku moja…dingi…alirejea kutoka kazini na magazeti yake, kama kawaida nikanyoosha mkono kuchukua gazeti la Uhuru nisome zangu habari za siasa na michezo. Baba akaninyang’anya lile gazeti na kunipatia gazeti la Daily News ambalo limeandikwa kwa lugha ya rafiki yangu Kiingereza. Kusema ukweli, siku ile niliambulia patupu. Niliweza kutambua maneno machache na viunganishi tu kama ‘the’, ‘and’, ‘of’ na ‘that’. Mara nisikie joto, mara jasho, mara kuwashwa mwili, alimradi tu. Kiingereza akanitia aibu tena mbele ya baba.”

Jana niliposoma nukuu hiyo hapo juu nikakumbuka jinsi dingi alivyonishukia alipoziona tu makala zangu tatu za Kiingereza nilizotaka kuzipelekea gazetini nikiwa mwanafunzi wa sekondari. Baba alishangaa ni jinsi gani niliandika tu Kiingereza ‘kilichovunjika’. Makala mojawapo binamu yangu aliihifadhi na kuichapa kwenye blogu yake ya Amkeni miaka mingi baadaye, unaweza leo kujionea jinsi gani pamoja na uhariri wa hapa na pale bado ilikuwa na nakisi.

Yote hiyo ilikuwa ni kukura kakara za kujitahidi kubobea katika Kiingereza. Kwa kiasi fulani zimezaa matunda. Ndiyo maana namuelewa sana Togolani na makala yake ya kuwapa pumziko wale wote wasumbukao na kuelemewa na mzigo mzito mno wa kujifunza Kiingereza katika mazingira magumu ya elimu yetu. Naelewa pia kwa nini haoni kutumia lugha ya Kiswahili kujifunza kwa furaha masomo mengine huku tukifundwa Kiingereza ndiyo mwarobaini.

Rai ya gwiji Togolani ni kuwa kamwe tusikate tamaa. Kiingereza ni lugha tu kama Kiswahili chetu ‘pendwa’. Inachohitaji ni mazingira ‘wezeshi’ kama vile vitabu, magazeti, watu wanaokijua wa kuongea nao shuleni na hata mitaani.

Cha kuzingatia sana ni kuwa, pamoja na hayo yote, Togolani bado alitambua umuhimu wa kufundishwa Kiingereza na wataalamu wa kukifundisha kama somo na/au lugha rasmi. Hakuamua kuchukua tu ile ile njia ndefu ya kuvuka milima na mabonde kutoka Forodhani. Siku ya siku huyo bila soni akajongea kwa hao magwiji wa lugha hiyo kutoka kwa Malkia wa Uingereza namna hii:

“Sikuona aibu, nikaenda kujiandikisha kusoma Kiingereza cha Kuandika Rasmi (Professional English Writing Skills) pale British Council Dar es Salaam.”

Aibu hutukosesha mengi kama Taifa. Na kiburi pia. Kama kile cha kuona ni heri tu walimu na wanafunzi wapige ‘msuli’ wee wakati kuna njia rahisi ya kukijua Kiingereza. Matokeo yake hadi maprofesa wetu wanataabika kama yule Togolani wa Azania. Pengine hawakupiga ‘msuli’ wa kutosha kama yeye.

Jitihada binafsi ni muhimu. Ila siyo mbadala wa juhudi za kitaasisi. Na kisera.

--

--